Mapato ya utalii yavunja rekodi ya tangu uhuru

Meneja Miradi ya Maendeleo Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Marcel Leijzer akizungumza na waandshi wa habari. Picha Mussa Juma

Arusha. Mapato ya sekta ya Utalii nchini  yamevunja rekodi  ambayo haijawekwa tangu nchi kupata uhuru baada ya kuingiza Dola 2.99 bilioni ambazo ni zaidi ya Sh5 trilioni.

Mapato hayo ambayo yametolewa na Benki Kuu nchini (BOT) ni hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu na yanatokana na watalii 1.6 milioni kuingia nchini.

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas ametoa taarifa hiyo leo Septemba 27, 2023 wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yaliyofanyika jijini Arusha.

Dk Abbas amesema ongezeko la mapato hayo ambayo, limetokana na kazi kubwa ya kutangaza Utalii wa Tanzania iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya Royal Tour.

“Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Programu ya The Royal Tour amefanya kazi kubwa ametembea maeneo mbalimbali kutangaza vivutio vya utalii sambamba na wadau wa sekta ya utalii,”amesema.

Amesema kutokana na mapato hayo, Serikali imepata fedha lakini pia wadau wa sekta ya utalii nao wamepata fedha.

"Hivyo leo tunapokutana katika maadhimisho haya tunapaswa kufurahi na kupongezana," amesema.

Hata hivyo, amesema kazi kubwa ambayo inapaswa kuendelea kufanywa kuendelea kutangaza zaidi vivutio vya utalii ikiwepo mazao mapya ya Utalii kama Utalii wa utamaduni, michezo, tiba na mengine.

"Tanzania kwa muda mrefu tumekuwa tukitegemea utalii wa wanyamapori, hifadhi, misitu na bahari lakini kuna utalii mwingine unaweza kuleta mapato mengine," amesema.

Awali Meneja wa Ushirikiano wa Miradi ya Maendeleo wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), Marcel Leijzer amesema Tanzania inaweza kufanya vizuri zaidi pia katika utalii wa utamaduni.

Amesema Tanzania kuna makabila mengi, yamejaliwa kuwa na tamaduni mbali mbali ambazo zinaweza kuwa kivutio kizuri na endelevu cha utalii.

"Serikali inapaswa kubainisha utalii huo wa utamaduni ikiwepo kuwajengea uwezo wanajamii ambao wanaweza kuendeleza utalii huu," amesema.

Akitoa mada kuhusu matumizi ya technolojia za kisasa katika kukuza na kutangaza utalii, Jnine Wencke amesema, kwa dunia ya sasa wadau wa sekta ya utalii ni lazima wajifunze kutumia teknolojia za kisasa.

Amesema technolojia hizo ni pamoja na kutumia akili bandia (AI) ambapo inasaidia kufanya kazi mbalimbali ikiwepo kuandika baruapepe, kutegeneza matangazo ya biashara na kujitangaza.

“Akili bandia huduma zake ni bure na haihitaji gharama kupata huduma mbali mbali hivyo ni muhimu kuelekea huko katika kutangaza Utalii,”amesema.

Maadhimisho hayo yameratibiwa na Chama cha Mawakala wa Utalii (Tato) Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Chuo cha Uhasibu Arusha na taasisi nyingine za Utalii barani Afrika.