Nchi 38 kushiriki maonyesho ya utalii Arusha
Muktasari:
- Maonyesho hayo ya Kimataifa ya utalii ya Karibu KiliFair, kampuni zaidi ya 370 za utalii kutoka nchi 12 duniani watashiriki maonyesho hayo yanayotarajiwa kuanza jijini Arusha,Juni 2 hadi Juni 4, 2023.
Arusha. Wanunuzi wa utalii kutoka nchi zaidi ya 38 duniani wamethibitisha kushiriki maonyesho ya Kimataifa ya utalii ya Karibu KiliFair, yatakayofanyika katika viwanja vya Magereza jijini Arusha kuanzia Juni 2 hadi 4, 2023, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri mwenye dhamana ya utalii.
Akizungumzia maandalizi ya maonyesho hayo leo Alhamisi Mei 18, 2023, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kilifair Promotion, ambao ndiyo waandaaji wa maonyesho hayo, Dominic Shoo, amesema maonyesho hayo yatafunguliwa na Waziri wa Utalii na Maliasili, Mohamed Mchengerwa.
Maonyesho hayo ambayo yatafanyika kwa mara ya pili baada ya kusitishwa kwa miaka miwili kutokana na janga la Uviko-19, yanategemea kuvutia washiriki kutoka Afrika Mashariki na wanunuaji kutoka masoko ya kimataifa.
Amesema kuwa wanunuzi hao watatembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo hapa nchini ambapo pia kampuni zaidi ya 370 kutoka nchi 12 wamejiandikisha kushiriki onyesho hilo hivyo itakuwa fursa ya kuendelea kutangaza vivutio vya utalii.
"Kupitia onyesho hilo tunalofanya kila mwaka tumefanikiwa kuleta watu zaidi ya 500 kutoka mataifa mbalimbali duniani ambao tunaamini wamekua mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini," alisema Shoo.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Utalii Tanzania (Tato), Henry Kimambo amesema lengo la kukutanisha wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi ni kufanikisha azma ya serikali ya kufikisha watalii milioni tano ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege Tanzania (ATLC), Patrick Ndekana, amesema wataendelea kutoa mchango wa kuchagiza sekta mbalimbali za kiuchumi nchini ikiwemo ya utalii.
"Kwa sasa soko la China limefunguka na sisi tunaenda kule mara tatu kwa wiki, hivyo hii ni fursa kwetu sisi wadau wa utalii kuliangalia hili soko kwa jicho la karibu sana, maonyesho haya yawe chachu ya kufungua na kuvutia watalii toka China," Amesema.