Bendera ya China chini ya Xi Jinping kupepea zaidi duniani
Rais wa dola na pia kiongozi wa chama tawala cha kikoministi nchini China, Xi Jinping
Rais wa dola na pia kiongozi wa chama tawala cha kikoministi nchini China, Xi Jinping anaweza kubakia kuwa rais wa maisha. Bunge la nchi hiyo wiki iliyopita liliondosha kikomo cha muda wa wadhifa wa urais.
Hadi mabadiliko hayo, wadhifa huo ulikuwa umewekewa kikomo cha mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja.
Wabunge 2,958 waliyaunga mkono mabadiliko hayo ya mwanzo ya Katiba tangu kupita miaka 14 sasa. Wabunge wawili walilipinga pendekezo hilo, na watatu wengine hawakupiga kura. Kura moja iliharibika.
Lakini, katika mitandao ya kijamii mabadiliko hayo yalisababisha malalamiko, watu wakipinga kurejeshwa mtindo wa utawala wa Kaizari, hasa wa kumvalisha Xi Jinping kofia mbili za urais wa nchi na mkuu wa chama.
Zaidi ya hayo, pia kuwa mkuu wa majeshi. Watu wanaanza kuingiwa na wasiwasi na enzi hii mpya inayochomoza nchini China ya Ujamaa ulio na Sura ya Kichina, msamiati uliotiliwa mkazo hivi sasa ndani ya utangulizi wa Katiba ya nchi.
Pia, ina maana kwamba wapinzani wa Xi sasa wanaweza kuchukuliwa kuwa ni wenye kuipinga katiba.
Bingwa wa taaluma za siasa huko Hong Kong, Willy Lam, alilalamika kwamba hali hii mpya ni kuirejea nyuma China katika enzi ya Mao Zedong.
Hivi sasa Xi hana tena upinzani. Ni kutokana na sababu hiyihiyo, ndio maana mwaka 1982, miaka michache baada ya nchi hiyo kujifungua kiuchumi, ndipo kuliwekwa kikomo cha muda wa kukamata urais wa nchi.
Hilo lilikuwa somo lililotokana na mapinduzi ya kitamaduni na pia kutokana na maafa ya mfumo wa utawala wa mtu mmoja (Mao Zedong) ulioitumbukiza Jamhuri ya Umma wa China ndani ya fujo.
Katika miongo ya miaka iliyopita, China imeshuhudia utaratibu wa kupokezana uongozi ambao uliruhusu kubadilishana nyuso za viongozi wa dola na chama kila baada ya kipindi cha miaka kumi.
Kwanza kukabidhiana madaraka kwa njia ya amani kulitokea mwaka 2002 pale Jiang Zemin aliporejea nyuma na kumpa nafasi ya urais mrithi wake, Hu Jintao. Yeye naye aliyaacha madaraka mwaka 2012 na kumkabidhi Xi Jinping.
Na kila mara pale uongozi ulipokuwa mpya ndipo mfumo wa utawala ulipokuwa kijana zaidi. Mabingwa wengi walihoji kwamba hiyo ndiyo sababu mfumo wa utawala wa China umekuwa madhubuti, jambo linalowapa hoja ya nguvu watu wanaounga mkono mabadiliko haya ya sasa ya katiba.
Katika mkutano wa waandishi wa habari kwenye ukumbi mkubwa wa umma, Shen Chunayao, mkuu wa kamati ya Sheria ya Bunge, alisema wadhifa wa mkuu wa chama hauna mpaka wa muda kama ilivyo cheo cha mkuu wa Kamisheni ya Kijeshi. Kwa hivyo inaingia akilini kwamba kikomo cha muda wa urais kiondoshwe. Imeonekana ni busara kwa kofia zote tatu- mkuu wa nchi, mkuu wa chama tawala na mkuu wa majeshi zivaliwe na mtu mmoja. Watangulizi wa Xi, (Hu na Jiang) walivaa kofia zote tatu.
Pia, Jumapili ya wiki iliyopita iliamuliwa kuingizwa ndani ya katiba ya nchi kifungu kinachohusiana na kuundwa Tume mpya ya Usimamizi ambayo itakuwa huru na Mahakama au Ofisi ya Kuendesha Mashtaka na ambayo pamoja na tume ndohgo kama hizo katika ngazi za wilaya itapambana na rushwa na ufisadi, kutoendeshwa uzuri utumishi wa umma na dharau zilizoenea katika kutekeleza malengo ya kisiasa yaliyoamuliwa. Wafanya kazi wote serikalini watahitaji kufuata amri za tume hizo- kutoka mameneja wa mashirika ya umma hadi waalimu wa vijijini. Tume hizo zinaweza kuendesha uchunguzi, kumkamata mtu anayeshukiwa, kufanya upelelezi na kutoa adhabu. Kwa vitendo vya kihalifu mshukiwa baadaye atakabidhiwa kwa mwendesha mashtaka. Hivyo katika siku zijazo Wachina watachunguzwa nyendo zao.
Kila mwaka maelfu ya wanachama wa chama tawala cha Kikoministi cha China wananaswa kutokana na makosa ya kutoa na kupokea rushwa. Tangu Xi alipokamata madaraka mwaka 2012 idadi ya makosa ya aina hiyo yamezidi kuripotiwa. Naye Xi anaiendeleza kampeni yake dhidi ya rushwa kwa mkono wa chuma. Katika hotuba zake hadharani anapinga vikali mtindo wa uchumi wenye kutoa “bahashishi” ambao unaendeshwa na “nzi” (makada wadogo) na”chui” (makada wenye nguvu). Maelfu ya makada wamebidi wafukuzwe kazi na ushindani wa kibinafasi makazini umepungua. Xi Jinping hugawa nyadhifa za kazi kama njugu, kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa kutoka kwa watangulizi wake mnamo miaka 40 iliyopita.
Suala la mamlaka yote kuweko tu mikononi mwa mtu mmoja limewashughulisha sana wasomo kwa miaka mingi tangu enzi na dahari, na hasa katika madarasa ya taaluma za siasa. Kuna hoja kwamba haifai kuyajaza madaraka yote kwa muda mrefu ndani ya mkono wa mtu mmoja ayatekeleze peke yake bila ya kudhibitiwa, au ndani ya kikundi kidogo cha watu fulani. Kuna hatari kubwa ya hali hiyo kupelekea kuchomoza utawala wa kidikteta na madaraka kutumika vibaya, kuzuka usultani na watu kupendeleana na kuoneana. Pia, kuna hatari ya watawala wa juu kutumikia maslahi yao tu ya kibinafasi, kutimiza ndoto zao kwa kuwabinya na kuyasahau maslahi jumla ya raia.
Bila shaka, utulivu na uthabiti wa dola ni lengo muhimu la kila utawala, lakini isisahaulike kwamba “urais wa maisha” si jambo zuri, ni mtindo unaopelekea “jamhuri” kuwa si thabiti, inaweza ikateleza haraka.
XI Jinping ni Biblia mpya ya Mao Zedong. Miaka ya sitini na sabini tulizowea kusikia “ Yaishi Mawazo ya Mao”, na leo Wachina wanaambiwa wasifu “ Fikra za Xi zenye Ujamaa wa Sura ya Kichina” na zilizoingizwa ndani ya katiba ya nchi. Hata hivyo, Wachina wasilisahau lile Genge la Watu Wanne, (akiwemo ndani yake pia mkewe Mao) ambalo lilisababisha kuangamia maelefu kwa maelfu ya Wachina, wengi wao wasomi, wakati wa Mapinduzi ya Kitamaduni katika miaka ya sitini. Wasisahau pia kwamba mamilioni ya wananchi wa kawaida wa China waliangamia kwa njaa katika kampeni ya Mao ya kuanzisha Vijiji vya Ujamaa. Wachina wasifanye makosa walioyashuhudia zamani, na yote yalitokana na “kumuabudu” mwanasiasa kama “Mungu”. Kumfananisha binadamu/mwanasiasa kama Mungu ni hatari, tena kubwa.
Wachunguzi wa mambo wanafahamu kwamba mara nyingi hata kama midomo ya watu inazibwa na watu kushindwa kufurukuta kisiasa, lakini watu haohao pale matumbo yao yanapojaa wanakuwa kimya, kwa muda. Na ndivyo ilivyo China hivi sasa. Wachina hawana sababu nyingi za kulalamika kwa sasa- labda kukosa kuvuta hewa ya uhuru tu. Lakini, uhuru wa kuishi na kushiba wanao. Uchumi wa nchi yao unapanda kwa asilimia 6.5 kwa mwaka, mabarabara makubwa, viwanja vya ndege na njia mpya za reli zanajengwa; deni la nchi linapungua na serikali ina akiba kubwa ya fedha za kigeni, hasa dola za Marekani, na inawekeza kwa wingi nchi za nje. Waziri mkuu Li Keqiang amehakikisha kwamba hatari zote za kiuchumi au kifedha kwa China zinaweza kudhibitiwa.
Wachina wanaonesha misuli yao ya kijeshi nje ya mipaka ya nchi yao. Mwaka huu wa 2018 bajeti yao ya kijeshi itapanda kwa asilimia 8.1, ambapo mwaka jana ilikwenda juu kwa asilimia 7.1. Xi Jinping anasonga mbele kwa haraka kulifanya jeshi la nchi yake liwe la kisasa kabisa, na hasa analipa umuhimu jeshi la majini.
Jambo hilo ni muhimu katika juhudi za kutafuta Ukubwa wa kuidhibiti Bahari ya Kusini ya China. Hata hivyo, China iko mbali sana kufikia kiasi cha fedha zinazotumiwa na Marekani kwa ajili ya jeshi lake. Mwaka 2018 Washington ilitumia dola bilioni 800 kwa shughuli zake za kijeshi.
Ilivyokuwa sasa Xi Jinping yuko usukani huko Beijing, tena milele, isifikiriwe hata kidogo kwamba bendera ya China itasita kupepea katika kona yeyote ya dunia. Dunia ya nguzo mbili – ile ya Marekani na Urusi- imekwisha zamani, tangu miaka ya thamanini. Pia, dunia ya nguzo moja tu, yaani ya Marekani, imetoweka.
Sasa ni dunia ya nguzo nyingi, muhimu ya nguzo hizo ni China. Kama China iko tayari kuubeba mabegani mwake uzito mkubwa wa dunia iliyobaki, hilo ni jambo la kusubiri na kungoja.