Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bobi Wine aruhusiwa kwenda Marekani

Muktasari:

  • Baada ya kuzuiwa Alhamisi na Ijumaa kushinda hospitalini hatimaye aliruhusiwa usiku kwenda Marekani

Kampala, Uganda. Hatimaye Mbunge wa Kyadondo Mashariki Robert Kyagulanyi maarufu kama Boni Wine ameruhusiwa kuondoka nchini kwenda Marekani kupatiwa matibabu maalamu baada ya kuteswa na maofisa usalama alipokuwa kizuizini katika gereza la kijeshi la Makindye.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Emilian Kayima alisema Ijumaa mchana Bobi Wine na mwenzake wa Mityana Francis Zaake waliokuwa wamezuiwa kuondoka Alhamisi wameruhusiwa kuondoka.

Taarifa za kuondoka kwa Bobi Wine zilitolewa Jumamosi na mwanasheria wake Nicholas Opiyo ambaye pia alifafanua matibabu yake.

Kwamba tofauti na wabunge wengine ambao matibabu yao hugharimiwa na Bunge baada ya kupata idhini ya Bodi ya Matibabu ya Uganda Bobi Wine atajigharimia mwenyewe.

“Atajigharimia mwenyewe mara atakapowasili Marekani. Hatujapata mawasiliano na yeyote kwamba kuna mtu atamlipia lakini maisha yake ni muhimu zaidi kuliko fedha kwa hiyo amechukua kila senti kwa ajili ya kupata matibabu bora,” alisema Opio.

Bobi Wine, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na fani yake ya muziki wa reggae kabla ya kujitosa katika siasa mwaka mmoja uliopita, Ijumaa yote alikuwa amelala kwenye hospitali ya serikali alikopelekwa baada ya kukamatwa kwenye uwanja wa ndege wa Entebbe akisubiri kwenda nje kwa matibabu.

Bobi Wine, mwenye shahada ya muziki alifanikiwa kuwa mbunge mwaka 2017, akiungwa mkono na vijana na kuwa mwiba mkali Rais Yoweri Museveni ambaye umri unamtupa mkono.

Agosti 13, Bobi Wine na wanasiasa wengine walikamatwa, wakateswa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini. Mkasa uliosababisa wanasiasa hao na wafuasi wao wakamatwe ni madai kuwa moja ya magari ya msafara wa Rais Museveni lilipigwa mawe na kuvunjwa kioo cha nyuma muda mfupi baada ya kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa Arua.

Kukamatwa kwa Bobi Wine kuliibua ghasia na maandamano na jumuia ya kimataifa ililaani kuteswa kwake pamoja na Zaake alikuwa anatarajiwa kupelekwa India.

“Bobi Wine aliondoka usiku karibu saa 5:00 kwa ndege ya Shirika la Ndege la KLM kuelekea Schipol (Amsterdam) ambako ataunganisha ndege kwenda Marekani,” alisema Opiyo. “Ameongozana na mkewe Barbie na kaka yake Daks Sentamu.”

Baada ya kuachiwa kwa dhamana Jumatatu, Kyagulanyi alikamatwa tena na polisi Alhamisi jioni kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe, nje kidogo ya jiji la Kampala, wanasheria wake walisema.

Waziri amlima barua mwenzake

Katika hatua nyingine, Waziri wa Sheria na Katiba Jenerali Kahinda Otafire Alhamisi alimwandikia barua mwenzake wa Mambo ya Ndani Jeje Odongo, akilalamikia mwenendo wa maofisa usalama kwamba tabia yao ni uvunjaji mkubwa wa sheria na vitendo vyao vinakiuka haki za kibinadamu.

Katika barua hiyo Jenerali Otafiire alisema: “Ukamataji usiofuata sheria, na vitisho lazima vikome”.

“Inaonekana kama kuna mpangilio fulani wa matumizi ya nguvu na ukandamizaji wa haki za kibinadamu kwa kutumia vibaya madaraka na dhuluma dhidi ya raia,” aliandika Jenerali Otafiire.

Otafiire, alitaja matumizi mabaya ya ofisi, madaraka, kuwatisha watu, kuwapiga wabunge, kuwateka nyara watu, kuunda ushahidi wa uongo, uchunguzi usio na msingi, kuwalaghai raia, miongoni mwa mengine ni tabia inayovunja moyo na isiyoweza kuendelea kuvumiliwa.

Katika barua hiyo Waziri Otafiire amemtaka waziri mwenzake kuchukua hatua za haraka kuleta nidhamu katika taasisi hiyo ya usalama.

“Kuna ongezeko la malalamiko dhidi ya maofisa wa usalama wakishirikiana na maofisa wengine serikalini, kuhusiana na ukamataji, kutishia raia, ulaghai na kutengeneza ushahidi wa uongo dhidi ya washukiwa,” inasomeka sehemu ya barua.

Lakini Waziri wa Usalama Elly Tumwine, amesema kuwa vyombo vya usalama haviwezi kuvumilia watu wanaotaka kuvuruga usalama wa nchi.

Tumwine ameonya: “Mkitaka kujaribu kuipindua serikali, sisi tupo tayari. Tumechunguza jumbe zote kwenye mitandao ya kijamii, chanzo chake ni nchi za nje kama Wakenya wanaofanya maandamano.

“Wakenya wana matatizo ya kutosha wanayostahili kuandamana huko sio kuingilia mambo yetu. Tuna ushahidi kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yanatumika kutuvuruga kwa kulipa vyombo vya habari, vijana na wanasiasa.”

Waziri wa Usalama anadai kwamba maadui wa Uganda wanawatumia vijana kuvuruga usalama wa taifa na kwamba serikali ya Museveni iko tayari kwa wale wanaotaka kupindua utawala uliopo.

Barua ya Spika kwa Rais

Barua ya Otafiire kwa Waziri Odong, iliandikwa siku tatu baada ya Spika wa Bunge Rebecca Kadaaga kumwandikia barua Rais Yoweri Museveni akitaka maofisa wote waliohusika katika kukamata na kuwatesa wabunge wawili Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine na Francis Zaake wakiwa kizuizini wakamatwe.

Jaji afafanua katiba

Ijumaa, Jaji Mkuu wa Uganda Bart Katureebe alitoa waraka kuviambia vyombo vya usalama kwamba katiba ya nchi inakataza watu kuteswa.

“Maofisa usalama, wakati mnawakamata raia wa Uganda, wakamateni kama binadamu na siyo kama wanyama,” alisema

Umoja wa Mataifa

Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za kibinadamu nayo inataka serikali ya Uganda kuruhusu uchunguzi huru usioegemea upande wowote kutokana na ukandamizaji wa haki za kibinadamu kufuatia vurugu za terehe 13 mwezi Agosti mjini Arua.

Pia inataka serikali kuwafunguliwa mashtaka wahusika wote, Kamishna mkuu wa haki za kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad al Hussein akisema kwamba umoja wa mataifa umesikitishwa sana na matukio nchini Uganda.