Katiba Mpya inawezaje kupatikana, kutumika kabla ya uchaguzi 2020?

Ikiwa imebaki takribani miaka miwili ili Tanzania iingie kwenye Uchaguzi Mkuu 2020 vuguvugu la kudai kuhuishwa kwa mchakato wa kuandika Katiba mpya limeshika kasi, huku swali ambalo mpaka sasa halijajibiwa ni kuwa je, kwa mazingira yaliyopo sasa, sheria hiyo mama inaweza ikapatikana kabla ya uchaguzi huo?

Serikali kwa upande wake ilishajitenga na mjadala huu ikisema kwamba haina mpango wa kuufufua mchakato wa Katiba Mpya kwa siku za hivi karibuni kwa kile ilichoeleza kuwa si kipaumbele chake, bali mwelekeo wa Serikali ya awamu ya tano ni utoaji wa huduma za kijamii na kujenga uchumi wa viwanda.

Msimamo huo wa Serikali hata hivyo unatofautiana na maoni ya wananchi wanaodhani kuna haja ya kuwa na Katiba Mpya sasa kabla ya kuingia kwenye uchaguzi mkuu.

Ripoti ya hivi karibuni ya shirika lisilo la kiserikali Twaweza inabainisha kuwa Watanzania wawili kati ya watatu wanahitaji Katiba Mpya sasa.

Tungeepuka mengi

Kutoka katika mitandao ya kijamii mpaka kwenye warsha na semina mbalimbali, sauti zimekuwa zikiongezeka zikisisitiza kufufuliwa kwa mchakato wa Katiba Mpya huku wengine wakitanabahisha kuwa bila ya kuwa na katiba hiyo Uchaguzi Mkuu ujao upo hatarini kutopita salama, unaweza kuambatana na fujo na matukio ya uvunjifu wa amani.

Wafuatiliaji wa mambo ya kisiasa wanatolea mfano fujo na kasoro kadhaa zilizotokana na chaguzi ndogo za marudio zilizofanyika katika majimbo ya Kinondoni na Siha, na katika kata 43 zilizotangulia kama dalili za kile kinachoweza kutokea katika Uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Kama Katiba Mpya ingekuwa ni kipaumbele chetu, tungeliepukana na mengi,” anasema Carol Ndosi, mjasiriamali na mwanaharakati wa haki za wanawake, katika barua yake ya wazi kwa Rais John Magufuli ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii.

Lakini, je, ni kweli Katiba Mpya inaweza kupatikana kabla ya uchaguzi ujao? Matarajio ya baadhi ya watu kwa sasa hayatoi picha hiyo.

Picha hii, kulingana na maoni ya wadau kadhaa wa masuala ya sheria na katiba nchini, inatokana kwa kiasi fulani na ukweli kwamba suala la Katiba Mpya si ajenda ya Serikali.

“Uzoefu unaonesha kwamba ili kitu kiweze kufanyika katika nchi hii ni lazima kiwe ni ajenda ya Serikali na Rais kwenye suala husika,” anasema Jenerali Ulimwengu, wakili na mwandishi mkongwe nchini.”

Hoja ya Ulimwengu inaonekana kupata nguvu ukizingatia ukweli kwamba ilikuwa ni Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliyeanzisha mchakato wa Katiba Mpya mnamo mwaka 2012.

Ni Kikwete aliyeunda Tume Maalumu ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba ambayo ilikuja na rasimu ya Katiba baada ya mchakato mrefu wa kukusanya maoni nchi nzima.

Rasimu ya katiba iliyotokana na Tume ya Warioba ‘ilipozwa’ na Bunge Maalum la Katiba kitu kilichopelekea wajumbe kutoka kambi ya upinzani na wengine kulazimika kutoka nje ya Bunge na kususia mchakato mzima wa Katiba mpya.

INAENDELEA UK 20

INATOKA UK 15

Wajumbe hawa wa upinzani waliokuwa chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wenzao ni sehemu ya Watanzania ambao wameendelea kuibua sauti za kudai katiba Mpya.

Hata hivyo, licha ya kususiwa na baadhi ya watu, Bunge Maalum la Katiba chini ya uwenyekiti wa spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri Samuel Sitta (marehemu), kwa sehemu kubwa likitawaliwa na wanasiasa wakiwamo wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, liliuendeleza mchakato na kutoka na Katiba Inayopendekezwa.

Kura ya maoni, ambayo ilipaswa kuwapa wananchi fursa ya kuikubali au kuikataa Katiba Inayopendekezwa haikuweza kufanyika mpaka sasa.

Lakini, sifa zote kwa mchakato huu uliokwama wa Katiba, za wema au ubaya, zilikwenda kwa Rais mstaafu Kikwete ambaye aliwashangaza hata wakubwa ndani ya chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM), alipouanzisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

Kwa kuwa Serikali ya sasa imeshaweka wazi msimamo wake kuwa Katiba Mpya si kipaumbele chake, Ulimwengu anasema haoni dalili yoyote ya kuipata kabla ya 2020.

Hii ni kwa sababu tu Serikali iliyopo madarakani haiitaki Katiba Mpya.

“Tuna Rais anayedhani kuwa anaweza ‘kuinyoosha’ nchi bila ya Katiba Mpya,” anasema Ulimwengu.

Kurejea kwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya, Ulimwengu anasema kunahitaji Serikali ilazimishwe iuchukue mchakato kama ajenda yake.

Katiba kudhibiti fujo

Kuwa na Katiba Mpya kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao kunaweza kukaepusha mengi na kuisaidia nchi kwa kiasi kikubwa, anatanabahisha Profesa Mwesiga Baregu ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akionyesha umuhimu wa kuwa na Katiba Mpya sasa, Profesa Baregu anasema kwamba uzoefu unaonyesha kwamba chaguzi nyingi huambatana na fujo na vitendo vingine vya uvunjifu wa amani kama chaguzi hizo zitakuwa zimejawa na kasoro nyingi.

Miongoni mwa sababu kadhaa zinazohusishwa na machafuko ya nchini Kenya baada ya uchaguzi mwaka 2007/2008 ni pamoja na nchi hiyo kuingia kwenye uchaguzi mkuu unaogombaniwa sana huku kukiwa na katiba dhaifu.

Hatimaye Kenya iliandika katiba yake mpya mwaka 2010 na chaguzi zote zilizofuata za 2013, 2017 na ule wa marudio wa 2018 hazikuwa zenye uvunjifu mkubwa wa amani kama ule wa 2007 ulivyokuwa.

“Tuna uwezo wa kuepukana na kile kilichowatokea Wakenya 2007. Hakuna haja ya kurudia uzoefu wao (kusubiri machafuko ndio tuone umuhimu wa kuandika Katiba Mpya), anasema Profesa Baregu.

Ni kutokana na umuhimu huu basi, suala la upatikanaji wa Katiba Mpya sasa linapata mashiko zaidi. Akizungumzia uwezekano huo wa kupata Katiba hiyo sasa kabla ya uchaguzi mkuu unaokuja, Profesa Baregu anasema inawezekana, kinachohitajika ni utayari wa kisiasa tu.

Baregu anaeleza kukerwa na kauli za Serikali kwamba suala la Katiba Mpya si kipaumbele chake. Anasema kwamba kwa jinsi ilivyo, suala lenyewe ni kipaumbele cha wananchi hivyo Serikali haina budi kuufufua mchakato wa kuandika Katiba Mpya.

Katika nchi yoyote ya kidemokrasia anasema, “nguvu na mamlaka vyote viko kwa watu.

Huu ni ukweli kwa nchi yoyote inayojiita ya kidemokrasia, ikiwemo Tanzania, vinginevyo Serikali iweke wazi kwamba misingi ya kidemokrasia iliyoasisi taifa hili haifai tena.”

Baregu anaeleza kuhuzunishwa na watu wanaotumia hoja nyepesi wanapojadili masuala mazito ya kitaifa, kama Katiba.

“Tunahitaji kutafuta namna ya kujenga maelewano miongoni mwa vyama vyote vya kisiasa na kuwa na suluhu moja ya namna gani tunajikwamua hapa tulipo kama taifa,” anapendekeza.

Faida kubwa

Hata hivyo, kwa mujibu wa mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Hamad Salim kupata Katiba Mpya kwa sasa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2020 ni kitu kisichowezekana.

Hata ikiweza kupatikana, Salim anasema, basi hadhani kama inaweza kutumika katika uchaguzi huo.

“Uwezekano wa kuwa na Katiba Mpya kabla ya 2020 ni mdogo sana kwa sababu walioko serikalini hawaoni umuhimu wa mchakato mzima kwa sasa,” anasema Salim.

Suala la upatikanaji wa Katiba linatatizwa zaidi na ukweli kwamba mchakato wote uliwekwa chini ya mtu mmoja, Rais mstaafu Kikwete, na wala haukuingizwa kwenye mipango ya muda mrefu ya Serikali.

Alipokuja Rais mwingine, Salim anasema, hakuona umuhimu wa kuuendeleza mchakato na kuukamilisha.

Lakini, mhadhiri huyo anabainisha kwamba serikali na chama tawala, CCM, inakosea na inatenda makosa makubwa kwa kutoupa umuhimu wa kutosha mchakato wa Katiba.

Kama kungekuwa na utayari wa kisiasa, ambao kwa mujibu wa Salim haupo, nchi ipo katika nafasi nzuri ya kuukamilisha mchakato wa Katiba mpya ikizingatia kwamba kuna hali ya utulivu nchini.

“Hii ni faida kubwa kwetu,” anasema Salim huku akipendekeza kuwa hakuna haja ya kusubiri mpaka mambo yaanze kwenda mrama ndio viongozi waone umuhimu wa kuleta Katiba Mpya.

Nini kifanyike?

Ulimwengu anasema endapo Rais Magufuli ataona umuhimu wa kufufua mchakato wa uandishi wa Katiba mpya, basi anaweza akachukua rasimu ya mwisho ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na Katiba Inayopendekezwa na kuona ni jinsi gani, kwa kupitia wataalamu wa masuala ya Katiba, jinsi nyaraka hizo mbili zinaweza kuchanganywa pamoja.

Hatuna sababu ya kusubiri mpaka tukabiliane na hali ya hatari, ndio tufufue mchakato wa Katiba Mpya,” anasema.

Anaonya kuwa ni hatari sana kwa taifa kuona wananchi wanadai kitu ambacho ni haki yao, na wale walio na mamlaka ya kuwapatia wanawapuuza.

Anashauri kuwa ni vyema Serikali ikaacha ukaidi na kuwapatia wananchi Katiba Mpya ili nchi iweze kuepukana na vitendo vya uvunjifu wa amani ambavyo vinaweza kusababishwa na kutokujali kwa Serikali.

Katika ushauri wa Profesa Baregu, ambao unaungwa mkono na Salim, ni kwamba kama Serikali itadhamiria kuwapatia wananchi Katiba mpya, inaweza ikaunda timu ya wataalamu, popote wanapoweza kupatikana, hata kama itakuwa ni nje ya Tanzania, ambayo inaweza kuendesha majadiliano na wadau tofautitofauti wa Katiba na kuona na jinsi gani wananchi wanaweza kupatiwa katiba yao.

+255 716 874 501