KUELEKEA MAJIMBONI : Mkoa wa Tabora hali si nzuri kwa Ukawa majimbo ya Uyui, Tabora na Igalula

Muktasari:

Wilaya ya Uyui inaundwa na majimbo mawili ya uchaguzi, jimbo la Uyui (Tabora Kaskazini) na jimbo la Igalula.

WILAYA YA UYUI

Wilaya ya Uyui ni moja kati ya wilaya saba za mkoa wa Tabora na inaundwa na kata 29, vijiji 156 na vitongoji 688. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wilaya hii ina jumla ya wakazi 396,623 kwa maana ya wanaume 196,446, wanawake 200,177 na kuna wastani wa watu 6.6 katika kila kaya.

Wilaya ya Uyui inaundwa na majimbo mawili ya uchaguzi, jimbo la Uyui (Tabora Kaskazini) na jimbo la Igalula.

TABORA KASKAZINI

Jimbo hili lilishiriki uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi na kushuhudia demokrasia pana kwa maana ya kuwepo kwa “vyama utitiri” huku upinzani ukikubalika kwa wananchi kuliko CCM. Hata hivyo mipango ya vyama vya upinzani ilionesha kila dalili ya kujikwamisha wao kwa wao na ndiyo maana haikushangaza CCM ilipoponea chupuchupu kwa sababu upinzani ulinyang’anyana “kasungura” kadogo na kila mmoja akatoka na kipande.

Emmanuel Paul Seleli wa NCCR ndiye alikuwa mshindi wa pili, alipata kura 4,304 sawa na asilimia 17.0, Samwel Msonda Simwanza wa CUF na Yasini Kasola wa NLD walipata asilimia 5.8 na 4.6 ya kura zote na Leila Shamshu Damji wa TADEA akiwa na asilimia 4.5. Mgombea wa CCM, Kesi Deusdedit Michael ndiye aliibuka mshindi wa jumla kwa kupata kura 13,850 sawa na asilimia 54.7 na kuapishwa kuwa mbunge. Kama vyama vya upinzani vingelijipanga kimkakati, jimbo hili lingechukuliwa na NCCR mwaka 1995.

Mwaka 2000 CCM ilimsimamisha Dk. James Msekela na kwa sababu ya kufifia kwa NCCR kada huyu hakupata shida sana kuchukua ushindi wa kutosha na kuliongoza jimbo hili hadi mwaka 2005.

Dk. James Msekela ndiye alichukua fursa ya kuwaongoza wana CCM kwa mara nyingine tena kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 ambapo nguvu ya CUF jimboni hapa ilikuwa ni moto wa kuotea mbali. Mgombea wa CUF, Emmanuel Albino Lugusha alipigiwa kura 10,837 sawa na asilimia 24.8 akifuatiwa kwa mbali sana na yule wa CHADEMA aliyekuwa na asilimia 2.3 ya kura zote. Mshindi akawa ni Dk. Msekela kwa kupata kura 30,309 sawa na asilimia 69.3. Wagombea wa vyama vingine kwa ujumla wao walikuwa na asilimia 3.9 ya kura zote.

Uchaguzi wa mwaka 2010 hapa Tabora Kaskazini ulikuwa mwepesi sana kwa CCM. Nguvu ya CUF ilishuka sana na naambiwa hapakuwa na mgombea mzuri. CCM mara hii ikimleta kada wake Sumar Shaffin Mamlo, iliibuka na kura 18,872 sawa na asilimia 81.54 ya kura zote. Kwa mbali sana alifuatia Kassoga David Sizya wa CUF akiweka kibindoni kura 2,521 sawa na asilimia 10.89. Wagombea kutoka Chadema, SAU na TADEA walikuwa na asilimia tano ya kura zote.

Nimejulishwa kutoka hapa Tabora Kaskazini kuwa huwenda Sumar anakabiliwa na upinzani mkubwa ndani ya chama chake lakini tathmini na utafiti wa kawaida unaonesha kuwa bado CCM imeweka mizizi mirefu katika jimbo hili kiasi kwamba si rahisi upinzani utalichukua kirahisi mwaka huu labda pawepo na mipango na juhudi za ziada.

Takwimu za matokeo ya serikali za mitaa kwa jimbo hili si nzuri kwa upinzani, CCM imeshinda vijiji na vitongoji kwa takribani asilimia 90 jambo lenye maana kwamba chama hicho kimezidi kumea hapa. Hakika, naona kila dalili ya jimbo hili kuendelea kumilikiwa na CCM baada baada ya uchaguzi wa mwaka huu.

JIMBO LA IGALULA

Kama ilivyokuwa kwa jimbo pacha la Tabora Kaskazini, hapa Igalula pia hapakuwa na mapambano dhahiri ya CCM na NCCR (kama ilivyotarajiwa) kwa sababu chama hicho cha upinzani kilinyang’anywa kura na vyama vingine na hivyo CCM ikaachiwa ushindi wa jumla wa kura 7,339 sawa na asilimia 55.3, mgombea wa chama hicho akiwa ni mwanamama machachari Tatu Ntimizi.

Aliyemfuatia Ntimizi kwa mbali ni mgombea wa NCCR, Shaaban Mnyonga aliyekuwa na kura 2,213 sawa na asilimia 16.7. Mgombea wa Chadema, Clement Mswanyama alipata kura 994 sawa na asilimia 7.5 ya kura zote. Wagombea wengine waliokuwa na nguvu za kukaribiana ni Masoud Mustapha Negenuka wa CUF na Faraji Hussein Katalambula wa TADEA ambao walipata asilimia 5.4 na 4.7. UMD ilipata asilimia 3.0, UDP asilimia 2.0, NRA asilimia 1.9, PONA asilimia 1.8 na NLD asilimia 1.6. Upinzani uliishia kujitafuna wenyewe na CCM ikapeta kwa kura zaidi kidogo ya nusu..

Mwanamama Tatu Ntimizi ndiye alishinda kwa mara ya pili uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2000 hapa Igalula na aliongoza jimbo hili hadi mwaka 2005 akiwa miongoni mwa wanamama wachache waliosimama majukwaani na kuwashinda wanaume kwenye chaguzi za mwanzo za kidemokrasia hapa Tanzania.

Kwa mara ya tatu, mwaka 2005, Tatu Musa Ntimizi alishinda uchaguzi wa ubunge wa Igalula. Pamoja na ushindi wake kupungua kulinganisha na ule wa mwaka 2000 walau alipata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote. Tatu alipigiwa kura 15,106 sawa na asilimia 60.0 na alifuatiwa na Shaaban Ally Mohamed wa CUF aliyekuwa na kura 8,270 sawa na asilimia 32.8 ya kura zote. Wagombea kutoka Chadema na Chausta kwa pamoja walipata asilimia 5.2 ya kura zilizopigwa na wale wa TLP, SAU na DP kwa pamoja walipata asilimia 2.0 ya kura zote.

Baada ya uongozi wa miaka 15, Tatu Ntimizi alikaa pembeni kuwaachia nafasi wana CCM wengine waweze kuonesha ubavu wao. Mwaka 2010 akaja Athuman Rajab Mfutakamba, kada huyu wa CCM alikutana na upinzani unaokua haraka lakini akafanikiwa kuzima ndoto za vyama hivyo kwani alipata asilimia 7 zaidi kulinganisha na matokeo ambayo CCM ilipata na kupitisha mbunge mwaka 2005.

Takwimu halisi zinaonesha kuwa Mfutakamba alishinda kwa kura 8,971 sawa na asilimia 67.25 na aliyemfuatia ni Erick Kabepele James wa Chadema aliyekuwa na kura 1,972 sawa na asilimia 14.78 na wa tatu alikuwa ni Hassan Juma Mwigwayasila wa CUF akiwa na kura 1,729 sawa na asilimia 12.96 ya kura zilizopigwa. Vyama vya DP na SAU kwa pamoja vilipata asilimia 1.4 ya kura zote.

Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi Desemba 2014 yanaonesha kuwa CCM imeshinda sana hapa Igalula. Japokuwa vyama vya upinzani vimeongeza ushindi wake ukilinganisha na mwaka 2009 lakini kitakwimu bado CCM ina nguvu tangu ngazi ya chini.

Pamoja na kuwa Mfutakamba anasongwa na hofu za kupita kura ya maoni ndani ya CCM, nimeambiwa kuwa apitishwe yeye au la ni kama vile mapambano makubwa zaidi hapa mwezi Oktoba yatakuwa yameshamalizwa ndani ya CCM mwezi Agosti. Mtandao wa vyama vya upinzani hapa Igalula unakua lakini haujajengwa kama vile ambavyo CCM wameweza. Sina shaka kabisa pale ntakaposema kuwa jimbo hili pia siyo zuri hata kidogo kwa upinzani baadaye mwaka huu.

JIMBO LA TABORA

Jimbo la Tabora Mjini ni sehemu yote ya Manispaa ya Tabora Mjini na manispaa hii inaundwa na kata 29, mitaa 135, vijiji 32 na vitongoji 145. Kwa mujibu wa sense ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tabora ina wakazi 226,999 ambapo wanaume ni 111,361, wanawake ni 115,638 na kuna wastani wa watu 4.7 katika kila kaya.

Jumla ya vyama 12 ndivyo vilisajili wagombea kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 1995 hapa Tabora Mjini, kitovu cha mkoa wa Tabora. Tatizo lile lile la vyama vya upinzani kuvutana na kuweka wagombea wengi ndilo lilisababosha jimbo hili lisiende mikononi mwa vyama hivyo. Kwenye uchaguzi naoungelea hapa CCM ilionekana kuwa na nguvu sana kama ingeshindana na chama kimoja kimoja na ingekuwa nyepesi sana kuangushwa ikiwa ingepigana na vyama vyote vikiwa na mgombea mmoja.

Nguvu ya wastani ilihodhiwa na NCCR na TADEA. NCCR ikimsimamisha Gilliard Joseph Mlaseko ilipata kura 8,461 sawa na asilimia 21.3 ya kura zote. Kassim Ahmed Aziz wa TADEA alikuwa na kura 5,080 sawa na asilimia 12.8 na mshindi wa jumla alikuwa ni Corona Faida Bussongo wa CCM akijipatia kura 21,318 sawa na asilimia 53.6 ya kura zilizopigwa.

Vyama vya TLP, Chadema, UMD, UPDP, PONA, NLD, TPP, NRA ma UDP kwa pamoja vilipata asilimia 12.2 ya kura zote na kuhitimisha safari ya upinzani kulikosa jimbo hili ambalo lilikuwa tayari lwa mabadiliko.

Kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 NCCR ilikuwa hoi bin taabani ikishughulikia migogoro na CUF ilianza kuja juu hapa Tabora japokuwa katika uchaguzi ule bado CCM ilishinda ikimtumia Henry Robert Mgombelo ambaye alipigiwa kura nyingi sana na kuondoka na ushindi mkubwa kuliko ule wa mwaka 1995.

Mapambano ya CUF na CCM hapa Tabora Mjini yalidhihirika tena mwaka 2005 kwenye uchaguzi mkuu mwingine. CCM ilibadilisha mgombea kwa mara nyingine baada ya kumuweka nje Mgombelo, mara hii ikimtumia mwanasiasa maarufu sana, Juma Siraju Kaboyonga. CUF nayo kwa kujipanga ilimuwekaShabani Juma Nyemela ambaye aliishia kupata kura 15,408 sawa na asilimia 27.8. Kaboyonga wa CCM alipigiwa kura 38.075 sawa na asilimia 68.7 na kupata nafasi ya kuwawakilisha wana Tabora Mjini. Wagombea kutoka Chadema, DP, Jahazi, Makini, NCCR, SAU, TLP na UDP kwa pamoja walikuwa na asilimia 3.5 ya kura zote.

Uongozi wa Kaboyonga ulikoma mwaka 2010 na alitaka kuendelea lakini kura ya maoni ndani ya CCM ikamuengua. Wana CCM wakampa fursa mdau wa michezo wa siku nyingi, Ismail Aden Rage. Rage alicheza karata zake vizuri ili kuzuia nguvu ya upinzani ambayo imekuwa inaenda mbele kwa kasi sana hapa Tabora Mjini. Alifanikiwa kuongoza kwa ujumla wa kura 27,329 sawa na asilimia 67.83 akafuatiwa na mgombea wa CUF, Kapasha Haji Kapasha aliyekuwa na kura 7,792 sawa na asilimia 19.34 huku mgombea wa Chadema, Mussa Hussein Kwikima akipata kura 3,682 sawa na asilimia 9.14. Vyama vya DP, Makini, UDP, NLD, SAU na UMD kwa pamoja vilipata asilimia 1 ya kura zote.

Matokeo hayo yalikuwa na maana kuwa Ismail Aden Rage ndiye mbunge wa Tabora Mjini na imekuwa namna hiyo hadi niandikapo kuhusu jimbo hili. Pamoja na kwamba vyama vya upinzani havikufanya vyema katika uchaguzi wa serikali za mitaa kulinganisha na CCM kwenye uchaguzi wa Disemba 2014, ukweli ni kwamba upinzani hapa Tabora Mjini unaungwa mkono sana ikiwa atapatikana mgombea mmoja mzuri na ambaye anauwezo wa kuwashawishi wananchi kuaminii kuwa anaweza kusimamia mabadiliko wanayoyataka. Nadhani uwepo wa Ukawa mwaka huu unaweza kukata kiu ya mabadiliko ambayo wana Tabora Mjini wamekuwa nayo kipindi kirefu.

Mimi binafsi naamini kuwa Ukawa ikipata mgombea mzuri sana hapa na anayekubalika, jimbo hili litakuwa ni hamsini kwa hamsini kati ya CCM na Ukawa, lakini akisimamishwa mgombea “bora liende”, CCM itapata inachotaka. Ismail Rage kwa upande wake anakabiliwa na mtihani wa kuvunja mwiko wa kuongoza jimbo hili kwa miaka 10 kwani tangu mwaka 1995 kila mbunge wa CCM aliyepita hapa alikaa miaka mitano peke yake bila kuongezewa kipindi cha pili.

HITIMISHO

Jumatano ya wiki ijayo (Tarehe 01 Julai 2015) tutadadavua majimbo ya Igunga, Bukene na Nzega na Jumamosi (tarehe 04 Julai 2015) tutakamilisha mkoa wa Tabora kwa kuchambua majimbo ya Sikonge, Urambo Mashariki na Urambo Magharibi.

(Uchambuzi huu unafanywa na Julius Mtatiro “Adv Cert in Ling, B.A, M.A, L LB (Student)”: +255787536759, [email protected], https://www.facebook.com/julius.mtatiro, - ni maoni binafsi ya mwandishi).