Maalim Seif aeleza zuio la mikutano linavyowapa wapinzani changamoto

Muktasari:

  • Baada ya zuio la wapinzani Tanzania kufanya Mikutanao ya Hadhara nje ya maeneo yao Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza changamoto zinazotokana na zuio hilo

Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza kuwapo changamoto inayotokana na zuio la mikutano ya kisiasa nchini, hasa katika kipindi cha utawala wa awamu ya tano.

Hamad aliyasem Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad a hayo katika kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) juzi usiku akiwa London, Uingereza.

Alisema kikawaida vyama vya siasa huhitaji kukua na kumea kila siku kupitia mfumo wa kuongeza wanachama wapya, jambo ambalo hivi sasa halifanyiki kutokana na marufuku iliyopigwa na Rais.

Alisema mikutano ya vyama vya siasa ndio njia pekee ya wao kuhubiri sera za vyama vyao hatimaye wananchi kuona nini chama kinafanya lakini pia kuikosoa Serikali pale wanapokesea.

Mwanasiasa huyo alisema vyama vya siasa vina nafasi ya uongozi kwenye maeneo mbalimbali ambayo wamepewa jukumu na wananchi, hivyo wanalazimika kupata mrejesho wa ahadi ambazo wametoa kwa wananchi sambamba na maendeleo ya maeneo yao.

“Hatua hii ni sawa na kuwanyima viongozi wa upinzani kuwaeleza wananchi yale waliyofikia na kukosoa pale inapobidi, lakini yote hayo hayafanyiki. Unalazimika kufuata mlolongo mkubwa kabla ya kuruhusiwa kufanya mkutano mdogo wa jimbo tu,” aliongezea Hamad.

Alidai mfumo huu unaoendelea sasa, wa kuzuiwa kwa mikutano ya siasa, haujawahi kutokea tangu kuasisiwa kwa vyama vya siasa.

Katika hatua nyingine, Hamad alidai vyama vya upinzani vimekuwa vikikandamizwa katika njia tofauti kwa lengo la kuhakikisha haviendelei kukua badala yake vimeendelea kudumaa na kurudi chini kiutendaji.

Alitolea mfano mgogoro wa miaka miwili sasa kwenye chama chake na kusema mgogoro huo umetengezwa makusudi na msajili wa vyama vya siasa Jaji Francis Mutungi kumrejesha Profesa Ibrahim Lipumba kwenye nafasi aliojiuzulu ya uenyekiti wa chama chao, madai ambayo Jaji Mutungi amekuwa akiyakanusha mara akwa mara.

Kesi zadhoofisha chama

Alisema mgogoro huo umesababisha kufunguliwa kwa kesi mbalaimbali umerudisha nyuma kwa kiasi kikubwa nguvu za upinzani kwenye chama chake lakini pia umoja wa vyama vya siasa ulioasisi katika Bunge la Katiba (Ukawa).

Alisema mchakato wa kujiuzulu kwa Lipumba ulitengezwa kwa dhana kuwa waliotengeza mkakati ule waliamini kwamba kutoka kwake kungeleta madhara makubwa ikiwemo kutoka na wafuasi wengine wa vyama vya upinzani.

Alisema CUF kama chama chenye wabunge na madiwani, kilitarajia kupatiwa ruzuku ili waendeleze harakati za ujenzi wa chama lakini ruzuku hiyo ilizuiliwa kwa madai ya kuwepo kwa mgogoro kwenye chama chao.

Hivi karibuni Jaji Mutungi alilieleza gazeti hili kuwa anatendelea kutoa ruzuku kwa upande wa Lipumba “Kwa sababu chama kilimwandikia kuelekeza hivyo.”

Hamadi anasema kilichoweza kunusuru ruzuku hiyo ya chama ni baada ya wao kwenda kufungua shauri na mahakama kuamuru kuzuia ruzuku hiyo, lakini vinginevyo ingeendelea kutoka hadi sasa.

Hamad pia alisema licha ya uwepo wa changamoto hizo, wanachofikiria kwa sasa ni kuunganisha nguvu zaidi ya vyama vya siasa ambavyo anaamini vitakua na tija kubwa kwa Watanzania katika kuelekea uchaguzi wa 2020.

Kuhusu muswada wa marekebisho ya vyama vya siasa mwaka 2018, alisema msajili ndiyo atakayeweza kuamua kiongozi gani anapaswa kuendesha chama na kiongozi gani hafai kwa mujibu wa muswada ambao umewasilishwa bungeni.

Pia, Hamad alisema muswada huo umeweka mazingira magumu kwa vyama vya siasa iwapo vinataka kuungana lazima vipate idhini ya waziri husika, jambo ambalo alidai si rahisi kukubalika.

“Tunajua kwamba waziri anatoka katika chama tawala, CCM, na inajulikana wazi kuwa umoja ni nguvu na watakapoungana ni wazi itakuwa changamoto, sidhani kama watakubali,” alifafanua zaidi Hamad.

Katika kufafanua zaidi alisema iwapo muswada huo utapita ni kwamba mtu aliyeacha chama chake na kwenda chama kingine hataruhusika kugombea nafasi yoyote ya uongozi kwenye chama kipya mpaka atakapotimiza mwaka mmoja.

Hamad aliweka wazi na kusema kwamba mazingira hayo yote yanatokana na baadhi ya watawala kuwa na hofu ya uchaguzi wa mwaka 2020, wakidhani baadhi ya viongozi miongoni mwao wanaweza kugombea nafasi kupitia vyama vya upinzani.

Akizungumzia kuhusu hatma yake na mbio za urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 alisema muda wakusema hayo bado na utakapofika ataweka wazi kila kitu.