Vyama vya siasa vianze kujisahihisha, kukosoana

Muktasari:

Wiki hii naelezea baadhi ya mambo yanayoweza kuisaidia nchi kupiga hatua kubwa ya kisiasa.

Na Andrew Bomani

Wiki hii naelezea baadhi ya mambo yanayoweza kuisaidia nchi kupiga hatua kubwa ya kisiasa.

Ni imani yangu hatuna budi kupata somo muhimu kutoka Bunge la Kenya. Bunge hili lina utaratibu tangu mwaka 2013 wa kujadili majina ya wateule wa rais kama mawaziri. Kwa Kiingereza inajulikana kama vetting.

Utaratibu huu ni tofauti na Tanzania ambako Rais akishamteua mtu ndio basi, hakuna kujadili chochote kwa upande wa wananchi. Historia yetu imeonyesha jinsi watu wenye kila aina ya doa wakipewa madaraka huku raia wakibaki kuwa watazamaji tu. Ukihoji unaambiwa una wivu!

Tubadilike sasa na kamati maalumu ya Bunge ikabidhiwe rungu, ila baada kwanza ya kuondoa sifa kuu ya kuwa mbunge kuwa ni kujua kusoma na kuandika kwa lugha ama ya Kiingereza au Kiswahili. Imepitwa na wakati!

Kinachofanyika Kenya, mteule anapita kwenye tanuri la moto. Unaanza kula kiapo na unaahidi kusema ukweli wakati wote. Baada ya hapo ni kuthibitisha kwamba huna doa kwa upande wa kodi, rushwa, uhalifu kwa ujumla na elimu. Pia unaanika unamiliki kiasi gani. Yote haya ni mubashara.

Pia unatakiwa kueleza historia yako kwa dakika kumi. Hizo ni dakiki nyingi kwa mtu ambaye ni mbabaishaji. Kamati ya uteuzi inapewa takriban saa mbili kumhoji mteule na kwenye kamati hiyo ni vigumu kujua wengi ni wa chama gani, tawala au upinzani kutokana na aina ya maswali.

Katika hali ya kawaida, hakuna mbunge atataka aonekane mbumbumbu kwenye kamati hiyo. Kwa upande wa mteule, kama una historia ya kutoa kauli zisizofaa kaa chonjo. Pia ni nafasi nzuri ya kujijenga kisiasa kama una mipango mizuri. Mwisho wa yote, kama kuna wananchi wenye vielelezo dhidi ya mhusika, wanakaribishwa kuviwasilisha kwenye kamati.

Katika kuimarisha uwajibikaji nchini, wabunge pia watafutiwe utaratibu kama ule uliopendekezwa na Tume ya Jaji Nyalali kuwa kama zaidi ya nusu ya wapigakura walioandikishwa kwenye jimbo wamewasilisha kwenye Tume ya Uchaguzi taarifa kwa maandishi kutokuwa na imani na mbunge, basi itabidi uchaguzi mdogo uitishwe.

Sasa katika kumalizia hili jambo la kushindwa kufanya shughuli za kisiasa kama watu wazima, nitatoa mfano wa mgombea huru. Hili suala limekuwa la maumivu kwa Taifa tangu 1992. Mzee Mwinyi katika kitabu chake cha mwaka jana aliandika yafuatayo: “Kwa ujumla Mwalimu Nyerere alifurahishwa na mchakato na mapendekezo. Tulishindana naye kwenye jambo moja tu- la wagombea binafsi. Yeye alitaka wawepo, lakini wengi kwenye chama na Serikali walihofu, kwa haki kabisa, kuwa hiyo itakuja kudhoofisha CCM, pale wasiopita kwenye mchujo wakiamua kusimama kama wagombea binafsi.

Aidha tulijitahidi kufanya iwe vigumu kwa vyama kuungana, tukasema wakitaka kuungana lazima wajifute kwanza na kisha kuanza na kujisajili upya. Lengo la hatua hizi mbili halikuwa kuipendelea CCM, bali kuimarisha msingi wa mfumo wa vyama vingi.

Kama ingekuwa kuimarisha vyama, mgombea binafsi ni njia ya uhakika kwa vile wale miungu watu watajua wagombea hawatavumulia uonevu.

Mifano ya uonevu ni mingi. Na kama kweli lengo ni kuwa na vyama madhubuti badala ya ushirikiano, njia hapo ni itikadi tu na si kufanya iwe vigumu kwa vyama kuungana.

Sasa madhara ya kuzuiwa mgombea huru ni kama hivi kuna chaguzi ndogo za ubunge na udiwani. Wenye vyama vya upinzani wakiamua kususia, wananchi wanabaki bila chaguo. Je, hiyo si ukiukwaji wa haki za msingi za mpiga kura na wagombea pia?

Mwinyi hapo alipaswa kujisahihisha na si kuendeleza mawazo ya mwaka 1992.

Kwa makusudi nimejaribu kuonyesha yanayotusibu kama Taifa. Kikosi kazi kimeshindwa kuweka wazi umuhimu wa mgombea huru wakati ni jambo ambalo limeshahangaikiwa hadi mahakama ya mwisho. Ni doa kubwa kwa Taifa. Umuhimu wake ni sawia na uwepo wa vyama vya siasa. Hata Nyerere kalitetea bila mafanikio.

Mzee Pius Msekwa mwaka jana alisema tusichelewe zaidi kwenye hili. Ukweli wa mambo ni kwamba ikipita itakomesha tabia ya wanachama kuburuzwa na miungu watu ndani ya vyama.

Pamoja na hayo, kama kuna jambo lililonikuna kuhusiana na kikosi kazi ni kuangazia matatizo ya vyama vya siasa.

Nikinukuu sehemu ya taarifa hiyo: “Eneo jingine ambalo wadau wametoa maoni mengi ni kuhusu demokrasia ndani ya vyama vya siasa. Licha ya kwamba Tanzania ina uzoefu wa miaka 30 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, bado idadi kubwa ya vyama vya siasa vyenye usajili kamili, haviendeshwi kama taasisi na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.

Hali hii inathibitishwa na uwepo wa malalamiko mengi na migogoro ndani ya vyama vya siasa, inayotokana na ukiukwaji wa sheria ya vyama vya siasa, katiba na kanuni za vyama hivyo.

“Demokrasia ya ndani ya vyama vya siasa ni kiungo muhimu cha kukuza na kudumisha demokrasia nchini. Tafiti zinaonyesha kuwa, katika idadi kubwa ya vyama vya siasa ambavyo haviendeshwi kama taasisi na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia, hali hiyo inasababishwa na mambo kadhaa yakiwemo:

a) Kasumba ya waasisi wa vyama kutaka mawazo yao yafuatwe;

b) Idadi kubwa ya vyama vya siasa kutokuwa na fedha za kutosha kujiendesha, hivyo baadhi ya viongozi wa vyama hivyo kutumia fedha zao kugharamia shughuli za chama na hivyo kuwa na maamuzi makubwa ndani ya chama;

c) Idadi kubwa ya vyama vya siasa kutokuwa na mfumo ambao unawapa sauti wanachama na hivyo maamuzi mengi kufanywa na viongozi;

d) Idadi kubwa ya vyama vya siasa kutokuwa na kanuni madhubuti za uendeshaji wa shughuli zake za ndani, ikiwemo kanuni za fedha na kanuni za uchaguzi;

e) Idadi kubwa ya vyama vya siasa kutozingatia suala la jinsia, makundi maalumu na kudhibiti vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia;

f) Uwepo wa rushwa ndani ya vyama vya siasa, hasa wakati wa uchaguzi; na

g) Idadi kubwa ya vyama vya siasa kutokuwa na mfumo au mfumo mzuri wa kuzuia na kutatua migogoro ya ndani ya chama.”

Hii hali ya vyama vingi vya siasa Tanzania ni aibu. Na vyote vinaungana kimya kimya kuzuia uwepo wa mgombea binafsi. Hatuwezi kufika popote bila kwanza kujisahihisha.

Ni kichekesho kumsikia kiongozi wa chama cha upinzani akidai Tume Huru ya Uchaguzi wakati ndani ya chama chake huwezi hata kumkosoa. Tuache siasa za kitoto!

Andrew Bomani ni mwanasayansi wa siasa na kaimu katibu mwenezi wa UDP: 0784219535