#WC2018: Keane ataja kilichoiponza England kwa Ubelgiji

Muktasari:

  • Ubelgiji ilitwaa nafasi ya tatu baada ya kuilaza England mabao 2-1, licha ya timu hiyo kumiliki mpira muda mrefu.

Nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane, ametaja sababu ya England kufungwa na Ubelgiji katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu wa Kombe la Dunia.

Ubelgiji ilitwaa nafasi ya tatu baada ya kuilaza England mabao 2-1, licha ya timu hiyo kumiliki mpira muda mrefu.

Keane, alisema kilichoiponza England ni uzembe wa mabeki Danny Rose na Phil Jones aliodai walicheza chini ya kiwango.

Nguli huyo alitoa kauli hiyo wakati akichambua mchezo huo uliokuwa wa pili kwa timu hizo kuvaana kwenye Fainali za Kombe la Dunia.

Katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ambao timu hizo zilipangwa kundi moja, England ilichapwa bao 1-0 kabla ya juzi jioni kunyooshwa kwa mara ya pili.

Keane, ambaye pia aliwahi kuwa nahodha wa Ireland, alisema Rose na Jones waliigharimu England kushindwa kudhibiti mashambulizi ya akina Edin Hazard.

England ilifungwa bao la kwanza dakika ya tatu na sekunde ya 37, baada ya Thomas Meunier kumzidi maarifa Rose ambaye alitolewa kipindi cha pili kabla ya kufunga bao akiwa ana kwa ana na kipa Jordan Pickford.

Jones anayecheza Man United, alishindwa kumzuia Hazard aliyekuwa kwenye kiwango bora katika mchezo wa juzi kufunga bao la pili.

“Kila unapoangalia matukio ya makosa kila wiki yanazidi kuongezeka. Hakuna mabadiliko kwa upande wa Rose na Jones,”alisema Keane aliyekuwa akichambua mchezo huo kwenye televisheni.

Alisema Rose na Jones hawana uwezo wa kuzuia kwa kuwa sio mabeki bora licha ya kufanya kazi na makocha wakubwa Ulaya.

Nguli huyo alisema mabeki hao wanatakiwa kubalidika, vinginevyo wataendelea kufanya makosa mara kwa mara na kuzigharimu timu zao kwa kuwa hawana mfumo bora wa kukaba.

Alisema bao la mapema dakika ya tatu, liliwatoa mchezoni England na kusababisha Ubelgiji kuongeza kasi langoni mwa England.

Kocha wa England, Gareth Southgate alibaini udhaifu wa Rose ambaye ni beki wa kikosi cha kwanza Tottenham Hotspurs ambapo alimtoa baada ya upande wa kushoto kuzidiwa kwa mashambulizi.