TUONGEE KIUME: Neno mwanamume linavyotuumiza wanaume

Ulipokuwa mtoto, ukiumia, ukaanza kulia, kama utabahatika kuambiwa pole basi neno litakalofuata litakuwa ni “nyamaza, wanaume hawalii.”

Labda waliotulea walikuwa na maana nyingine, lakini iwe kwa kujua au bila kujua na sisi watoto wa kiume tumeelewa kuwa walikuwa wanamaanisha mtoto wa kiume kuhisi maumivu ni dalili ya udhaifu.

Matokeo yake tumekuwa wanaume tunaoishi kwenye mazingira magumu, yenye kutusababishia kila aina ya maumivu, lakini katu hatuthubutu kunyanyua midomo yetu kuyazungumza kwa sababu kufanya hivyo ni kuwa kinyume cha maana ya mwanamume, tuliambiwa wanaume hawalii.

Kwenye ofisi zetu tunafanya kazi kwenye mazingira magumu sana, tunabebeshwa majumuku yasiyotuhusu, tunanyanyaswa, tunatukanwa, tunadhalilishwa, tunadhulumiwa lakini hatuna kwa kusemea kwa sababu haiingii akilini mwanamume kwenda kushitaki eti unanyanyaswa au unadhalilishwa na bosi wako ambaye usikute ni mwanamume pia.

Sasa wewe utakuwa mwanamume gani? Kulalamika ni kwa ajili ya wanawake tu, mwanamume halii, ndivyo tulivyoambiwa kipindi tunakua.

Kwenye familia zetu tunaishi kwa mateso, hatuna furaha, tuna majukumu kuzidi uwezo wetu au kuzidi kiasi cha majukumu ambacho labda tulitakiwa kuwa nacho.

Unatakiwa uhudumie familia yako, yaani wewe, mkeo na watoto wako; bado unatakiwa uhudumie wazazi wako na wazazi wa mkeo na kamwe huwezi kudiriki kusema mzigo huu ni mzito, siuwezi.

Utakuwa ni mwanamume wa aina gani wewe? Mwanamume ni majukumu na hiyo ni kauli ya Mungu kutoka katika vitabu vyake takatifu, imeandikwa mwanamume atakula kwa jasho, utashitaki kwa nani?

Tena kwenye familia zetu tunaishi kwa mateso, tunaishi kwa hofu, tunanyanyaswa na kudhalilishwa, tukishindwa kuhudumia familia kiuchumi tunakumbwa na hofu ya kuonekana mwanaume suruali, wakati bado hofu ya kuitwa vibamia, hofu ya kukosa nguvu za kiume na hofu ya kushindwa kuwaridhisha wenza wetu kitandani inatutafuna, lakini yote haya hatuna jukwaa la kuyazungumzia kwa sababu sisi ni wanaume, mwanamume halii.

Matokeo yake tunaishia kuwa na msongo wa mawazo, tunaishia kuugua magonjwa ya akili yanayosababishwa na msongo wa mawazo, tunaishia kuwa walevi kwa sababu angalau tukilewa tunapata likizo ya joto kali na mateso ya maisha yetu halisi ambayo hatuwezi kuyazungumza kokote.

Matokeo yake, mwaka juzi, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa ripoti kuhusu vifo vinavyotokana na kujiua na kupitia ripoti hiyo ilionekana wanaume wanajiua zaidi ya wanawake, lakini yote haya yanaanzia kwenye neno mwanamume.

Baadhi ya matatizo yanatatulika kwa kuyazungumza tu, wanaume wenzangu tuhakikishe tunafanya hivyo kila tunapopata fursa, tuyaseme matatizo yanayotutesa wanaume.

Tusipokuwa makini tutajikuta tunaupoteza uanaume wetu halisi kwa kujibana sana kuhakikisha tunalinda uanaume unaoishi kwenye jina mwanamume.