TUONGEE KIUME: Usichotakiwa kufanya ukiwa mwanamume usiye na ajira

Katika kitabu chake cha Jobs Ends, milionea kijana Taylor Pearson ameandika, “kwa enzi hizi za matumizi makubwa ya mashine na intaneti, ajira yako ni kitu kinachoweza kupotea kufumba na kufumbua, kwa hiyo ujasiriamali ni salama zaidi ya ajira.”

Nasema katika enzi hizi za matumizi makubwa ya mashine na intaneti na siasa chafu za Kiafrika, hakuna usalama katika ajira wala ujasiriamali.

Kama unavyoweza kuamka ukaambiwa kampuni iliyokuajiri inapunguza wafanyakazi, ndivyo unavyoweza kuambiwa Serikali imepiga marufuku uuzwaji wa nguo za mitumba, wakati huo wewe una shehena ya mashati ya mitumba iko stoo.

Ninachojaribu kukwambia, siku yoyote unaweza kuwa huna chimbo la kupata pesa tena.

Na mwanamume bila pesa ni mwanamume suruali. Na hili sio mpaka uambiwe, hapana! Litaanzia kwako mwenyewe, taratibu utaanza kujiona unapoteza ‘hamu’ ya kuwa mwanamume.

 Sasa kila mwanamume anajua cha kufanya asipokuwa na kazi, ni kimoja tu, kutafuta kazi nyingine, lakini wengi hatujui nini hatutakiwi kufanya tusipokuwa na kazi, na leo ndiyo tutazungumzia hicho.

Usikae nyumbani; hata kama huna mahali pa maana pa kwenda, hakikisha haukai nyumbani kabisa. Amka asubuhi, nenda zako hata posta stesheni kaangalie jinsi reli ya SGR inavyojengwa siku nzima, ikifika jioni rudi nyumbani kama umetokea ofisini.

 Hufanyi hivi ili majirani wasijue kibarua kimeota nyasi, hapana. Unafanya hivi ili nyumbani wasikuzoee, kwa sababu kwa mazoea tu, unaweza kushangaa mkeo anakutuma ukalete mwiko, na ukiona umeshafikia huku, jua pointi inayofuata inakuhusu.

Usiwe na mtazamo hasi kwa mkeo; mwanamume ukiwa huna hela, huna kazi, uko nyumbani tu, unakuwa kama kamusi, kila neno litakalosemwa, wewe una tafsiri yake.

Mkeo akisema, “baba Rashidi, naomba muangalie mtoto mara moja niende dukani.” Wewe utasikia kasema, “baba Rashidi, kwa sababu huna hela na huna kazi, umekaa hapa siku nzima unapoteza muda kwa kuangalia TV utadhani unalipwa, sasa kaa na mtoto, mimi naenda dukani kununua cha kupika hapa, ili nipike, ule, ujaze hilo tumbo, upate nguvu ya kushika rimoti na kuendelea kubadilisha chaneli, na kupoteza muda zaidi.”

Kuanzia hapo utamjibu vibaya, atakujibu vibaya pia, mtajibizana, matokeo yake hakuna hata kitakachopikika kabisa.

Kwa hiyo ili usifike huku ni vyema sana kujitahidi kutokuwa na mtazamo hasi kuhusu mkeo.

Yaani usiwe na mtazamo hasi kiasi kwamba hata akisema jambo baya kukuhusu, wewe lichukulie chanya.

Usijifanye kila kitu kiko sawa; kwa sasa huna kazi, labda huna hela pia, kwa hiyo lazima kuna vitu havitaenda kama kawaida nyumbani, hili ni la kulitegemea. Kitu ambacho hutakiwi kufanya wakati kama huu ni kuigiza kila kitu kiko sawa, utaharibu.