Masaibu ya wanawake walioolewa kama hawajaolewa

Dar es Salaam. “Wengi hawazingatii wajibu wao, kila mmoja hajui anatakiwa afanye nini, au tupeane mitihani kabla ya kuingia kwenye ndoa?

“Mtu anaweza kuwa na vyeti vingi vya elimu lakini hajui wajibu wake wa ndoa ni nini. Ndani ya wiki mbili ndoa imevunjika na tulichangishwa kweli, inaumiza sana.”

Hii ni kauli ya Dk Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu alipofungua kongamano la kwanza la kutafuta suluhisho la kukithiri kwa talaka nchini, lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Waziri pia alitaja sababu za kuwapo migogoro ndani ya ndoa kuwa ni mawasiliano hafifu ya wanandoa, hali ya kipato, wanandoa kutofahamu wajibu wao, mila na desturi zisizofaa, udhaifu wa malezi kwa watoto na taarifa zisizokuwa na uthibitisho.

Alichosema Dk Gwajima kinaungwa mkono na baadhi ya wanawake waliozungumza na Mwananchi, wakieleza kwamba, ingawa wamo ndani ya ndoa kwa miaka kadhaa, maisha yao ni sawa na kama vile hawajaolewa kwa kuwa hubeba majukumu yote ya kulea familia.

“Nina miaka 10 ya kumiliki cheti cha ndoa na kuishi na mwanamume nyumba moja lakini kwa uhalisia, maana halisi ya ndoa niliishi ndani ya mwaka mmoja pekee.
“Baada ya hapo tunaishi kama watu wenye uhusiano kwa sababu tayari tuna watoto na tunalala kitanda kimoja, lakini ukweli ni kwamba kila mtu ana maisha yake.

Hakuna upendo kati yetu, mwanamume ameamua kuwa na maisha yake, hataki kujihusisha na kitu chochote kinachohusu familia hii. Hajui watoto wanakula nini, wanasomaje na maisha yao kwa ujumla, maana kila unachomwambia kuhusu fedha anakwambia hana. Kwa kifupi nimeolewa ila naishi kama nisiyeolewa.”

Ni kauli ya Siwema (si jina halisi), anayeeleza mzigo wa majukumu anayoachiwa na mume wake.

“Nimechoka kupigizana kelele na mtu asiyetaka kuwajibika. Si kwamba hana uwezo, ana shughuli za kumuingizia kipato, ila naona ni tabia iliyo ndani yake hataki kuwajabika,” anasema Siwema.

Kwa upande wake, Clara (si jina halisi) aliye ndani ya ndoa kwa takribani miaka mitano anaeleza:

“Unaishi na mume kwenye nyumba lakini kodi, ada, chakula na gharama zote za nyumbani zinakuangalia wewe, mwenzako hana msaada na ndiyo maana unasikia wanawake wa siku hizi wana mambo mengi. Ni vigumu kutulia ukiwa na mwenza wa aina hii, hata kichwa hakiwezi kuwa sawa, muda wote una mahangaiko mara Vicoba, Finca, Brac kote huko unatafuta mikopo ili mambo yaende.”

Wakati wanawake hawa wakisema hayo, hivi karibuni mtangazaji wa redio, Loveness Malinzi maarufu Diva aliweka wazi maisha anayopitia kwenye ndoa akisema; “Niliamini ndoa ni yale maneno aliyoniambia awali kwamba atanilinda na siku zote atakuwa kwa ajili yangu, mambo yalikuwa kinyume chake, mimi ndiye niliyekuwa namlinda na kuhangaika kwa ajili yake.”

Simulizi hizi ni kielelezo cha maisha ya baadhi ya wanawake wanaoachiwa mzigo wa majukumu ya kulea familia, hali inayowasababisha kufanya mambo zaidi ya uwezo wao.

Baadhi wanaeleza tabia ya wanaume kukwepa majukumu yao ya kiuchumi kwa familia ni miongoni mwa sababu zinazowasukuma kuchepuka ili kupata watu wa kuwasaidia na wakati mwingine kuwapa faraja.

Tofauti na wanawake hao, Ramadhan Digosi, mkazi wa Madale yeye anasema: “Hawa wanawake wakiwa na elimu na hela ni tatizo. Inaweza ikatokea siku zote unamhudumia lakini mambo yakabadilika uchumi ukiyumba yeye akahudumia familia, balaa itaanzia hapo. Dharau, kejeli na kila aina ya udhalilishaji, sasa mwanamume ni vigumu kuvumilia hayo.”

Katika uchambuzi wake, mwanasaikolojia Dk Chris Mauki aliwahi kusema; “Kuna kampeni nyingi zinaendelea za kumuinua mwanamke, zimekuwa na mafanikio, sasa hivi watoto wa kike wanasoma, wanapata kazi, wanafanya biashara, kwa kifupi wako vizuri kiuchumi, wanajitambua na kujiamini.

“Swali linakuja je, wanaume wameandaliwa kuishi na hawa wanawake walioinuliwa na kujitambua? Jibu ni hapana, na ndiyo maana unaweza kukuta kwenye nyumba zile hatua anazopiga mwanamke kwa mwanamume akaona kama ni dharau.”
 

Kiini cha tatizo

Mshauri wa uhusiano, Deogratius Sukambi anasema tatizo ni kubwa kuliko inavyoelezwa na upo uwezekano miaka 15 hadi 20 ijayo hali ikawa mbaya zaidi kutokana na malezi wanayopewa watoto.

Anawagawa wanaume wenye tabia hizo katika makundi matatu, la kwanza ni wanaopenda kuhudumiwa, pili wanaotambua majukumu yao lakini hawana uwezo, na la tatu ni wanaoamua kuacha majukumu yao baada ya kuona wanawake wanayabeba.

Anasema wa kundi la kwanza ni wasiotaka kujishughulisha kwa chochote wakiamini wanastahili kulelewa, huku wa kundi la pili wakifahamu na kutambua majukumu yao lakini hawana uwezo, hivyo huyaacha kwa wenza wao.

Kundi la tatu anasema huacha kuhudumia familia kwa kukusudia wanapoona mwanamke anabeba majukumu yake. Anasema hili ni kundi la hatari zaidi.
Katika kukabiliana nalo, anasema ni muhimu mwanamke kutambua mwisho wa majukumu yake na kumuacha mwenza wake atimize ya kwake, kinyume cha hapo mwanamume ataona amedharauliwa.

“Si kitu cha kawaida mwanamume kutegemea kuhudumiwa na mwanamke au kuacha majukumu yake yafanywe na mkewe. Inapofika hatua hii, lazima tujiulize tumekosea wapi, maana tusipoangalia kama wanajamii hali itakuwa zaidi ya ilivyo sasa,” anasema.

Sukambi anasema kumekuwa na wimbi la wanawake kubeba majukumu ya familia na watoto, hivyo wanaume wanapooa huamini wake zao watawasaidia kubeba majukumu.

“Tunapozungumzia uchumi shirikishi, wanawake wamevuka mpaka na kwa sababu hiyo, wameachiwa majukumu ya kutunza na kuhudumia familia. Unapotengeneza usawa kwenye kutekeleza majukumu ya familia na mwanamke akafanya basi mwanamume anaona anaweza kumuachia, hasa ikitokea amefanya bila ridhaa ya mume.

“Ifahamike kwamba taasisi ya ndoa kiongozi wake ni mwanamume na kutokana na uongozi huo, basi anatakiwa kubeba majukumu yote ya familia kuanzia mwanzo hadi mwisho. Mwanamke ataingia kama msaidizi, hivyo atafanya pale atakapoelekezwa kufanya,” anasema Sukambi.

Anasema kinachotokea kwa wanawake wengi ni kufuata hisia zao na kuamua kubeba majukumu ya mume akiamini ananusuru mambo yasiharibike, matokeo yake huachiwa mzigo.

“Kutokana na kutawaliwa na hisia utakuta mwanamke anaona mtoto hajalipiwa ada anakimbia kulipa, chakula hakipo nyumbani ananunua tena bila kupata ridhaa ya mwenza wake, hapa ndipo tatizo linapoanzia. Mwanamke kazi yake ni kumsaidia mumewe, kama mwanamume hafanyi anavyotakiwa jukumu la mwanamke siyo yeye kuyafanya, bali kumsaidia jinsi ya kufanya majukumu hayo,” anasema.
 

Viongozi wa dini

Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Taifa ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka, anasema ni muhimu kwa jamii kurudi katika misingi ya dini na kuzingatia inachoelekeza kuhusu ndoa.

“Ukisimamia misingi ya dini huwezi kupata shida, turudi katika dini tuangalie inatuelekeza kufanya nini katika ndoa. Tukiyajua na kuzingatia maelekezo basi kila kitu kitakwenda sawia.

“Mwanamume atajua wajibu wake na mwanamke atafahamu vitu gani azingatie kama mke ndani na nje ya nyumba. Nitoe mfano dini inazuia masuala ya kutoka nje ya ndoa, sasa kama unazingatia mafundisho hayo suala la michepuko halitakuwa na nafasi kwako. Amani, upendo na utulivu vitatawala kwenye ndoa yenu,” anasema.

Kwa upande wake, mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja anasema kuna umuhimu wa vijana wa kiume kuandaliwa kuingia kwenye ndoa.

Hananja anasema mwanamume bora ni yule anayebeba wajibu wa familia na kuitunza kama ambavyo vitabu vya dini vinaelekeza.

“Inashangaza siku hizi unakuta baba anajiondoa kwenye jukumu la kutunza familia kisa mama anafanya kazi, hii si sawa. Baba unapaswa kuonyesha nafasi yako ili hata watoto wajifunze kutoka kwako,” anasema.

Sifa nyingine ya mume kulingana na Hananja ni kutoa majibu ya maswali yanayoikumba familia.

“Usitengeneze mazingira kwamba kila wanachotaka watoto wanakimbilia kwa mama yao na wanakipata, ila wewe kila siku huna. Hapa utaitengeneza dharau,” anasema.
 

Ikoje kisaikolojia?

Mwanasaikolojia, Modesta Kimonga anasema kwa asili mwanamke ameumbwa kupokea, hivyo anapokuwa na mwenza halafu akakosa huduma muhimu hupata msongo wa mawazo kutokana na kulazimika kujitafutia.

“Kisaikolojia na kisosholojia mwanamke ana hali fulani ya kuhitaji kupatiwa, hata kama anaweza kukipata kile kitu, hiyo ni asili yake, sema mambo yanabadilika kwa sababu siku hizi wanawake wanafanya kazi,” anasema na kuongeza:

“Msongo wa mawazo kwa mwanamke unakuwa mara mbili, kwanza, ile kutoka nyumbani kwenda kujitafutia, pili akiwaza huyu mwanamume anapeleka wapi pesa yake au hanipendi, kwa nini ananionea, anamhudumia nani zaidi yangu.”

Anasema mwenendo wa wanaume hivi sasa kwa kiasi kikubwa unachangiwa na malezi kutokana na wengi kukua katika familia ambazo mama ni mpambanaji.

“Mtoto anakua akiona mama ndiyo kila kitu, baba hana muda, kwa hiyo anaamini hivyo ndivyo inavyotakiwa kuwa, hata yeye akiwa na familia anamuachia mkewe,” anasema.
Florentine Senya, mtaalamu wa malezi wa kituo cha Maadili Senya, anaeleza nafasi ya baba katika familia nyingi hivi sasa imekuwa ndogo, huku mama akiwa mbadala wake.
Anasema hali hiyo imechangiwa na harakati za kumkomboa mwanamke ambazo zimemfanya awe imara kifikra na kiuchumi, hivyo kuwa tayari kubeba majukumu ya familia.

“Hii 50 kwa 50 imetafsiriwa vibaya. Wanawake wanabeba majukumu yasiyo yao, hilo linawafanya kinababa wajisahau. Matokeo yake wanakuwa tu kwenye familia lakini hawasimami kwenye nafasi zao,” anasema.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Rose Reuben anasema kukosekana kwa mawasiliano baina ya wenza kunachangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo.

“Kesi za aina hii huwa zinakuja (Tamwa) na zimegawanyika katika makundi mawili. Kuna wanaume ambao uwezo wao ni mdogo kuliko mahitaji wanayotaka wanawake. Wapo pia ambao ni kweli wametelekeza majukumu kwa wenza wao kwa sababu wanaweza kujitafutia. Kutatua hili tunakaa na wenza wote wawili na kuzungumza nao.

“Katika utatuzi wa kesi za aina hii wakati mwingine tunabaini wanawake wanahitaji makubwa kuliko uwezo wa wenza wao, wapo pia ambao wanalazimika hata kuingia kwenye madeni ili kumudu makali ya kuendesha familia. Kitu muhimu tunachosisitiza ni mawasiliano. Inawezekana kabisa kama mnazungumza vizuri kusiwe na migogoro,” anasema Rose.
 

Nini Kifanyike

Ofisa ustawi wa jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha anasema ofisi yake hupokea mashauri ya aina hiyo, lakini yakiwa ndani ya kapu la migogoro ya wenza.
“Tunapata ripoti za kesi za aina hii kutoka huko chini, ni kweli tatizo lipo na linachangia kwa kiasi kikubwa kwenye migogoro ya ndoa ambayo inakuja kwenye ofisi zetu, wanaume wakielezwa kushindwa kuwajibika ndani ya familia zao.

“Changamoto hii ni matokeo ya watu kuingia kwenye majukumu ya kutengeneza familia wakiwa bado hawajajiandaa au hawako tayari kubeba jukumu, hata kama kipato chao kinaruhusu. Kingine ninachokiona ni kuteleza kwenye malezi, watoto wanalelewa katika mazingira ya kutopewa majukumu na hawapati fursa ya kujifunza kwa wazazi wao,” anasema Elisha.

Anatoa wito kwa wanawake wanaokabiliwa na changamoto za aina hiyo kutosita kuzitumia mamlaka husika kuwasilisha malalamiko na hasa pale wanaume wanapokuwa na uwezo lakini wanakwepa kutimiza majukumu yao.

Naye Sukambi anasema ili kubadili mwenendo huo, ni muhimu kuwekeza nguvu kubwa katika malezi ili watoto walelewe katika mazingira yatakayochangamsha ubongo wao.

“Tusiwalee watoto kama kuku wa kizungu, mtoto anapaswa kuelewa si kila anachotaka atapata kwa wakati anaotaka. Siku hizi utasikia mtoto anaamua shule hii haitaki anataka ile, ni muhimu wazazi tuwafundishe kwamba kwenye ulimwengu huu si kila unachotaka utakipata kwa urahisi. Hii haimsaidii mtoto, anakua akiamini anastahili kupewa kila anachohitaji. Hili ni bomu linalokuja miaka 20 ijayo kutokana na wazazi wengi tunavyolea watoto,” anasema.

Kwa upande wake, Mchungaji Hananja anashauri: “Mahubiri yetu yajikite kusema ukweli wa hali ilivyo sasa. Kumekuwa na semina nyingi za wanawake kwenye nyumba za ibada. Ifike mahali sasa turudi kwa wanaume na vijana wetu wa kiume tuwafundishe nafasi yao na ya mwanamke katika dunia ya sasa.

“Hali ikiendelea kuwa hivi migogoro itakuwa mingi, ndoa zitasambaratika na matukio ya kudhuriana hadi kuuana. Tusisubiri waumini waishe ndiyo tuanze kuhubiri, tuanze sasa kunusuru hatari inayoweza kujitokeza mbele,” anasema.
 

Hali ya migogoro

Takwimu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu zinaonyesha migogoro 28,773 ya wanandoa imepokewa kati ya Julai, 2022 na Aprili mwaka huu.

Kati ya migogoro hiyo, 22,844 ilisuluhishwa, huku 5,929 ikikosa usuluhishi licha ya kukatiwa rufaa ngazi ya Mahakama.
Kutokana na migogoro hiyo, watoto 18,922 waliathiriwa katika malezi, baadhi wakikimbilia mitaani, kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya au ndoa za utotoni.