UCHAMBUZI: Wafugaji wa vipepeo na ‘kilio cha samaki’

Ni matarajio yetu kwamba mabadiliko ya Baraza la Mawaziri aliyofanya Rais John Magufuli hivi karibuni yanaweza kubadili mwelekeo wa utendaji kazi katika wizara mbalimbali, ikiwamo kufanyia kazi haraka vikwazo vilivyokuwapo awali.

Matumaini haya yanakuja kutokana na kauli aliyowahi kuitoa Rais Magufuli akiwa katika ziara mkoani Tanga Septemba mwaka huu, kwamba baadhi ya malalamiko

anayokumbana nayo yalistahili kumalizwa na mawaziri wake badala ya kumngoja yeye.

Kauli hii ya mkuu wa nchi ilikuwa ni nzito na iliambatana na kuwasuta baadhi ya mawaziri kwa kutofanya kazi jinsi anavyotaka, pia ni ujumbe ambao unastahili kufanyiwa kazi na mawaziri wote hasa ikizingatiwa kuwa wengi wao ni vijana.

Wakati mawaziri hao wakiendelea kujipanga jinsi watakavyotatua kero za wananchi, ningependa kwa leo kuwasilisha kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, kilio cha wafugaji wa vipepeo waliopo katika Tarafa ya Amani katika milima ya Usambara Mashariki na katika vitongoji vya Wilaya ya Korogwe vilivyo katika mtandao wa milima ya tao la mashariki.

Huko kuna wafugaji wa vipepeo ambao kuanzia mwaka 2003 walipoanza kufanya shughuli hiyo baada ya kupelekewa elimu hiyo na mtaalamu mmoja kutoka nchini Ujerumani.

Wafugaji hao walishaanza kupiga hatua kimaendeleo kutokana na ubora wa vipepeo vyao na vinavyovutia walifikia hatua ya kuteka soko la wadudu hao duniani, hasa nchini Marekani.

Jumla ya wafugaji 156 waliopo katika vijiji sita vinavyozunguka hifadhi ya Amani walikuwa wakiingizia nchi dola za Marekani 90,000 kwa mwaka na kati ya hizo Sh500 milioni zikienda moja kwa moja kwa wafugaji hao kutokana na kuuza nje vipepeo.

Kutokana na biashara hiyo maisha ya wafugaji hao yalianza kubadilika kwani waliweza kujenga nyumba za kisasa na kuweka nishati huku vijana wakimudu

kununua vyombo vya usafiri na hivyo kuondokana na vitendo vya uharibifu wa mazingira ya Hifadhi ya Amani.

Hata hivyo, Baadaye Serikali iliingiza vipepeo kama viumbe hao waliopigwa marufuku kusafirishwa na kufunga mlango huo wa ajira na chanzo cha fedha za kigeni.

Kutokana na uamuzi huo wa waziri wa zamani wa wizara hiyo, Profesa Jumanne Maghembe, wafugaji hao wanaomba Serikali iwaondolee zuio la kuuza nje vipepeo ili waendelee kama kawaida.

Wanatoa hoja kwamba vipepeo havikustahili kuwemo kwenye orodha hiyo kutokana na ukweli kwamba aina ya ufugaji wake kuanzia kutega mayai

kuyakuza, kutotoa na kuvisafirisha nje vinatokana na juhudi za mkulima tofauti na viumbe wengine hai.

Hoja nyingine ni kwamba kutokana na ushindani wa soko duniani, iwapo wafugaji wa amani watashindwa kuuza vipepeo kwa muda mrefu ni wazi kuwa soko hilo

litatekwa na nchi nyingine na kulirejesha haitakuwa rahisi.

Kilio chao kinakolezwa na kauli ya Maghembe aliyoitoa siku moja kabla ya Rais kutangaza mawaziri wapya na kumwacha, kuwa Serikali haitatoa kibali kwa vipepeo na kuwataka wafugaji hao kusubiri taratibu zilizosababisha kupigwa marufuku zikamilike.

Kauli hiyo ndiyo inayowafanya wafugaji hao wakimbilia kwa Dk Kigwangalla ili aone machozi yao yasiwe kama samaki yanayoishia majini bila kuonekana.

Ningependa kufikisha kilio cha wafugaji hao kwa Waziri Kigwangalla na baada ya kukisikia afunge safari awatembelee wafugaji wa vipepeo wa amani ili ashuhudie kinachotendeka na kuwatendea haki.

0658376434