Ukitaka kujua ustaa haudumu muulize Mr Nice, Dudu Baya

Muktasari:

Kuna wasanii kwa sasa nikimwandika inabidi nimtambulishe kwa kukumbushia kazi zake. Kwa wale wa kizazi cha zamani kidogo wanaweza kumtambua ila kwa wasomaji wa kizazi kipya watamwona chipukizi.

Nimekuwa mwandishi wa habari za burudani kwa miaka minane sasa. Katika kipindi hiki nimeandika habari za msanii chipukizi, akawa staa halafu akarudi kuwa chipukizi tena.

Kuna wasanii kwa sasa nikimwandika inabidi nimtambulishe kwa kukumbushia kazi zake. Kwa wale wa kizazi cha zamani kidogo wanaweza kumtambua ila kwa wasomaji wa kizazi kipya watamwona chipukizi.

Nathubutu kusema maisha ya umaarufu kwa asilimia 80 ya wasanii wote nchini ni miaka mitano tu.

Kwa maana hii wasanii wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi hasa baada ya umaarufu wao kushuka.

Mara nyingi huanza kupata pesa katika umri mdogo na umaarufu hudumu kwa kipindi kifupi. Hapa nchini msanii anaweza kuwa katika kilele cha mafanikio kwa miaka isiyozidi mitano.

Kipindi cha umaarufu wake ndiyo huwa cha kupata pesa. Mialiko ya matamasha, mikataba ya matangazo na dili nyingine huja wakati huu, lakini umaarufu unapopungua na mirija yote ya pesa hukata na hapa ndipo yanapoanza matatizo ambayo tumeshuhudia yakiwasukuma wasanii kujiingiza katika vitendo visivyofaa.

Utafiti uliofanywa mwaka juzi na Taasisi ya Marekani ya National Bureau of Economic Statistic inasema msanii wa Afrika anaweza kuingiza mpaka Sh4 bilioni katika kipindi cha miaka mitano ya mafanikio yake.

Swali linabaki je, msanii huyu anazifanyia nini pesa hizi wakati zinaingia au anaishia kuzitapanya akiamini kuwa kesho zitakuja nyingine?

Niwakumbushe tu kujituma katika kipindi hiki cha miaka mitano ya umaarufu kwa kuwekeza na pia angalau kuhakikisha baada ya muda huo jina halishuki moja kwa moja.

Wasanii kama AY, Mwana FA, Profesa Jay, Lady Jay Dee, Chegge, Mr Blue na wengine wamejitahidi kubaki katika mstari (nachelea kusema wa juu), lakini ingefaa wengine wote wabaki hivi.

Haitawezekana kamwe msanii kubaki juu kwa kuwa nyakati hubadilika na pia mahitaji huwa tofauti. Kwa maana hii hao niliowataja ni wa kupigiwa mfano.

Wasanii kama Dudu Baya, Mr Nice, Chid Benz, Ray C ni baadhi ya waliowahi kuwa juu. Wamewahi kufikia kilele cha mafanikio katika muziki, lakini maisha yao sasa yanawakumbusha kuwa ni muhimu kuwekeza katika kazi hii kwa umakini.