URITHI WETU: Chifu Mkwawa alivyowachapa wakoloni Lugalo

Muktasari:

Huwezi kuwazungumzia Wahehe ukaeleweka vizuri bila kumtaja Chifu wao, Mkwawa.

Huwezi kuwazungumzia Wahehe ukaeleweka vizuri bila kumtaja Chifu wao, Mkwawa.

Chifu Mkwawa alizaliwa mwaka 1855, akapewa jina la Ndesalasi, maana yake ikiwa ni “mtundu au mdadisi”.

Historia inaonyesha kuwa alizaliwa katika kijiji cha Luhota, Wilaya ya Iringa na kwamba jina la Mkwawa linatokana na neno Mkwavinyika likimaanisha ‘mshindi wa nchi nyingi’.

Sifa kubwa ya Mkwawa ilikuwa ni nguvu na uwezo wake wa kupigana vita.

Simulizi zinaonyesha kuwa ukubwani, miaka ya 1887 Mkwawa pia aliitwa ‘Mtwa Mkwava Mkwavinyika Mahinya Yilimwiganga Mkali Kuvago Kuvadala Tage Matenengo Manwiwage Seguniwagula Gumganga’.

Jina hilo linamaanisha ni “Mtawala, mtekaji wa nyika, mkali kwa wanaume, mpole kwa wanawake asiyetabirika, aliyeshindikanika, mbabe mwenye nguvu, udongo pekee ndio utakaomuweza”.


Vita ya Mkwawa na Wajerumani

Ni vita iliyopiganwa mwaka 1891. Kiongozi wa kikosi cha maofisa Wajerumani 13, Von Zelewski pamoja na askari 320, baadhi wakiwa Waafrika kutoka Sudan, pamoja na wapagazi 113, aliwadharau Wahehe kwa sababu wao walikuwa na silaha duni kama mikuki na pinde huku wao wakiwa na bunduki, mizinga na mabomu.

Historia inaeleza kuwa akiwa njiani na kikosi chake, alikutana na Wahehe watatu waliomkaribia, naye akaagiza wauawe bila mazungumzo.

Wahehe hao walikuwa mabalozi wa Mkwawa aliyetaka kufanya majadiliano na Wajerumani.

Von Zelewski aliongoza kikosi chake mpaka aneo la Lugalo, hiyo ilikuwa ni Agosti 17, 1981.

Meneja wa mradi wa fahari yetu Tanzania, unaozungumzia historia ya Iringa na Wahehe, Dk Jimson Sanga katika simulizi yake, anasema wakiwa karibu na eneo la Lugalo, askari wa Kijerumani walikutana na nyasi ndefu hivyo wakalazimika kupita hapo.

Mkwawa alikuwa anamsubiri na alikuwa na askari wake 3,000 na walinyamaza mpaka Wajerumani waliposogea na kuwashambulia.

Inasadikiwa kuwa Wajerumani walikosa muda wa kuandaa silaha zao, hivyo sehemu kubwa ya askari waliuawa, akiwemo Von Zelewski.

Kutokana na ushindi huo Wahehe walipata bunduki 300 za kisasa walizokusanya, mizinga miwili na bomu moja.

Gerald Malangalila, mzee wa kimila wa kabila hilo anasema vita hiyo ilimpatia sifa kubwa Mkwawa kwa kuwa alipigana akiwa na silaha duni.

Mtembeza wageni katika makumbusho ya Boma – Iringa mjini, Aboubakar Said anasema mpaka sasa mzinga mmoja uliotekwa wakati huo bado upo, umehifadhiwa kwenye makumbusho.


Jina la Lugalo

Lugalo ni eneo ambalo Mkwawa aliwashinda Wajerumani na kupata umaarufu mkubwa.

Baada ya Uhuru, Mwalimu Julius Nyerere aliamua kambi kubwa ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania iliyoko jijini Dar es Salaam iitwe Lugalo.

Mzee Malangalila anasema, Mwalimu Nyerere alifanya hivyo kama kumbukumbu ya kipigo cha Wahehe dhidi ya Wajerumani.

Inasadikiwa baada ya shambulizi la Lugalo, Wajerumani walikwenda kujipanga upya kwa ajili ya kumshambulia Mkwawa na jeshi lake.

Wakati huo, Mkwawa alikuwa ameweka makazi yake katika eneo la Kalenga, nje kidogo ya mji wa Iringa.

Miaka mtatu baadaye, Wajerumani walirudi wakiwa wamejipanga chini ya Kanali Friedrick Von Scheele na kuanza kushambulia ngome ya Kalenga.

Said anasimulia kuwa kikosi kipya cha Wajerumani kilitumia zana za kisasa zaidi na za masafa, ikiwamo mizinga ambayo walikuwa wakipiga kutoka katika eneo la Tosamaganga.

Mzee Malangalila anasema, wakati walipokuwa wakipiga Wahehe, walianza kusema ‘vitosa maganga’ ikimaanisha wanarusha mawe, kumbe yalikuwa mabomu na hiyo ndiyo ikawa mwanzo wa eneo hilo kuitwa Tosamaganga.


Mama ajiua

Baada ya mama yake Mkwawa kuona hali tete aliamua kwenda kujitumbukiza kwenye maji eneo la Kikongoma.

“Mpaka sasa hili eneo ni maarufu, linafaa kwa utalii na kuna wageni wa ndani na nje huwa wanaenda kutembelea,” anasema Dk Sanga ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa.

Pia inasadikiwa mama yake Mkwawa alikuwa akiandaa dawa kwa ajili ya askari wa Kihehe na inasadikiwa alienda kujiua akiwa na kikapu chake cha dawa ili wapinzani wasiichukue.

Pamoja na shambulio hilo, Mkwawa alifanikiwa kutoroka akakimbilia porini ambako alianza kupigana vita ya msituni.

“Akiwa porini alitumia mbuyu kama chakula na alikaa huko kwa miaka minne kabla ya kuzingirwa katika maficho yake, eneo la Mlambalasi,” anasema Dk Sanga.


Mkwawa ajiua

Simulizi za Mkwawa zinaeleza kuwa, mwaka 1898 chifu huyo alipoona amezingirwa hakutaka kuuawa na Wajerumani wala kukamatwa, akaamua kuwatuma askari watatu aliokuwa nao wakachote maji.

Mzee Malangalila anasema, askari wawili kati ya watatu waliokuwa naye walikubali kwenda kuteka maji lakini mmoja aligoma.

Anasema wakati huo alikuwa amekoka moto ili akijiua mwili wake uangukie motoni kisha kuteketea, ili Wajerumani wasiambulie hata mwili.

“Kwa sababu askari mmoja hakutaka kuondoka, alimpiga risasi kisha akajipiga yeye, lakini bahati mbaya mwili haukuangukia kwenye moto kama alivyotaka,” anasimulia Mzee Malangalila.

Mzee Malangalila anasema kwa sababu mlio wa risasi uliwastua Wajerumani waliokuwa karibu na eneo hilo, walifuatilia na walipofika eneo alipojiulia waliamua kumkata kichwa, wakatenganisha na kiwiliwili kama ushahidi.

“Walichukua kichwa chake wakaondoka nacho, walipeleka Ujerumani kama ushahidi na mwili ukazikwa kwenye eneo hilo. Mpaka sasa kuna kaburi lake eneo hilo,” anasema.

Kichwa cha Mkwawa kilikabidhiwa kwa Kapteni Tom von Prince na kutumwa Berlin – Ujerumani na kuhifadhiwa makumbusho.


Utawala wa Waingereza

Katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914-18), majeshi ya Uingereza kwa msaada wa mashujaa wa Kihehe yaliichukua Iringa kutoka kwa Wajerumani mwaka 1916.

Ili kulipa fadhila ya msaada waliotoa Wahehe wakati wa vita, utawala wa Waingereza kwa niaba ya Wahehe ulitaka kurudishwa kwa fuvu la Mkwawa.

Hatimaye, Julai 9, mwaka 1954 fuvu la Mkwawa lilirejeshwa nchini na kuhifadhiwa kwenye jengo la makumbusho katika Kijiji cha Kalenga.

Mjukuu wa Mkwawa, Adam Sapi Mkwawa ambaye alikuwa Spika wa Kwanza wa Bunge la Tanzania ndiye aliyelipokea fuvu hilo.

Hadi leo, Chifu Mkwawa ni shujaa maarufu wa Taifa la Tanzania, akiwakilisha Wahehe.

“Haiba yake ya upinzani mkali dhidi ya Wajerumani inaonekana kama mshale wa awali kwa Taifa kutaka kujitawala na hii ilitoa msukumo kwa nchi kuanza harakati za kupigania uhuru wake,” anasema Dk Sanga.

Kesho ni mwisho wa simulizi hii na tutaangazia mila maarufu kuhusu Wahehe na pia madai kuwa watu wa kabila hilo ni wapenzi wa nyama ya mbwa na ni wepesi kujitoa uhai.