Uzalendo si muujiza, ni uwekezaji

Muktasari:

  • Kitu nitakachokigusa hapa ni uzalendo wake. Waziri Mkuu kujiuzulu si jambo la jepesi. Lakini kuzingatia maslahi ya Taifa dhidi ya maslahi binafsi ni uzalendo uliotukuka. Nakumbuka Rais wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliwahi kujing’atua kutoka nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ili kulinusuru Taifa baada ya kadhia ya mauaji ya vikongwe yaliyofanywa na vyombo vya usalama.

Dar es Salaam. Kwanza tupeane pole kwa kumpoteza aliyekuwa kiongozi wetu mahiri, Waziri Mkuu mstaafu bwana Lowassa. Ukiachilia mbali kashfa zilizompelekea kujiuzulu uongozi wake wa juu, tusherehekee maendeleo ambayo kwa nguvu za utashi wake yalionekana bila kupingwa. Tukizungumzia matatizo yaliyokuwa kama kansa lakini yakapata ufumbuzi kwa kichwa chake (kama sekta ya elimu na bodaboda) nadhani nimeeleweka. Mungu ampe pumziko la kheri.

Kitu nitakachokigusa hapa ni uzalendo wake. Waziri Mkuu kujiuzulu si jambo la jepesi. Lakini kuzingatia maslahi ya Taifa dhidi ya maslahi binafsi ni uzalendo uliotukuka. Nakumbuka Rais wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi aliwahi kujing’atua kutoka nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ili kulinusuru Taifa baada ya kadhia ya mauaji ya vikongwe yaliyofanywa na vyombo vya usalama.

Mzee Mwinyi alitaja sababu za kujiuzulu kwake nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa kulitokana na kulinda heshima ya Taifa na ya Rais wa awamu ya kwanza. Hata hivyo, alipata amani ya moyoni baada ya kujiuzulu kwake. Waswahili husema “Mlango mmoja ukifungwa, mingine inafunguka”.

Akizungumza katika hafla ya siku ya wazee duniani, Mzee Mwinyi alisema Mwaka 1976 akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alilazimika kujiuzulu nafasi yake baada ya kutokea mauaji katika Mkoa wa Shinyanga. Lakini miaka tisa baadaye kwa kuzingatia uzalendo wake kwa Taifa, alipendekezwa na Mwalimu Nyerere na kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha miaka kumi.

Mwezi huu tumeshuhudia uzalendo mkubwa ndani ya Taifa la Cote d’Ivoire. Hakuna aliye na shaka juu ya uwekezaji wao wa muda mrefu kwenye nyanja za michezo. Lakini mwaka huu walipoingia kwenye michuano ya Afcon 2023, walikuwa kama sisi maana walikuwa wakipigwa hadi kupoteza matumaini. Lakini Mungu bariki waliponusurika kutolewa walijijenga upya na kuhakikisha ndoo inabaki nyumbani.

Yeyote aliyeutazama mtanange wa fainali dhidi ya Nigeria lazima atakuwa na ya kuhadithia. Mpira ulianza kama vita, na ikumbukwe Wanaijeria walisindikizwa na nyota wao wa zamani ili kuwaongezea wachezaji wao jambo hilohilo la uzalendo. Lakini kwa upande wa Cote d’Ivoire, licha ya mastaa wa zamani pia walisindikizwa na viongozi wakuu wa serikali pamoja na wa michezo. Nilipomsikia nguli wa muziki Alpha Blondie akitema cheche nikajua jambo limeisha.

Ama kwa hakika vijana walipambana kama wanajeshi wanaoikomboa nchi yao baada ya kuvamiwa na adui. Nikivuta taswira ya miaka ya themanini, naiona Taifa Stars na klabu za soka hapa nchini zilivyokuwa zikipambana kwa jasho na damu katika kuipandisha Tanzania kwenye ramani ya soka la Afrika na dunia. Makipa wetu waliwahi kutishiwa na silaha za moto uwanjani, lakini walikataa kuachia magoli.

Kwenye tukio moja kule Misri tuliwahi kuzimiwa umeme ndipo tukafungwa. Kwa kuwa tulikuwa kwao na walishafanya mipango na waamuzi, hatukuwa na jinsi zaidi ya kurudi kinyonge. Lakini ukitazama uzalendo uliobebwa na Watanzania utahakikisha kuwa hata wao hawakuwa wakituchukulia poa. Wakati mwingine wachezaji wetu walipoonewa walifikia kusema “kama mbwai na iwe mbwai”, zikapigwa ngumi!

Sijui ni mzimu gani uliokuja kutuangusha. Wakati ule wenzetu waliendelea kuzijenga timu zao kwa faida inayoonekana leo, sisi tulikuwa tukihangaika na siasa na mambo mengine. Leo tunapeleka timu zisizo za kishindani na kuziahidi mabilioni iwapo zitafanya vizuri. Kwangu hili halina tofauti na kumpeleka mtoto asiyesoma kwenye mitihani na kumuahidi zawadi nono iwapo atafaulu.

Kila jambo linataka uwekezaji. Huwezi kujidanganya kuwa utaweza wakati hakuna ulichowekeza tangu miongo iliyopita. Wenzetu wanaosomeka leo michezoni waliwekeza sera za michezo kwenye mipango ya nchi zao. Nasi kama tunataka kufika huko, basi tuwekeze kuanzia leo. Tukumbuke ujio wa Pan African ya mtaa wa Mkunguni, Pamba ya Mwanza, CDA ya Dodoma na zinginezo zilizowaweka roho juu Simba na Yanga.

Ikumbukwe pia sanaa na michezo viliwakutanisha washiriki kutoka ngazi ya Kata, Kijiji, Wilaya, Mkoa hadi Taifa kwenye mashindano. Sote tunakumbuka Umitashumta, Umisseta na michezo mingine ambayo ilipasua anga hadi kujulikana kimataifa. Huu ulikuwa ndiyo wakati ambao wanafunzi na wafanyakazi wa mashirika ya umma waliweza kujadili uzalendo wao kwa mapana yake.

Jirani zetu Wakenya walichoka na figisu za timu kongwe nchini mwao, Luo Union na Abaluhya. Timu hizi zilikuwa na mrengo wa makabila ya Wajaluo na Waluhya, yalikuwa ni makabila yenye uhasimu wa jadi. Kwa sababu ya kuendekeza ubabe wao, hakukuwa na uwekezaji kwenye michezo kwani makabila hayo ndiyo yaliyokuwa na uongozi wa Kenya. Kiwango cha mpira kilishuka hadi kufikia hadhi ya kichwa cha mwendawazimu, Wakenya wakazipiga chini timu hizo.

Hapa Bongo kulikuwa na uwekezaji mzuri wa Azam FC. Lakini kwa sababu zinazotajwa na baadhi ya wapenzi wa soka kuwa ni kupandikizwa U-simba na U-yanga, Azam ikapunguza kasi na kupoteza dira. Hatukatai kila mkoa zilikuwepo Simba na Yanga zao, lakini lengo halikuwa “uchawa” bali kupata timu kubwa za kuzihamasisha hizi ndogo. Tusipokuwa makini huu ndiyo utakuwa mwisho wetu. Kama tunataka ushindi tuwekeze kwanza.