Kitabu cha Lowassa kilivyofungwa Chadema

Edward Lowassa wakati anatambulishwa kwa mara ya kwanza katika Kamati kuu ya Chadema Bahari Beach Kunduchi jijini Dar es salaam.

Muktasari:

  • Julai 28, 2015, Edward Lowassa aliandika historia za siasa Tanzania baada ya kutangaza kung’oka chama tawala- Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na chama kikuu cha upinzani- Chadema.  Wengi walimfuata huko na baadaye waliunagana kurejea walikotoka.

Ugeni mkubwa uliingia Chadema Julai 28, 2015. Ugeni ulitokea CCM. Mwaka 2016, wageni walianza kurejea walipotoka. Ulipofika mwaka 2020, hatimaye, hakuna aliyekuwa amebaki.

Ugeni uliovamia Chadema Agosti 2015, ulitokana na matokeo ya mchakato wa uchaguzi wa awali ndani ya CCM kumpata mgombea urais. Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani, alikuwa mwenye nguvu nyingi. Hata hivyo, alikatwa.

Lowassa, na ile kauli mbiu yake ya “Safari ya Matumaini”, si uongo, alijenga matumaini makubwa kwa wafuasi wake, kundi kubwa la wana-CCM na Watanzania wengi kwamba ndiye angepewa tiketi ya CCM kugombea urais, kisha angekuwa Rais wa Tano.

Alijitengeneza au timu yake ilimtengeneza kuwa mwanasiasa mwenye nguvu nyingi. Nyendo zake zilitengeneza kishindo cha aina yake. Jinsi makundi ya watu, wakiwemo viongozi wa dini, walipotokeza kumshawishi agombee. Watu wakasema alikuwa anafanya maigizo.

Hatima ya Lowasa Chadema

Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye, alipomuonya Lowassa na wimbi lake la watu kumuomba agombee, Lowassa alijbu “siwezi kuzuia mafuriko kwa mikono”. Likawa jina lingine la utani “Mzee wa Mafuriko”.

Kila hatua ya Lowassa kuuelekea Urais wa Tanzania mwaka 2015, ilikuwa na kishindo. Alimwaga fedha makanisani na misikitini, watu walipohoji alipozitoa, alijibu “kwa marafiki”. Mamia ya mamilioni.

Uwanja wa Sheikh Amri Abed ulifurika Lowassa alipotangaza nia. Kisha ndege na chopa vilipasua mawingu, mabasi yaliyopambwa picha za Lowassa na yale maandishi “Safari ya Matumaini”, msururu wa Toyota Land Cruiser 200 series, yalizifanya barabara za nchi nzima kuwa na hekaheka. Lowassa alikuwa anazunguka kutafuta wadhamini.

Mamia elfu walijitokeza kumdhamini Lowassa. Udhamini ulikuwa wa kishindo. Kila kitu kilichomhusisha Lowassa na urais mwaka 2015, kilikuwa na kishindo kikubwa, hata alipokatwa, wengi walistaajabu. Ilionekana isingewezekana kukatwa.

Na kwa sababu Lowassa ndiye alikuwa ‘mmiliki’ wa vishindo vya siasa hasa za urais mwaka 2015, alipotangaza kuhama CCM na kujiunga Chadema, ulikuwa uhamaji wenye kishindo. Vigogo na wanachama waandamizi CCM walimfuata. Unaweza kuuita uhamaji wa mafuriko kutokana na ule msemo wake.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisalimian na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho Edward Lowassa wakati wa moja ya mikutano ya ndani ya chama hicho 2015 kuelekea uchaguzi mkuu.

Ni Lowassa aliyekuwa na vishindo vingi. Waliogoma kumpokea Chadema ilibidi waondoke wao. Dk Willibrod Slaa, alikuwa Katibu Mkuu Chadema, alipisha njia, Lowassa alipoingia na kuteuliwa kuwa mgombea urais. Slaa alipinga uamuzi wa kumpokea Lowassa.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015, Chadema waliungana na vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, kupitia mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuteua mgombea urais wa pamoja. Lowassa alipitishwa. Mwenyekiti wa Cuf, Prof Ibrahim Lipumba alijiuzulu, ingawa baadaye alirejea, alipoandika barua ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu.

Lowasa kujiunga Chadema

Mguu wa Lowassa Chadema, uliongozana na wengi. Wa kwanza ni veterani Mkomunisti, Kingunge Ngombale Mwiru, aliyekataa kuchukua kadi lakini alisema “aliunga mkono mabadiliko”, zaidi alipanda majukwaa ya Chadema kumwombea kura Lowassa.

Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Laurence Masha, Balozi Juma Mwapachu, walikuwa wenyeviti wa CCM, Hamis Mgeja (Shinyanga), Mgana Msindai (Singida) ni sehemu ya waliokuwa vigogo CCM ambao walipaza sauti ya “ulipo tupo”, kwamba popote Lowassa wangekwenda naye, wao wangemfuata.

Waziri Mkuu wa mihula yote miwili katika Serikali ya Awamu ya Tatu, Fredrick Sumaye, alishitua wengi alipoungana na Lowassa Chadema, wakati walipokuwa CCM, hawakupata kuelewana. Tambwe Hiza, mwana CUF aliyekimbilia CCM kipindi cha Ukatibu Mkuu wa Yusuf Makamba, naye alirejea upinzani, Chadema, kuungana na Lowassa.

Walikuwepo waliopigwa mwereka kura za maoni CCM katika vinyang'anyiro vya ubunge, nao walipanda ‘basi’ la Lowassa Chadema. Dk Milton Makongoro Mahanga na James Lembeli, walihamia Chadema baada ya kushindwa CCM.

Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, yeye alikuwa mbunge wa Viti Maalum (CCM) mwaka 2010-2015, na alitarajiwa kuwania kura za maoni kwenye chama hicho, alibadili gia dakika za mwishoni, akahamia Chadema ambako alipewa tiketi ya kugombea na kumshinda mwanasiasa mwandamizi nchini, Stephen Wasira.

Bulaya, pamoja na kwamba alihamia Chadema wakati wa vuguvugu la Lowassa, yeye hakuwa wale wa “Lowassa ulipo tupo”, kwani alihusishwa muda mrefu kujiunga na Chadema kutokana na urafiki wake mkubwa na Halima Mdee, mbunge wa Kawe na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha).

Naliweka sawa la uhamaji wa Bulaya ili kuwasilisha picha kubwa ya namna ambavyo “kitabu cha Lowassa Chadema” kilivyofungwa. Hakuna masalia yaliyobaki. Wengi wamerejea CCM, watatu walipokea wito wa Mungu.

Wa kwanza kurejea CCM, alikuwa Balozi Mwapachu, yeye mapema, Machi 2016, aliirejea kadi yake ya CCM, ofisi ya Kata ya Mikocheni, na aliyefunga kitabu ni Dk Mahanga, aliyefariki dunia Machi 23, mwaka huu.

Tambwe alifariki dunia mapema Februari 2018, akiwa bado Chadema. Februari 2, 2018, Kingunge alifariki dunia. Japokuwa Kingunge hakuwahi kuchukua kadi ya Chadema, lakini alikuwa upande wa chama hicho na Lowassa mpaka mauti yalipomfika.

Kutoka Machi 2016, Balozi Mwapachu alipowahi CCM na kuwa wa kwanza kusifu utendaji wa Rais John Magufuli, huku akitamka kwamba alikosea kuhama, wengine walirejea CCM kwa mafungu.

Lowasa arudi CCM

Msindai alipokelewa CCM kwenye Mkutano Mkuu Maalum, Dodoma, ulioketi kumchagua Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti wa CCM, baada ya mtangulizi wake kuamua kumkabidhi kofia hiyo ya uongozi wa chama mapema.

Msindai, alingozana kurejea CCM na Moses Machali aliyetokea ACT-Wazalendo na Fred Mpendazoe, aliyetokea Chadema. Mpendazoe hakuwa wa upepo wa Lowassa. Yeye alijiunga Chadema tangu mwaka 2010 akitokea kilichokuwa Chama Cha Jamii (CCJ). Kabla ya CCJ alikuwa mbunge wa Kishapu (CCM).

Masha na wengine walihama kwa awamu kurejea CCM. Masha baada ya kukosa ubunge wa Afrika Mashariki, kwa tiketi ya Chadema, hakuchukua muda mrefu alirejea CCM huku akisema “wapinzani hawawezi kushinda dola”.

Machi Mosi, mwaka jana, Lowassa alirejea CCM. Baada ya hapo Mgeja alitimiza usemi wa “ulipo tupo”, naye alikwenda CCM. Familia ya Lowassa pia ilitangaza kurejea CCM.

Mpaka mwishoni mwa mwaka 2019, Sumaye na Mahanga ndio walionekana wagumu kurejea CCM. Desemba 2019, Sumaye alijiuzulu uanachama wa Chadema na kustaafu siasa, kwa kile aichodai chama hicho hakina demokrasia.

Februari mwaka huu, Sumaye alirejea CCM. Sasa mgumu alibaki Mahanga peke yake. Kisha naye, Mungu akamtwaa. Sasa, baada ya kifo cha Mahanga, ndio kitabu cha Lowassa ndani ya Chadema kimefungwa. Wote walimfuata, ama walirejea au walifikwa na mauti.