Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vipodozi sahihi kwa mama anayenyonyesha

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)kina mama wanapaswa kunyonyesha watoto wachanga maziwa pekee bila kuchanganya na kitu chochote ndani ya miezi sita.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO)kina mama wanapaswa kunyonyesha watoto wachanga maziwa pekee bila kuchanganya na kitu chochote ndani ya miezi sita.

Unyonyeshaji huo ni mchakato wa kutimiza lishe kamili ya mtoto ambaye hajaanza kupewa vyakula vya aina nyingine.

Wataalamu mbalimbali wa afya wanasema zipo faida nyingi za kunyonyesha mtoto, hasa kukidhi mahitaji ya ulaji kamili wa lishe inayoweza kusaidia ukuaji wake kimwili na kiakili, kumuweka katika uzito wa kawaida, kumuongezea kinga ya mwili ili asipate magonjwa kirahisi na kukuza uhusiano mzuri wa kihisia kati ya mama na mtoto.

Pamoja na umuhimu huo, yapo mambo kadhaa ambayo mama anayenyonyesha anapaswa kuyazingatia ili kuhakikisha kitendo hicho kinafanyika kwa usalama wa mtoto na kinakuwa na matokeo chanya.

Hata hivyo, Tovuti ya HelloMotherhood inaeleza kuwa, kuna makosa mama anayenyonyesha akiyafanya yanaleta matokeo mabaya kwa mtoto, ikiwamo kujipaka vipodozi vyenye kemikali.

Vipodozi hivyo ni pamoja na losheni na mafuta ya kupakaa mwilini yanayoweza kuwa na vikorombwezo hatari kwa mtoto kwa kuwa, anaponyonya hufyonza na kemikali alizopaka mama kwenye ngozi.

Kwa mujibu wa tovuti hiyo, kuna losheni na cream zinazotumiwa na wanawake kujichumbua zenye zebaki, hivyo mtoto anapokutana nazo afya na ukuaji wake unakuwa hatarini na wenye kusuasua.

Kemikali nyingine hatari ambayo hupatikana kwenye losheni na cream ni hydroquinone, hii hutumika zaidi kutengeneza vipodozi vyenye lengo la kung’arisha ngozi, hivyo mama anayenyonyesha akitumia kipodozi cha aina hiyo anamuweka mtoto hatarini.

Miongoni mwa vipodozi hatari vinavyotumiwa na baadhi ya kinamama vilivyopigwa marufuku na Serikali ni Exta Clear Cream, Fair&White zote, Claire Cream, Miki Beauty Cream, Clere Lemon Cream, Clare Extra Cream, Binti Jambo Cream, Body Clear Cream, na Jaribu Skin Lightening Lotion.

Mbali na vipodozi vya ngozi, vingine vinavyopaswa kuepukwa na mama anayenyonyesha ni matumizi ya manukato, kwa kuwa yanaweza kumuathiri mtoto kwa kiasi kikubwa.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, manukato mengi yanatengenezwa kwa kemikali ambazo si rafiki kwa ukuaji na afya ya mtoto, kwa kuwa uwezo wa ngozi yake kupokea hizo kemikali ni mkubwa na hana uwezo wa kukabiliana nazo, hivyo anaweza kupata maumivu ya kichwa, mzio, mafua au hata kubanwa kifua.


Kauli za wataalamu wa afya

“Kemikali hizi zinazuia ukuaji wa viungo vya mtoto, zinaathiri ukuaji wa ubongo na zinaweza kuathiri uwezo wa kufikiri wa mtoto. Si hayo tu, zinaathiri hata uwezo wa mtoto kujifunza kuongea hivyo anaweza kuchelewa kuzungumza,” anasema Daktari Linner Stephane.

“Haya yote ni madhara ya kumuweka mtoto karibu na zebaki na hydroquinone, tena anaipata kwa mama yake kupitia vipodozi anavyopaka.”

Hayo pia yanaelezwa na Dk Issack Maro, akisema mama anayenyonyesha anapaswa kujiweka mbali na vitu vyote vyenye kemikali, ikiwamo vipodozi na manukato kwa kuwa vina madhara makubwa kwa mtoto.

“Tunashauri mama anayenyonyesha kujiweka mbali na vitu hivi, kwanza inaweza kumsababishia mtoto allergy (mzio), pumu ya ngozi na athari nyingine za kiafya anazoweza kumuepusha mtoto, hii ipo hata kwenye vyakula vyenye kemikali, kuna uwezekano mtoto akazipata wakati akinyonya,” anasema Dk Maro.

Akizungumzia hilo, mkunga mstaafu, Salome Milinga anasema matumizi ya manukato ni kosa linalofanywa na wazazi wengi wa sasa wanaonyonyesha, kwa kile wanachodai ni kukata harufu ya maziwa bila kujua kuwa wanaathiri afya za watoto.

“Mtoto huanza kuvuta harufu tangu akiwa tumboni, anapozaliwa tayari anakuwa na uwezo mkubwa wa kunusa. Hapa ndiyo sababu anaweza kumtambua mama yake kwa harufu ile ya asili, sasa unapomuwekea manukato unamchanganya,” anasema Salome.

“Ni hatari mno kutumia manukato kama wewe ni mama wa mtoto mchanga, sio tu yatamchanganya kwenye uwezo wake wa kutambua, pia kuna madhara unaweza kumsababishia, ikiwamo mafua, mzio hata magonjwa ya ngozi.

“Haya ni matokeo ya wasichana wengi wanaopata watoto sasa kutozingatia suala zima la kliniki, binti anapata mtoto anamlea kihuni, baada ya miezi mitatu anambwaga anaendelea na kazi zake. Akitoka anajipulizia perfume (manukato) akirudi kabla hajajisafisha anamdaka mtoto, anaivuta ile harufu yote, unajiuliza kwa nini mtoto haponi mafua au kila siku anabanwa na kifua kumbe ni tatizo lako,” anasema mkunga huyo.

Salome anasema hakuna kitu muhimu ambacho mama anayenyonyesha anapaswa kuzingatia kama usafi, kuanzia wa mwili wake, mtoto na mazingira kwa jumla wanayokuwapo yeye na mtoto.

“Labda niwaambie hawa wasichana wanaozaa miaka hii, uzazi na malezi ya mtoto mchanga yanahitaji usafi wa hali ya juu, hutakiwi kumshika mtoto kumnyonyesha kama mwili wako mchafu au una jasho, lazima atakulamba mwilini, ukiwa umepaka vitu visivyofaa ndiyo hatari zaidi, magonjwa ya kuharisha yatakuwa hayakauki kwa mtoto,” anasema Salome.

“Ukiwa unalea angalia hata mitindo ya nywele, zamani wazazi wengi ilikuwa wanakata au kusuka nywele za kawaida, lakini siku hizi utakuta mama ananyonyesha amesuka manywele hadi yanamfikia mtoto usoni au nywele zinapukutika tu, hii ni hatari, utamsababishia matatizo bure mtoto,” anasema.


Wazazi wanafahamu hili?

Akizungumzia vipodozi vyenye kemikali na kubandika au kusuka nywele ndefu kupakwa na kinamama wanaonyonyesha, Jackline Michael anakiri kuwepo kwa changamoto hiyo hasa wenye shughuli zinazowalazimu wazazi kutoka na kuwaacha watoto nyumbani, wanaporudi akili inakuwa kwa mtoto kabla ya kujifanyia usafi.

“Hakuna anayependa asikike akinuka harufu ya maziwa na siku hizi wazazi hawataki kuachwa na fasheni, utakuta mtu ana mtoto wa miezi miwili au mitatu anamuacha anaendelea na shughuli zake, anapotoka ni lazima ajipodoe, anukie lakini sasa tukumbuke kujisafisha na kuondoa vipodozi vyote mwilini kabla ya kuwashika watoto,” anasema Jackline.

“Masuala haya yawe yanafundishwa kliniki au kwenye hospitali itasaidia kutukumbusha maana harakati za maisha zimekuwa nyingi watu tunakwenda mbio hadi tunasahau vitu vingine muhimu.”

Mama Farha, mkazi wa Ilala anasema huwa anatumia vipodozi anavyohisi vina madhara kwa kuwa ngozi yake imebadilika rangi kidogo lakini hakuwahi kumfikiria mtoto kipindi alichokuwa ananyonyesha.

“Unajua unavyotumia hivyo vipodozi lakini ujipake mwili mzima, vinginevyo utajikuta sehemu ya kifuani inakuwa tofauti na sehemu (rangi tofauti), lakini linapokuja suala la mtoto unapombeba anaweza kukulamba hata shingo au mkono, sio kunyonya tu,” anasema mama huyo mwenye mtoto wa miaka sita sasa.

“Nawashauri wanaopaka hivyo vipodozi, wakitaka kunyonyesha watoto, wajisafishe kwanza ili kumuepushia mtoto madhara.”