Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vyoo vya umma siyo hatari kama unavyodhani

Muktasari:

Goodluch Josephat anasema miongoni mwa sehemu ambazo hapati uhuru wa kujisaidia ni uwanja wa ndege: “Vile ambavyo niwewahi kufika, sijawahi kuona maji ya kujisafisha. Mara nyingi kuna kuwapo tishu pekee. Kila anayeingia analazimika kutumia hizo. Napata wasiwasi wa maambukizi kutokana na mazingira hayo.”

Ipo hofu miongoni mwa wananchi juu ya matumizi ya vyoo, hasa vya umma. Hofu ya kupata maambukizi ya magonjwa kutokana na muingiliano wa watu kwenye choo kimoja. Lakini watalaamu wanasema hakuna haja ya kuwa na mtazamo huo, vyoo hivi ni salama.

Goodluch Josephat anasema miongoni mwa sehemu ambazo hapati uhuru wa kujisaidia ni uwanja wa ndege: “Vile ambavyo niwewahi kufika, sijawahi kuona maji ya kujisafisha. Mara nyingi kuna kuwapo tishu pekee. Kila anayeingia analazimika kutumia hizo. Napata wasiwasi wa maambukizi kutokana na mazingira hayo.”

Vyoo vya umma vipo sehemu nyingi kwa lengo la kutoa huduma inayostahili kwa wateja, wasafiri, wagonjwa au watalii kulingana na bidhaa au huduma inayotolewa. Usafi ni moja ya vitu vinavyopewa kipaumbele ili mteja asijiulize anapotimiza haja zake.

Ritha Swai, mwanafunzi wa chuo kikuu jijini hapa anasema hana uhakika na usafi unaofanywa, hivyo mara zote anachukua tahadhari. “Natembea na tishu, nikihitaji kwenda maliwatoni nazitumia kwa tahadhari. Huwezi kujua nani katoka kutumia choo unachoingia, kila mtu na ustaarabu wake,” anasema.

Mitazamo ni mingi. Wengi wanamtazamo hasi juu ya vyoo vya umma, hasa vya kukaa. Ni tofauti na jinsi wengi wanavyovithamini vyoo vya nyumbani ambavyo usafi wake unasimamiwa na wao wenyewe.

“Ninao utaratibu maalumu wa kusafisha choo, kila mmoja anafahamu wajibu wake pindi anapomaliza kukitumia, muda wote vitendea kazi vipo kwa ajili hiyo. Choo kisafi kinavutia na kuhamasisha mtu kukitumia, vya umma havina ratiba inayoeleweka, unaweza ukakuta uchafu utakaokukera kwenye baadhi ya vyoo,” anasema Afra Ndunguru.

Mgunduzi wa vyoo vya kukaa, Thomas Crapper amewahi kueleza siri ya bidhaa yake kwamba ni kuongeza utulivu wakati wa kujisaidia na utambulisho wa ustaarabu na maendeleo.

Licha ya vyoo hivi kuonekana vya kisasa na kistaarabu kama Crapper anavyosema, bado baadhi ya watu wana hofu juu ya uwezekano wa kuambukizwa magonjwa ya ngozi hususan vinapokuwa vinatumiwa na watu wengi.

Wataalamu wa tiba wanaandika kwenye mtandao wa Asap Science juu ya kutokuwa na hofu kuhusu matumizi ya vyoo hivyo, kwa maelezo kwamba havina maambukizi yoyote ya magonjwa wala havihifadhi bakteria kwa muda mrefu kiasi cha kutishia maisha.

Wanaeleza kuwa kitu muhimu ni usafi utakaozingatia taratibu kila unapofanywa. Asap Science inafafanua kwamba, hatari ya kupata bakteria na maambuzi ya magonjwa ipo endapo mikono ya mtumiaji haitasafishwa vizuri baada ya kutoka chooni na kugusa chakula, macho au sehemu za mwili zilizo wazi ambazo ni rahisi kwa vijidudu kupenya.

“Ukweli ni kwamba sinki la choo ni safi kuliko vifaa vingine likitunzwa vizuri. Bakteria aina ya E.coli, hawana uwezo wa kuishi kwa muda mrefu kwenye sinki hilo,” inabainisha Asap Science na kuongeza: “Vile vile kinga ngozi ya binadamu haiwezi kuruhusu bacteria kupenya kwa urahisi kama haina jeraha au uwazi wowote utakaowezesha bacteria kuingia mwilini.”

Ili kupunguza gharama zisizo na ulazima na kujiweka salama zaidi, wanatahadharisha juu ya matumizi ya tishu kufunika sinki, kwamba zinaweza zikawa zimebeba bakteria wenye madhara. Wanasisitiza kujisaidia kwa uhuru na kufanya usafi wa mikono baada ya kutoka haja.

Wataalamu wa hapa nyumbani pia wana mtazamo kama huo. Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania, Dk Namala Mkopi anasema hakuna madhara yoyote ya kutumia choo cha kukaa kwa watu wengi kama usafi unaofanyika unazingatia taratibu za afya salama.

“Kama usafi unafanyika ipasavyo hakuna madhara yoyote kiafya. Choo cha umma ni sawa na kusalimia kwa kushikana mikono. Matendo yote yanahusisha ngozi. Watu wanagusana,” anasema Dk Mkopi.

Dk Mkopi anasema siyo magonjwa yote yanaambukizwa kirahisi na kwamba uimara wa kinga za mwili alizonazo mtu pamoja na ngozi yenyewe ni vitu muhimu kuzingatia, unapozungumzia maambukizo ya bakteria kwa mfumo wa mgusano. Anafafanua kuwa hilo linawezekana kama ngozi ina majeraha na kinga za mwili haziko imara, ila kinyume na hapo ni vigumu kwa mtumiaji kupata maambukizi kutoka chooni.

“Nadhani kinachofanywa na watu ni tahadhari ya kawaida inayotokana na kukosa imani na usafi unaokuwa umefanyika ndiyo maana majumbani kwao hawafanyi hivyo,” anasema Dk Mkopi.

Dk Prinus Saidia anasema kuna uwezekano wa maambukizo ya magonjwa kutokea endapo choo kitatumiwa na watu wengi lakini baadhi yao wakiwa wanamagonjwa ya ngozi tayari, ila hali hiyo inaepukika endapo kutakuwa na usafi thabiti.

“Kwa hali halisi vyoo hivi havipaswi kutumiwa na watu wengi, kwani mfumo wa mwili wa binadamu na choo hugusana hivyo unahitaji usafi wa hali ya juu kila baada ya matumizi choo kisafishwe kwa dawa tofauti na hapo maambukizi yatakuwepo, ” anasema Dk Saidia.

Ili kupunguza wasiwasi uliopo, Dk Saidia anapendekeza, kwa kuwa usafi katika vyoo vya umma, bado haujawa wa uhakika ni bora vikawa vya kuchuchumaa na vya kukaa vikabakia kwa ajili ya walemavu na watu wengine wenye mahitaji maalumu.

Mtaalamu wa ngozi wa Chuo Kikuu cha Sayansi Muhimbili (Muhas), Profesa Kasali Pallangyo aliwahi kuliambia gazeti hili kuwa matumizi ya vyoo hivi yanaweza kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa ya ngozi na ngono.

Aliyataja magonjwa yanayoweza kuambukizwa kupitia vyoo vya kukaa kuwa ni kaswende, harahara, mba, kisonono na upele. “Mtu mwenye magonjwa ya ngozi au ya ngono anaweza kuyaacha katika sinki anapolikalia, hivyo ni rahisi kwa mtu mwingine kuyachukua mara atakapolitumia wakati wa kujisaidia,” alikaririwa akisema Profesa Pallangyo.

Namna ya kusafisha choo

Wataalamu wanashauri kwamba, kwakuwa mara nyingi choo cha kukaa hutengenezwa kwa marumaru ambayo ni rahisi kusafishika unapaswa uwepo utaratibu wa kusafisha kila mtu anapotumia.

Ni vyema choo kikasafishwa kila siku, na angalau mara mbili kwa wiki ufanyike usafi mkubwa wa kusugua kila sehemu ya choo kwa sabuni na dawa maalumu za kusafishia.