Wajawazito wajifungulia kwenye mitumbwi
Waendesha mitumbwi wakiwasafirisha wanananchi kutoka Merela kwenda chita katika mto Kihansi, wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro
Muktasari:
- Usafiri wa mitumbwi kwenye mto Kihansi unahitaji nidhamu ya pekee, abiria hutakiwi kujitikisa mjamzito anapojifungua ghafla wanaume wanatakiwa kugeuza nyuso zao.
Morogoro.Ni safari yenye karaha iliyotumia takriban wiki nzima kutoka Morogoro hadi kijiji cha Mlimba, lengo ni kufuatilia ukweli kwamba wajawazito wengi hujifungulia kwenye mitumbwi wakati wakivuka mto Kihansi wakipelekwa katika zahanati ya kijiji cha Chita, tarafa ya Mngeta wilaya ya Kilombero kufuata huduma ya afya.
Kijiji cha Chita kiko umbali wa kilometa 110 kutoka makao makuu ya wilaya ya Kilombero yaliyopo Ifakara, mji uliojaa neema ya zao la mpunga na samaki wa kila aina kutoka mto Kilombero, ukiachilia neema nyingine iliyopo mkoa wa Morogoro. Licha ya umbali wa kilometa 110 kutoka Ifakara hadi Chita, pia itakulazimu kutembea kilomita 10 za ziada ili kufika katika kijiji cha Merela, ambapo wananchi wake husafiri kwa muda wa saa tatu kipindi cha masika kufuata huduma za afya, huku shida za kila aina zikiwakumba, wanafunzi wa sekondari, wajawazito, wagonjwa na wale wenye kutafuta mahitaji muhimu kijiji cha Chita.
Nikiwa na Diwani wa Kata ya Chita, Hassa Kidapa, tulianza safari kwenda Merela saa tano asubuhi, huku mvua ikinyesha, tukipita ndani ya maji yaliyojaa barabarani, sehemu zingine yakiwa na kina cha usawa wa kiuno, sehemu zingine magotini na kifundo cha mguu na kutembea umbali mfupi wenye eneo kavu ulipo mtumbwi kwa ajili ya safari ya kijijini Merela.
Mitumbwi inayotumika kusafirisha watu ni midogo, iliyotengenezwa maalumu kwa uvuvi na siyo kwa ajili ya kusafirisha abiria, hivyo kukulazimu kukaa bila kujitingisha wala kujigeuza kwakuwa mtingishiko wowote unasababisha mtumbwi kuyumba na hatari ya kuzama.
Celelin Ndopwele (45) yeye anajishughulisha zaidi na kilimo na Mvuvi katika bonde la Kihansi, anasema ana uzoefu wa miaka mingi wa kuvusha watu kwenye mto Kihansi na ameshuhudia wajawazito wakijifungua kwenye mitumbwi.
“Ni kweli wajawazito kujifungua katika mitumbwi na kinachofanyika hapo, kwanza baharia ni lazima utie nanga mtumbwi pembeni kwenye kina kidogo cha maji na wanaume kutoka katika mtumbwi ule na kwenda umbali wa mita 50 na kuwaacha akinamama wakimsaidia mwenzao kujifungua,”alisema Ndopwele.
Aliongeza kwa kusema kuwa kama kuna kina kirefu cha maji itawalazimu wanaume kugeuza nyuso zao kwa kuangalia macho kule unakotoka mtumbwi, ili kuepusha macho kuangalia kitendo cha mwanamke mjamzito kujifungua ama anasaidiwa kujifungua mtoto.
Alieleza kuwa kuna adha na kero zinazojitokeza katika safari za kusafirisha abiria katika bonde hilo kipindi cha masika, zikiwamo zile za kupambana na vitumbwi vya wanyama adui namba moja kiboko na mamba ambayo wamekuwa wakifanya vitimbwi mita chache katika maeneo yanayopita mitumbwi.
Kazi ya kusafirisha abiria hutozwa kwa viwango tofauti ikianzia Sh1,000, Sh1,500 hadi Sh2,000 tangu kwa kuanza kwa msimu wa masika wa Machi hadi Julai kila mwaka, viwango hivyo tozwa kulingana na umbali wa maji.
Kuna jumla ya mitumbwi 13 inayoegeshwa upande wa Chita na ule wa Merela inayofanya kazi kila siku kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa moja jioni, katika mazingira magumu ya kutembea na mwanga hafifu na kuambulia kipato cha Sh 10,000 hadi 20,000 kwa siku.
Ndopwele anasema kiwango hicho wanazotozwa abiria wao wakati mwingine wapo wanaowabeba bure na nauli pungufu na kujikuta siku nyingine wakiambaulia sh10,000 au pungufu ya hapo.
Akizungumzia Ndopwele, wanyama wakali wa majini kama mamba na viboko wamekuwa wakiibuka jirani na mitumbwi na kuzua hofu kwa wasafiri wanaotumia chombo hicho kusafiria na kumlazimu baharia kurudisha nyuma mtumbwi ili kupisha wanyama kufanya michezo yao ambayo kwa binadamu huwatia hofu ya kuvamiwa.
Mtendaji kijiji cha Merela
Tukiwa katika kijiji cha Merela kata ya Chita tarafa ya Mngeta wilaya ya Kilombero, Kaimu Ofisa Mtendaji, Abdom Undole anaeleza kwa ufupi historia ya kijiji hicho:
Kijiji cha Merela kina vitongoji vya Idunda, Kalihanya, Kitundu, Ipungahewa na Msita ikiwa na zaidi ya wakazi 7,960 na kaya zaidi ya 1,200 huduma muhimu zikitegemea kijiji cha Chita kama huduma za afya. Kuna zahanati imeanza ujenzi wake tangu 2010, boma likijengwa kwa nguvu ya wananchi huku Serikali ikitoa kiasi cha Sh30 milioni kwa ajili ya kumalizia. Undole anasema kijiji kina vitongoji vitano na kuna mpango wa vitongoji viwili kuwa vijiji kamili.
Akielezea maisha ya wakazi wa kijiji hicho ambao shughuli yao kuu ni uvuvi, kuwa changamoto kubwa ni shida ya usafiri kutoka Chita hadi Merela kutokana na ukosefu wa barabara ya uhakika zinazoweza kupitika wakati wote.
“Hatuna barabara ya uhakika wakati wa masika kwani usafiri wetu kwa asilimia 85 ni kusafiri katika maji na nyakati za kiangazi ndiyo tunapata fursa ya kutembea kwa magari na pikipiki, kwa kusafirisha wagonjwa na wananchi wenye kuhitaji mahitaji muhimu katika kijiji cha Chita ama kwenda Mlimba na Ifakara,” anasema Undole. Anaongeza kuwa wanaoathirika zaidi na shida hiyo ya usafiri ni akinamama wajawazito, wakiwemo wale wa jamii ya wafugaji ambao wengi wao hujifungulia njiani kwakuwa hawatambui kalenda za nyakati za kujifungua.
Undole anasema kutoka na shida hiyo pia kumekuwa na idadi kubwa ya vifo vya wagonjwa, na hasa nyakati za masika kwakuwa baadhi huzidiwa njiani wanapokuwa kwenye usafiri wa mitumbwi.
Kumekuwa na idadi kubwa ya vifo kwa wagonjwa wanaosafirishwa kwa kutumia mitumbwi, wakati wakipelekwa hospitali ya Ifakara, kituo cha afya Mlimba ama zahanati ya Chita.
Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2012-2013 pekee wastani wa wajawazito watano walijifungulia katika mitumbwi, wagonjwa watano wamefariki dunia na bidhaa za dukani zilitumbukia mto Kihansi. “Matukio yaliyojitokeza katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2013, kuna vifo vya watu watano wamepoteza maisha na wajawazito kwa idadi hiyo wakijifungulia katika mitumbwi, kutokana na adha ya usafiri nyakati za masika na mtoto kuporochoka mgongoni mwa mama yake na kutumbikia kwenye maji, lakini aliokolewa.” alisema Undole.
Ushuhuda wa Mganga kiongozi
Dustan Mkotte ambaye ni mganga kiongozi zahanati ya Chita, anasema kuna shida ya huduma ya afya kwa wananchi wa Chita na vitongoji vyake inayosababishwa na tatizo la usafiri.
Anasema kutokana na tatizo hilo wajawazito wengi hujifungulia njiani na kesi hizo hujitokeza kwa wastani wa kinamama watatu kwa mwezi. “Takwimu hizi ni kwa wale ambao wamejifungua wakati tayari wamevuka mto Kihansi, lakini wale wanaozalia njiani kabla ya kuvuka mto, wengi hugeuza na kurudi nyumbani, lakini hao huwa tunawagundua wakati wa utoaji wa chanjo,” anasema Mkotte.
Mkotte anasema kuna hatari ya wajawazito wengi kupoteza maisha kwa kujifungulia kwa wakunga, ambao hawana utalaamu wa ziada wa kutambua dalili hatari za mama mjamzito.
Historia ya kijiji cha Merela
Marthin Chogo (68) anasema mwaka 1971 reli ya Tazara ilijengwa na wananchi wa kando ya reli walifaidika na usafiri huo, lakini kukosekana miundombinu ya barabara ya uhakika kwa wakazi wa Merela kwenda Chita, kumewalazimu kutegemea zaidi usafiri wa mitumbwi nyakati za masika.
“Kupitisha mazao, wagonjwa, wajawazito kujifungulia njiani kama kwenye mitumbwi, wananchi kusafiri na bidhaa kutumbukia majini, hii kero inaweza kutoweka kwa Serikali kutengeneza barabara hilo litasaidia wananchi kuondokana na adhabu nyakati ya masika,” alisema Chogo.