Wasanii na kilio cha kupigwa fedha kisasa

Kwa zaidi ya miaka saba Harmonize hajapokea fedha yoyote ya uchapishaji na usambazaji wa muziki wake, huku zaidi ya Sh100 zikiwa zimepigwa kupitia wimbo wake ‘Kwangwaru’ aliyomshirikisha Diamond Platnumz.

Hayo ni madai yaliyotolewa na Harmonize mwenyewe Februari 21, 2023 ambapo alitupa lawama zake kwa kampuni ambayo ndio iliyokuwa inahusika na usambazaji wa kazi zake na kuwataka waeleze ni nani aliyepiga fedha zake!.

“Namiliki ‘master’ zote lakini sijui nani anakusanya fedha zangu, nataka kuwakumbusha kitu nipo hapa kwa ajili ya ‘future’ yangu, nahitaji maisha mazuri kufanya kazi kwa bidii. Masimango, manyanyaso, mateso na kudhalilishwa halafu kuna mtu anachukua fedha zangu,” alidai Harmonize.

Staa huyo wa Konde Music Worldwide alikwenda mbali zaidi na kusema ataacha muziki ili wanaofanya hivyo wafurahi na kusistiza hakuna Prodyuza ambaye anapokea fedha za uchapishaji na usambazaji.

Akilizungumzia hilo mtayarishaji wa muziki Bongo, Zest alisema ni jambo la aibu katika tasnia, na muziki unakatisha tamaa kutokana na dhuluma zinazoendelea.

‘’Watu wenye roho mbaya ukidai haki yako wanaona kama umeishiwa, miaka saba bila kupata malipo hili ni tatizo na aibu sana kwenye sanaa yetu, hata sisi watayarishaji tunadhulumiwa sana haki zetu’’ alisema Zest.

Kwa muda sasa madai na mamalamiko ya wasanii Bongo kwenda kwa kampuni za uchapishaji na usambazaji ambazo nyingi ni za nje yamekuwepo, Vanessa Mdee ni miongoni mwa waathirika wa jambo hilo. Vanessa ambaye aliachana na Bongofleva kwa madai ya kutomlipa kulingana na jitihada na uwekezaji wake, Agosti 2022 aliilamikia kampuni moja kutomlipa fedha zake licha kufanya jitihada kubwa kudai. “Jamani pesa ya muziki zinatafuta kwa shida kweli kweli na wasanii kuanzia kubuni hadi ifikapo kwa wananchi. Tafadhali nawaomba mnilipe pesa zangu kwa makubaliano tulionayo. Nimejaribu ‘the professional way’ na timu yangu sana imefikia hatua ya nyie kitojibu,” alieleza Vanessa.

Akizungumza na gazeti hili, Silvano Mazengo kutoka Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) alisema changamoto kubwa ni wasanii kutosajili kazi zao na kukosa elimu ya hakimiliki, licha ya kuwaita kuwapatia mwitikio ni mdogo sana. “Mara nyingi tunawapigia wasanii wengi njooni msajili nyimbo na mjue haki zenu lakini mtu anaanza kulalamika tena, ila mtu akijua ofisi ya Cosota inafanya kazi gani ni rahisi yeye kupata haki zake za msingi,” alisema.

Alisema suala la Harmonize Cosota wanaweza kulipatia ufumbuzi kama msanii huyo atakuwa tayari kushirikiana nao, huku akisisitiza kuwa hakimiliki ndio msingi wa ulinzi wa kazi ya msanii.

“Suala kama hilo Harmonize akifika ofisi hapa kila kitu kitaenda sawa na hicho anachokidai huko kitafuatiliwa na kila kitu kitakaa sawa” alisema na kuongeza. “Ila cha kwanza tutamwambie awe mwanachama wetu kama bado, na kila wimbo atakaotoa lazima usajiliwe na upewe hakimiliki, utakapotumika popote pale ana haki na anaweza kuja kulalamika na akapata haki zake,” amesema Mazengo kutoka Cosota. Utakumbuka mtayarishaji kutoka Bongo Records, P Funk Majani, Julai 2022 alidai Prodyuza mwenziye, S2kizzy alikosa fedha zake (publishing advance) Dola75,000, wastani wa Sh175.3 milioni kutoka kampuni moja ya nje baada ya nyaraka zinazomtambua kama mbunifu wa kazi kugushia na fedha hizo kuchukua watu wengine.


Wadau wawapa mbinu kuondoa kilio hiki

Akizungumzia kitu ambacho wanaohusika kuandaa wimbo kuanzia kutunga hadi unapotoka ili kila mmoja awe na haki anayostahili, mwanamuziki mkongwe John Kitime anasema kuwa, “ Wasanii wengi waimbaji na waandishi wa maneno, huku utayarishaji wa wimbo wenyewe ikiwamo vyombo wakimtegemea zaidi mtayarishaji.

“Lakini tangu awali si mwandishi, mwimbaji wala mtayarishaji wanaokumbuka kuingia mikataba itakayowalinda wimbo ukianza kuingiza fedha kupitia mitandaoni ambako wanapeleka ukachezwe ili walipwe,”anasema Kitime. Kitime anafafanua kuwa wanaofanya kazi kwenye lebo wanapaswa kuliangalia suala hilo kwenye mikataba. “Unakuta yupo chini ya lebo, ametunga wimbo, amelipiwa studio kwa maana ya kufanyiwa audio na video, lebo ikaupeleka wimbo kwenye mitandao ambako utasambazwa ili ulipiwe, hapo lazima mwenye haki atakuwa mwenye lebo. “Ili msanii na wengine walioshiriki wawe na haki wakiwamo watunzi, lazima tangu mwanzo kuwe na makubaliano ya nani anapata nini na yawasilishwe kwa wanaohusika kwa ajili ya kuweka sawa mchanganuo wa malipo. Tofauti na hapo wataendelea kulalamika kuibiwa na hakuna mahali watakwenda kushinda kesi ya namna hiyo, makubaliano ya kimaandishi kisheria ndiyo kila kitu,”anafafanua Kitime.

Anasema hata msanii anapotayarisha wimbo kisha akaupeleka kwa wakala ili ausambaze, lazima wakala atalipwa asilimia fulani, hakuna kazi ya bure.

Kwa upande wa mtayarishaji mkongwe wa muziki Joachim Kimario, maarufu Master J anasema msanii au mtunzi huwa ana haki ya msingi katika umiliki wa nyimbo kama amehusika katika utayarishaji wake.

“Kama wewe haujatunga mashairi, hujatengeneza mdundo wewe sio mtunzi, maana yake hauna haki ya nyimbo hiyo,’’ anasema. Master J anafafanua kuwa endapo msanii, hajahusika katika kimojawapo basi na yeye hana haki ya umiliki wa nyimbo hiyo, labda kama ataamua kumsainisha mkataba yule aliyemuandikia nyimbo ili apate umiliki wote.

Anasema katika tasnia ya muziki watu wamekuwa wakifanya kazi kiholela kiasi cha kushindwa kupata haki ya kazi zao.

“Kimsingi mtu yeyote aliyehusika katika utayarishaji wa muziki, awe mwimbaji, mtunzi wa mashairi, aliyetengeneza mdundo huwa ana haki ya msingi katika umiliki wa nyimbo kisheria kabisa, labda kama kuna mkataba upo kati yao,’’ anasema.

“Zipo sheria na taratibu ambazo zinawalinda na ni jambo la Serikali kukazia sheria hizo kupitia Cosota ili kila mtu apate haki yake na kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.

Hata sasa iwapo msanii atafuata utaratibu ulioainishwa kabla ya ngoma kutoka, yaani kuipeleka Basata ikakaguliwe maadili, Cosota ambako kimsingi wao wanajua mchanganuo wa nani anapata nini na ikitokea ulikopeleka kazi wanasumbua kukulipa wao watasimamia ulipwe. Lakini wengi hawafanyi hivyo.