ACT-Wazalendo ni moto wa mabua?

Chama cha ACT-Wazalendo kilizindua mwanzo mpya wa mikutano ya hadhara Februari 19, 2023. Hii ni baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutoa ruhusa ya shughuli za kisiasa.

ACT-Wazalendo walianzia Zakhem, Mbagala, Dar es Salaam. Walionesha ujio wenye matumaini makubwa kisiasa, baada ya kifungo cha miaka saba. Ratiba inaonesha kituo kijacho ni Nungwi, Zanzibar, Februari 26, 2023.

Umati mkubwa wa watu kwenye mkutano wa kisiasa ni kielelezo cha ushawishi. Uwezo wa kuitoa halaiki nyumbani kuja kuwasililiza ni ama mnajenga matarajio yao au mnavutia kuja kutazamwa na kusikilizwa.

Chama cha siasa kinapaswa kuvutia kwa namna kinavyojenga matumaini kwa wapigakura, sio mvuto wa mikutano yao kutazamwa peke yake. Ingawa, kuvutia watazamaji ni mtaji kuelekea kusimika matarajio chanya kwa watu.

Ni hivi; umeshawishi watu kuja kwenye mkutano, wamekuja kwa wingi. Baada ya hapo wanaondoka na nini? Sera nzuri na hoja zenye ufumbuzi kuhusu maisha yao au mlicheza mdundiko na kupiga porojo?

Bila shaka, kama ni mdundiko na porojo, wataondoka wakifurahia jinsi watu walivyosakata ngoma kwa vibwebwe pamoja na kumbukumbu za soga na vichekesho vya siasa. Ikiwa maisha yao yalizungumzwa na kuwagusa, wataweka akilini. Watakipenda chama.

Mkutano wa ACT-Wazalendo Mbagala, umekuwa na matokeo makubwa kwa chama hicho katika historia yake. Umati mkubwa wa watu na rangi ya zambarau ilivyoshamiri. Ni kuonesha kuwa ACT-Wazalendo wana watu.

Maandamano kwa miguu yakiongozwa na Kiongozi wa Chama, Zitto Kabwe pamoja na Makamu Mwenyekiti Zanzibar ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, kuanzia Mbagala Misheni hadi Zakhem, yalitengeneza msongamano mkubwa wa magari. Watu walikuwa wengi mno.

Uwanja wa mkutano wenyewe ulisheheni watu. Kwa Dar es Salaam, naweza kuthubutu kusema ule ndio mkutano wa kwanza wa ACT-Wazalendo uliokusanya watu wengi kwenye historia yake.

Swali linaweza kuwa moja tu; mkutano wa Mbagala kwa ACT-Wazalendo, ni kiashiria kuwa huo ndio mwanzo wa ukuaji mkubwa wa chama hicho au kilichotokea ni moto wa mabua? Muda utaleta majibu. Jaribio la kwanza litakuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024.


Upekee wa ACT

ACT-Wazalendo, baada ya tangazo la Rais Samia kutengua katazo la mikutano ya kisiasa, hawakukimbilia kuingia mtaani. Walifanya vikao na kuibuka na tarehe; Februari 19, Dar es Salaam.

Wapo walioshangaa kuona ACT-Wazalendo walichagua kujichelewesha wakati ruhusa ya mikutano imetolewa na ndio kilikuwa kilio cha kila chama. Jinsi walivyojipambanua kwa mikakati kuelekea Februari 19, ilitosha kuonesha umakini wao.

Februari 18, 2023, siku moja kabla ya mkutano wa Mbagala, chama hicho walikutana Serena Hotel, Ohio, Dar es Salaam, wakazindua “Brand Promise”, yaani thamani ambayo wanachama na wananchi kwa jumla wanapaswa kuitarajia kupitia chama hicho endapo kitashika dola.

Hiyo Brand Promise yao ikapambwa na kauli mbiu ya “Taifa la Wote, Masilahi ya Wote”. Kisha ungekatiza barabarani na kuona mabango ya mwaliko wa mkutano. Hapa ilionesha kwamba chama hicho kilijipanga na kujiandaa kupata matokeo yaliyodhihirika Mbagala.

Kabla ya mabango na uzinduzi wa Brand Promise, viongozi wa ACT-Wazalendo, wakiongozwa na Zitto, waliingia mtaani kuzungumza na wananchi. Zitto alionekana soko la Mbagala, akizungumza na wafanyabiashara kuhusu hali ya biashara na kupanda kwa bei za bidhaa.

Hicho kilichofanyika ndicho wanazuoni wa Sayansi ya Siasa huita “Community Politics” – “Siasa za Kijamii.” Yaani kuwaendea watu kwenye maeneo yao, kujadili changamoto zao na kushirikiana kuzitatua.

Asili ya Community Politics ni siasa za UK. Chama cha Liberal, ndicho kilianza kutembea na sera hizo, Greens waliiga. Liberal siku hizi wanaitwa Liberal Democrats, ni baada ya Liberal kuungana na Social Democratic, Machi 3, 1988.

Moja ya mifano ya matokeo makubwa ya Community Politics ni jimbo la Leeds Magharibi, London. Kiasili, jimbo hilo lilikuwa ngome ya Chama cha Labour. Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa UK 1983, Michael Meadowcroft wa Liberal, alijikita kufanya siasa za kijamii kwenye jimbo la Leeds Magharibi.

Meadowcroft, aliwafuata wananchi walipo na changamoto zao, kwenye mitaa yao na kujadiliana nao. Matokeo yake, Labour walipoteza jimbo, ingawa lilikuwa ngome yao. Meadowcroft alimshinda aliyekuwa mbunge maarufu, Joseph Dean.

Hoja hapa ni kuwa matumizi ya Siasa za Kijamii hulipa haraka. Wananchi hupenda kuona wanaheshimiwa. Hutamani kuwapa kura wale ambao wana uhakika kuwa wanazijua shida zao na wanafahamu ukweli wa maisha yao. ACT-Wazalendo walipita humo kuelekea Mbagala.

Haikuwa mara ya kwanza, imekuwa desturi ya ACT-Wazalendo kutuma viongozi wao kwa wananchi, sokoni, mitaani hadi vijiweni. Shabaha ni kupokea sauti za wananchi ili wanapotokeza kwa umma kuzungumza, hoja zao ziwe zinashabihiana na yale yaliyo kwenye vifua vya watu.

Kwa mantiki hiyo, eneo hilo la Siasa za Kijamii, ACT-Wazalendo wanafanya vizuri. Inawezekana matunda yake ndio hayo yaliyoonekana Mbagala, Februari 19. Kwa vile sasa hivi kuna uhuru wa kufanya siasa, matokeo yatajionesha mbele tuendeko.


Moto wa mabua?

Umati ambao ACT-Wazalendo waliupata Mbagala, imekuwa historia Dar es Salaam. Hata hivyo, kwa Zanzibar chama hicho kilishathibitisha msuli wake tangu Uchaguzi Mkuu 2020.

Chama hicho kilifunga mitaa ya Unguja kwa umati mkubwa wa watu, siku Maalim Seif Sharif Hamad, alipokwenda kuchukua fomu ya kuomba kuwa mgombea urais wa Zanzibar.

Hivyo basi, tangu ACT-Wazalendo walivyodhihirisha kukubalika kwao Zanzibar mwaka 2020, isingekuwa ajabu kwa chama hicho kupata umati mkubwa visiwani. Athari ya Seif ilikuwa kubwa mno. Imeshangaza Dar es Salaam.

Hapohapo, upo msemo kuwa Dar es Salaam haina kawaida ya kugomea mikutano. Kwamba watu wa Dar wakiitwa mikutanoni huitikia. Kwa maana hiyo, inawezekana ACT-Wazalendo wamefanikiwa Mbagala kwa sababu ya asili ya Dar es Salaam. Watu wake hupenda shughuli.

Changamoto yao kama chama ni kudhihirisha nguvu yao mikoa mingine. Waonekane Nyanda za Juu Kusini, watandaze zambarau Kaskazini. Kanda ya Ziwa hadi Kati, napo waonekane. Hivyo ndivyo itathibitisha kuwa moto wa Mbagala haukuwa mwepesi mithili ya ule wa mabua. Bali, moto wao ni mzito kama wa pumba, na Mbagala umeashiria mwanzo wa ukuaji mkubwa wa chama.