Miaka miwili ya ACT bila Maalim Seif

Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa gazeti la Mwananchi jijini Dar es Salaam jana kuhusu uzinduzi wa mkutano wa hadhara unaotarajiwa kufanyika kesho viwanja vya Mbagala-Zakheim. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Leo kuzindua dira yake mpya kuelekea uzinduzi mikutano ya hadhara

Dar es Salaam. Wakati chama cha ACT Wazalendo kikizindua dira yake mpya inayoitwa “Ahadi yetu kwa Watanzania,” leo, pia kinaadhimisha miaka miwili ya kifo cha mwenyekiti wake, Maalim Seif Sharif Hamad.

Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ugonjwa wa Uviko-19.

Mwenyekiti huyo anakumbukwa kama mwanasiasa aliyeleta mageuzi makubwa katika demokrasia ya vyama vingi nchini hasa upande wa Zanzibar, ambako alikuwa na ushawishi mkubwa uliosaidia kukiwezesha chama hicho kupata nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

“Tunamkumbuka sana mwenyekiti wetu,” alisema Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe aliyefanya mahojiano maalumu na Mwananchi jana.

Katika mahojiano hayo, Zitto alisema leo chama kinazindua dira mpya ikiwa imebaki siku moja kabla ya kuzindua mikutano yake ya hadhara itakayofanyika nchi nzima kwa awamu tofauti, huku wakilenga kuwafikia Watanzania wengi katika maeneo yao.

“Ahadi ya chama chetu kwa Watanzania itahusisha masuala yanayowagusa wananchi katika maisha yao ya kila siku pamoja na suluhisho la changamoto hizo katika kujenga jamii ya Watanzania yenye ustawi,” alisema Zitto.

Alisema ahadi hiyo wataitambulisha kesho kwa wananchi katika mkutano wa hadhara utakaozinduliwa kwenye uwanja wa Mbagala Zakheim, Dar es Salaam.

“Wageni wa ndani na nje ya nchi watahudhuria hafla ya uzinduzi wa ahadi zao na hadi kufikia jana tumepata uthibitisho wa wageni 341 watakaohudhuria hafla hiyo wakiwemo mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, viongozi wa vyama vya siasa, wakuu wa taasisi za kitaifa na kimataifa, viongozi wa kitaifa na kimataifa, marafiki kutoka nje ya Tanzania na Afrika.

“Baada ya uzinduzi wa “Ahadi yetu kwa Watanzania”  (leo), Jumapili  tutakuwa na mkutano mkubwa wa hadhara katika viwanja vya Mbagala Zakhiem ambako tutaitambulisha hiyo ahadi, baada ya hapo tutakwenda kwenye mikoa mbalimbali,” alisema kiongozi huyo.

Zitto aliongeza kuwa Februari 25, watafanya pia uzinduzi wa ahadi yao kwa Wazanzibari na watafanya mkutano wa hadhara eneo la Nungwi kule Zanzibar na wiki inayofuata watafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Tibirizi, Pemba.

Baada ya hapo, alisema wataendelea na mikutano ya hadhara Tanzania Bara kwa kuifikia mikoa ya Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Tabora na Kigoma.

“Watanzania watege masikio kwa ajili ya kusikia masuala tutakayoyaibua kesho (leo), wakati tunazindua ahadi yetu na keshokutwa (kesho) Jumapili wakati tunaitambulisha rasmi kwa wananchi wa Tanzania,” alisema Zitto. Kiongozi huyo wa chama alisema ACT Wazalendo ni chama kinachojishughulisha na masuala yanayowahusu wananchi na wamepata majawabu ya masuala hayo kwa maana ya mambo ambayo watafanya endapo watafanikuwa kukamata dola.

Alitoa mfano kwamba hivi sasa kuna mgogoro mkubwa wa maeneo ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo, ACT Wazalendo wana jawabu la suala hilo na si jawabu la kinadharia bali kihalisia.

Zitto alibainisha wanakwenda kuanza mikutano ya hadhara katika mikoa saba kwa awamu ya kwanza na hatua ya pili wataifikia mikoa mingine minane baada ya mapumziko ya kipindi cha mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

“Uendeshaji wa mikutano ya hadhara ni gharama, si jambo jepesi, inahitaji rasilimali fedha, rasilimali watu. Kwa hiyo tunaenda awamu kwa awamu, tutaanza awamu ya kwanza katika mikoa minane kuanzia Dar es Salaam Februari 19, tutamalizia Machi 18 Kigoma Ujiji.

“Hatuendi kwa Watanzania na malalamiko tu, tunakwenda na masuala ambayo ni changamoto zao na majawabu ambayo sisi tungeweza kuyafanya na kuwaambia Watanzania sisi tuko tayari kuendesha Serikali na tumejiandaa, tukichaguliwa leo tuko tayari,” alisema Zitto.