Je, Trump kuwashughulikia mahasimu wake kisiasa?
Muktasari:
- Kwa nyakati tofauti amekuwa akiwatuhumu akitaka washtakiwe mahakamani, huku baadhi akiwaita majina mabaya.
Dodoma. Kurejea kwa Donald Trump madarakani kunahofiwa kuwa mwanzo wa kuwashughulikia mahasimu wake kisiasa kutokana na kauli zake za kuwashutumu, ikiwamo kutaka washtakiwe na kufungwa jela.
Miongoni mwa mahasimu wake wa kisiasa ambao amekuwa akiwatolea kauli kali baada ya kushindwa uchaguzi mwaka 2020 ni Rais Joe Biden, Makamu wa Rais Kamala Harris, Rais mstaafu Barack Obama na Hillary Clinton.
Kwa mara ya kwanza Trump alishinda urais wa Marekani mwaka 2016 alipopambana na mgombea wa Democrat, Hillary, lakini uchaguzi wa mwaka 2020 alipochuana na Biden alishindwa akawa Rais wa muhula mmoja.
Trump ambaye hakukubali matokeo ya uchaguzi, aliendelea kuwashambulia kwa maneno viongozi wa kisiasa akiwaona ni watu wanaostahili kufungwa jela, sasa amerejea madarakani.
Rais Joe Biden
Trump amekuwa akimshambulia Biden kwa maneno makali, akimuita fisadi, mpotovu, na rais mbaya zaidi katika historia ya Marekani.
Juni mwaka jana, Trump alichapisha ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social akidai kiongozi huyo anafaa kukamatwa.
Trump alitaka Biden na familia yake wachunguzwe akiwaita ‘familia ya uhalifu’ huku akiahidi kuteua mwendesha mashitaka maalumu ili kumchunguza rais huyo na kutafuta haki dhidi ya mambo anayodai ni dhuluma.
Kamala Harris
Trump amekuwa na matamshi makali dhidi ya Makamu wa Rais, Kamala akidai anapaswa kushtakiwa.
Katika moja ya mikutano ya hadhara huko Erie, Pennsylvania, Trump alimlaumu Kamala kwa kile alichokiita uvamizi wa wahamiaji kupitia mpaka wa kusini, akidai ana matatizo ya kiakili akimtuhumu kwa kusababisha changamoto za mpaka.
“Sijui ni nini kibaya kwake, lakini kuna kitu kinakosekana,” alidai huku akiongeza kuwa: “Unajua nini, kila mtu anajua hilo.”
Trump anaamini ana haki ya kumshambulia Kamala kwa masuala binafsi kwa sababu anadai kuwa wapinzani wake wametumia mfumo usio wa haki kummaliza kisiasa.
Barack Obama
Uhasama ulianza wakati wa utawala wa Obama, Trump akidai mara kadhaa kuwa Rais huyo mstaafu hakuzaliwa Marekani, bali Kenya.
Mzozo huu ulifikia tamati pale Obama alipotoa cheti chake cha kuzaliwa ili kumaliza uvumi huo.
Mwaka 2019, Trump alimshutumu Obama kwa uhaini akidai alihusika katika njama ya kupeleleza kampeni yake ya urais ya mwaka 2016, madai yaliyosababisha uchunguzi wa muda mrefu kuhusu ushiriki wa Russia katika uchaguzi huo.
Mwaka huu 2024, Trump aliweka wazi kupitia Truth Social kwamba anataka mahakama ya kijeshi ya umma kwa Obama, akionyesha kuwa uhasama wake kwa Rais huyo mstaafu haujafifia.
Hillary Clinton
Mvutano kati ya Trump na Hillary uliongezeka wakati wa mchuano wa urais wa 2016.
Katika kampeni zake, Trump aliongoza umati wa wafuasi wake kuimba ‘mfungeni’ akirejea kashfa ya barua pepe ya Clinton alipokuwa waziri wa mambo ya nje.
Trump aliwahi kusema atateua timu maalumu ya uchunguzi kuchunguza kashfa hiyo, na alipoulizwa alisema kuwa Clinton anapaswa kuona aibu.
Mwaka huu 2024, Trump amependekeza tena kuwa Clinton anapaswa kufikishwa mahakamani, akimaanisha mvutano haujaisha.
Spika Nancy Pelosi
Trump amekuwa akimuita spika wa zamani wa Bunge, Nancy Pelosi, kwa majina makali kama vile kichaa, akidai anapaswa kushtakiwa mahakamani.
Mbali ya hao, mvutano mwingine mkali ni baina ya Trump na Mwanasheria Mkuu wa New York, Letitia James, ambaye aliwasilisha kesi ya madai dhidi ya biashara ya Trump, akimtuhumu kwa udanganyifu wa kifedha na ukiukaji wa sheria.
Trump amekosoa kesi hiyo, akidai ni shambulio la kisiasa dhidi yake.