Ruto na ‘pata madaraka tujue tabia zako halisi’

Rais wa Kenya, William Ruto.

Mwanafalsafa wa Ujerumani, Immanuel Kant aliwahi kusema mfanyie mwenzako kitu ambacho na wewe unapenda kufanyiwa. Waswahili wanasema ‘pata fedha tuijue tabia yako’ , pengine msemo huu kwa wanasiasa tunaweza kuubadilisha kidogo na kusema ‘ pata madaraka tujue tabia yako’.

Ni dhahiri kuwa Uchaguzi Mkuu wa Kenya wa 2022 ulikuwa na mvutano mkubwa wa kisiasa kiasi kwamba kumalizika bila machafuko ni jambo ambalo kila mtu alishukuru lakini misemo niliyoianisha hapo juu namlenga moja kwa moja aliyekuwa mgombea Urais wa umoja wa Kenya Kwanza, William Ruto.

Wakati wa kampeni na Mara baada ya kushinda kiti hicho, Agosti 15 pale ukumbi wa Bomas nje kidogo ya Jiji la Nairobi alitoa kauli kubwa mbili ambazo wadau wote wa siasa ulimwenguni wanaona Kama hazifuati na kiurahisi ni anautafuna ulimi wake mwenyewe.

Kwanza aligusia suala la kutolipiza kisasi kwa watu ambao walikuwa na itikadi tofauti na yeye wakati wa Uchaguzi akiwemo Rais wa awamu ya nne wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa anampigia chapuo Raila Odinga wa Azimio la Umoja.

“Kwa wale waliotukosea , nataka kuwaambia hakuna cha kuogopa, hatutalipiza kisasi, hatuna muda wa kuangalia nyuma,”

Kiongozi huyo wa awamu ya tano nchini Kenya anayejinasibu mpaka Sasa na kauli ya kutolipiza kisasi wachambuzi wa siasa wanaikosoa baada ya kuanza kuiandama familia ya Uhuru Kenyatta na kuwataka walipe Kodi bila kuangalia matabaka.

“Na mimi nimefurahi sana kwamba sasa Kenya yote tumeunganisha mawazo yetu na tumekubaliana hakuna mkubwa wala mdogo mbele ya sheria na sisi wote tutalipa ushuru kulingana na mapato yetu.”alisema.

Sheria ya kutolipa kodi kwa mali ya urithi ilianzishwa mwaka 1969. Baada ya kifo cha rais wa kwanza, Rais Jomo Kenyatta, Rais wa pili Daniel Moi aliongeza jina lake kwenye orodha hiyo Mwaka 1982, sheria hiyo ilibadilishwa na kujumuisha Wakenya wote waliorithi mali kutolipishwa kodi.

Kauli ya Ruto inakinzana na sheria ya Kodi huku mvutano ukiendelea kuwa mkali, hata hivyo mke wa Rais Jomo Kenyatta ambaye pia ni mama wa Rais wa awamu ya nne, Uhuru Kenyatta, tayari amejitokeza hadharani na kukubali kulipa kodi kwenye Mali hizo.

Kauli ya pili ambayo, Rais Ruto anajipinga mwenyewe kwa mdomo wake aliitoa siku hiyohiyo ya kutangazwa kuwa mshindi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika mahojiano maalumu na waandishi wa habari ambapo alisema Serikali yake haitaua upinzani kwa maridhiano na badala yake watauacha ukue ili uikosoe Serikali.

Kwa ambacho Ruto anakifanya tangu aingie madarakani ni dhahiri kwamba anatembea njia tofauti na kauli ya kuuhitaji upinzani kwasababu mpaka Sasa anaendelea kuchukua wabunge wa vyama vingine hasa vya umoja wa Azimio la Umoja na kuwaweka upande wake.

Kwa mantiki hii unajiuliza swali dogo tu, je kuchukua wawakilishi wenye mtazamo tofauti na Serikali hakudhoofishi upinzani? Je, nani ataikosoa Serikali kwa itikadi tofauti na mawazo mbadala?

Sekeseke la kuchukua wabunge wenye mrengo tofauti na Rais Ruto ulianza siku mbili tu baada ya kutangazwa na IEBC ambapo alichukua wabunge 10 wasiokuwa na vyama na kuhamia chama chake Cha UDA na umoja wa Kenya Kwanza.

Kama hiyo haitoshi, Februari 7 mwaka huu Ruto pamoja na makamu wake, Rigathi Gachagua walikutana na wabunge tisa wa chama Cha upinzani (ODM) ambao wanaunda umoja wa Azimio la Umoja huku walichokizungumza bado kikiwa hakijajulikana.

Hofu kubwa ikiwa ni huenda wabunge hao wakahamia UDA chama ambacho kinaongozwa na Rais Ruto. Japokuwa mmoja ya wabunge hao Felix Jalang’o wa Jimbo la Lang’ata alisema wameenda kuzungumzia masuala ya maendeleo na sio vingine.

Baada ya tukio hilo Azimio la Umoja kupitia kiongozi wake, Raila Odinga waliwaonya wabunge hao na kuwataka siku nyingine kuomba ruhusa kabla ya kwenda kuzungumza na Rais mambo ya maendeleo.

Tukio hilo pia linasemwa kuwa ni kinyume na kauli ya Ruto ya kuuhitaji upinzani ilihali anazunguka kwa nyuma na kuwaomba waunge mkono juhudi.

Wabunge wa upinzani waliokutana na Ruto na Gachagua walikuwa; Gideon Ochanda (Bondo), Elisha Odhiambo (Gem), Mark Nyamita (Uriri), Caroli Omondi (Suba South), Shakeel Shabir (Kisumu East, Independent) Felix Odiwuor alias Jalang’o (Lang’ata), Paul Abuor (Rongo), John Owino (Awendo) na Seneta wa Kisumu Tom Ojienda.

Geoffrey Mlwilo, mchambuzi na mfuatiliaji wa siasa za Kenya anasema kitu anachofanya Ruto sio kigeni kwa siasa za Afrika.

“Nchi nyingi za Afrika wanasiasa wake ndio wapo hivyo, akiwa kwenye kampeni anaongea kitu hiki lakini akiingia madarakani anakuwa na mawazo tofauti kabisa na awali, hasa katika kuogopa upinzani ndio maana wanalazimika muda mwingine Hadi kuwanunua wabunge wa upinzani,”anasema.

Shaban Jamal anasema wanasiasa wa Afrika hawaaminiki kwa kuwa hawana msimamo thabiti kwani anaweza kukataa leo lakini kesho akakubali jambo hilo hata kama ni baya ilimradi awe ameshawishiwa na kiongozi aliye madarakani.

Ruto aliibuka mshindi baada ya kumshinda Raila Odinga kwa kura milioni 7.1 sawa na asilimia 50.49 huku Odinga akimfuatia kwa kura milioni 6.9 sawa na asilimia 48.85.

Vilevile mgombea wa chama cha Roots Party George Wajackoyah alipata kura 69,969 huku mwenzake wa chama cha Agano, Waihiga Mwaure akipata kura 31,987.