ACT-Wazalendo: Tutafuta ushuru wa mazao

Muktasari:
- Kimesema endapo hakitafanikiwa kushika dola, kitawatumia madiwani na wabunge watakaopatikana ili kusukuma ajenda itakayowanufaisha wakulima wa mikoa mbalimbali wakiwemo wa Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Songea. Ili kuleta unafuu kwa wakulima wa kuuza mazao yao kwa ufanisi na kujikimu kimaisha, Chama cha ACT- Wazalendo, kimesema kitafuta ushuru wa mazao endapo kitashika madaraka katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata hivyo, endapo hakitafanikiwa kushika dola kitawatumia madiwani na wabunge watakaopatikana ili kusukuma ajenda itakayowanufaisha wakulima wa mikoa mbalimbali ikiwamo Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Msimamo huo umetolewa jana Jumanne Julai 8,2025 na Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe wakati akiwahutubia wananchi wa Namtumbo katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Samia mkoani Ruvuma.
Zitto aliyeambatana na viongozi wengine waandamizi wa ACT-Wazalendo, akiwemo naibu katibu mkuu wa chama hicho (bara) wapo mkoani Ruvuma katika ‘Operesheni Majimaji Linda Kura’ yenye lengo la kuhamasisha Watanzania kujitokeza kupiga kura na kuzilinda.
Katika maelezo yake, Zitto amesema tangu aanze ziara mkoani Ruvuma amekuwa akipokea kilio cha ushuru wa mazao kupitia vikao mbalimbali vya ndani huku wengine wakimfuata moja kwa moja kumuelezea changamoto hiyo.
" ACT-Wazalendo itakaposhika madaraka au tukifanikiwa kuwapeleka kina Bonifacia Mapunda (mtia nia ubunge wa Namtumbo) bungeni kazi watakayoifanya ni kuhakikisha tunafuta kabisa ushuru wa mazao.
"Ushuru wa mazao unapaswa kuwa sifuri, najua kuna watu watauliza sasa mkifuta wa halmashauri watapataje fedha? ACT-Wazalendo tuna timu ya wataalamu iliyofanya utafiti," amesema.
Jinsi halmashauri zitakavyopata fedha
Zitto amesema timu ya wataalamu wa chama hicho imefanya utafiti na kubaini kuwa ushuru wa mazao nchini unaokusanywa unaiingizia Sh136 bilioni ambayo ni sawa na asilimia nane ya mapato ya halmashauri.
Kiongozi huyo mstaafu wa ACT Wazalendo, amefafanua kuwa wizara ya fedha watakayoiunda wataweka utaratibu wa kuzilipa fidia halmashauri zote kutokana na kuondolewa kwa ushuru huo.
"Si tulikuwa na kodi ya kichwa hapa Tanzania mnakumbuka? Ilikuwa inaitwa kodi ya maendeleo na ilivyofutwa halmashauri si zilipata fidia. ACT-Wazalendo itafutilia mbali ushuru wa mazao kote.
" Zile halmashauri zinazotegemea ushuru wa mazao Hazina itawafidia, tunataka wakulima wabaki na fedha za kutosha kwenye mifuko ili kuendesha maisha yao, " amesema Zitto.
Mmoja wa wakazi Namtumbo, Hamisi Lukaya amesema wanaipokea ahadi ya ACT-Wazalendo kwa mikono miwili akisema ushuru wa mazao umekuwa kero kubwa kwa wakulima wa mkoa wa Ruvuma.
Katika hatua nyingine, Zitto amesema ACT-Wazalendo haitachoka kuipigia kelele changamoto ya tembo wanaokwenda kuharibu mashamba kwa kula mazao ya wakulima na kuwasababishia hasara.
" Nimeambiwa tembo anakula mazao yenu, lakini hakuna linalofanyika, sheria ya wanyama pori inazuia wanyama kuharibu maisha yenu. Lakini hakuna mtu asiyetaka uhifadhi, ila usihifadhi maisha yenu.”
"Lazima tuweke mazingira ambayo wananchi mlindwe, tunataka haya mambo tukayapigie kelele ili tukomeshe changamoto hii," amesema Zitto.

Naye, Mapunda ambaye ni naibu mwanasheria wa ACT- Wazalendo, amedai amekuwa akigombea ubunge wa Namtumbo tangu mwaka 2015 bila mafanikio, lakini cha kushangaza licha ya wagombea wa CCM kushinda bado changamoto zinazowakabili hazijatatuliwa.
" Wananchi Namtumbo ni kama wamedharauliwa vile, yale niliyoyasema mwaka 2020 kuhusu kero za jimbo hili hadi sasa hakuna kilichobadilika. Mwaka 2020 mlikuwa na malalamiko ya mashamba ya kulima, lakini hata hivi hawana na wale waliokuwa nayo wamenyang'anywa," amesema Mapunda.