Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Atoa wito wanachama kuongeza ushirikiano kuijenga CCM

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Salim Abri 'Asas' akiwa ameshikilia keki wakati wa maadhimisho ya miaka 49 ya Chama hicho mkoani Mbeya, pembeni ni viongozi wa Chama hicho mkoani humo walioshiriki tukio hilo.

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi, CCM mkoani Mbeya imeadhimisha miaka 49 ya kuzaliwa kwake, huku viongozi wa chama hicho wakitaka waliochaguliwa kufanya kazi na kipimo chao kitakuwa miaka mitano ijayo.

Mbeya. 'Uchaguzi umeisha sasa ni kazi'. Ni kauli ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa (MCC), Salim Abri 'Asas' wakati akizungumza na wananchi mkoani Mbeya kwenye maadhimisho ya miaka 49 ya chama hicho.

Akizungumza leo Jumatano Februari 4, 2026 Asas amesema kwa sasa uchaguzi umeisha, wabunge na madiwani wanajulikana hivyo wanaonuna hawatafanya mabadiliko yoyote badala yake kilichobaki ni kazi.

Amesema jukumu la viongozi wa CCM ni kuishauri Serikali kuhakikisha waliochaguliwa wanafanya kazi na kipimo chao kitakuwa cha miaka mitano ijayo kubaini walichofanya.

"Tunachohitaji ni kuona wananchi wanapata maendeleo na jukumu letu viongozi wa CCM ni kuishauri Serikali, tumeona kazi alizoanza kufanya Mwenyekiti wetu wa Taifa na tuendelee kumuunga mkono," amesema Asas.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema Serikali imefanya mambo mengi ya maendeleo kwa wananchi, ikiwamo barabara ya njia nne iliyoanza kujengwa kwa kiwango cha lami na mradi wa maji Mto Kiwira.

"Kuna miradi mingine ya soko pale Matola stendi ya mabasi, haitoshi upande wa afya Serikali imejitajidi chini ya Rais Samia, Mbeya ameifanyia mengi na tutaendelea kumuunga mkono," amesema Itunda.

Akitoa salamu za Chama, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mkoa wa Mbeya (MNEC), Ndele Mwaselela amesema kauli yao ni maendeleo na amani akieleza kuwa ndio ilikuwa falsafa ya waasisi wa chama hicho.

Amesema katika kuadhimisha miaka hiyo ya chama, hawatakubali kudhihakiwa au kudhalilishwa kwa Mwenyekiti wao Taifa na yeyote atakayemtikisa hawatanyamaza.

"Sisi Mbeya hatutakubali kutikiswa kwa Mwenyekiti wetu, yeyote atakayeonesha kumkwamisha katika kazi, kumdharau au kumdhalilisha hatutamfumbia macho," amesema Mwaselela.

Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya mjini, Patrick Mwalunenge amesema Rais Samia ameanza utekelezaji wa ahadi ambapo upande wa ajira, wapo watumishi wameanza kufika vituoni.

Kuhusu mpango wa bima ya afya kwa wote, amesema tayari utekelezaji umeanza ambapo wananchi wakiwamo wazee wataanza kupata huduma bila changamoto na suala la mikopo amewaomba vikundi kujisajili ili kunufaika na fursa hiyo.

"Tunampongeza kwa utekelezaji huu na kuendelea kuiongoza nchi kwa maendeleo, CCM Mbeya tuko imara, niombe tusiweke mgawanyiko kichama bali tuwe sehemu ya kuunganisha wananchi, Serikali na chama," amesema Mwalunenge.

Awali Katibu wa CCM wilaya ya Mbeya mjini, Mohamed Mavallah amesema wanapoadhimisha miaka 49 ya chama hicho, wanampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kudumisha umoja na mshikamano.

"Hakuna kitu cha thamani na bora kama afya na amani, katika hili tunamshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wetu Taifa, kudumisha amani, upendo na utulivu katika nchi," amesema Mavalah.