Prime
CCM, ACT-Wazalendo bado kwafukuta
Muktasari:
- Pande hizo mbili zimeanza kushutumiana kutokana na makubaliano ya tamko la pamoja CCM ikidai ACT-Wazalendo inatoa siri huku ACT- Wazalendo ikisisitiza kuwa lazima kila kitu kiwe wazi ili wananchi wajue.
Unguja. Wakati ACT-Wazalendo ikiendelea kuwafafanulia wanachama wake kuhusu tamko la pamoja walilolisaini, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeonya kuwa hatua hiyo ni kuvujisha siri za mazungumzo na kwenda kinyume na makubaliano yaliyowekwa, jambo linaloweza kuhatarisha mazungumzo yanayoendelea kati ya vyama hivyo viwili.
Mvutano huo umeibuka siku chache baada ya vyama hivyo kusaini tamko la pamoja Julai 9, 2026, katika Ikulu ya Zanzibar.
Tamko hilo liliorodhesha hoja saba zitakazojadiliwa kwa pamoja, kabla ya kuundwa kwa kamati ya pamoja na tume itakayosimamia utekelezaji wa maridhiano hayo.
Julai 12, 2026, Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, alipokuwa akizungumza na viongozi wa majimbo na mikoa saba ya chama hicho, aliwaeleza kuwa kuna hoja ambazo hazikuwekwa wazi kwa umma wakati wa kutolewa kwa tamko hilo la pamoja.
Katika hoja saba zilizotangazwa Ikulu, Othman alifafanua hoja ya tano, ambayo ina vipengele vidogo 10, akieleza kuwa lengo ni kuwafahamisha wanachama na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala yaliyokubaliwa na yale yatakayojadiliwa katika mazungumzo yanayoendelea.
Vipengele hivyo ni pamoja na mageuzi ya mfumo wa utoaji haki, mageuzi utumishi wa umma, mageuzi katika Serikali za mitaa ambayo wanataka msimamizi mkuu awe diwani kama ambavyo Katiba inasema badala ya masheha.
“Tunataka vitambulisho vya Mzanzibari na sio Mzanzibari Mkaazi, kuna maeneo mahsusi katika kura ya mapema na Daftari la Mpigakura, kuwepo wa tume ya maridhiano, kamati ya ushauriano wakati wa uchaguzi, vyombo vya habari vya umma, vyombo vya ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi na muundo wa SUK,” amebainisha Othman.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 14, 2026, Katibu wa Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis amesema miiko na usiri wa ajenda za vikao unapaswa kuheshimiwa na iwapo wakienda kinyume wanaweza kuharibu mchakato mzima.
“Kilichosainiwa pale ni tamko la pamoja. Na ndani ya tamko kulikuwako na vipengele vingine, tamko likasema kutakuwa na ajenda ambazo zitakwenda kujadiliwa, sasa hizo ajenda zikasema kutaundwa kamati na hiyo kamati ndio itakwenda kujadili hizo ajenda na ndio itakuwa inatoa taarifa,” amesema Mbeto.
Mbeto amesema makubaliano ya pande zote mbili ni kwamba kila kitakachokuwa kinajadiliwa au kinatakiwa kutolewa hadharani lazima kitolewe kwa pamoja.
“Sasa leo hata kabla ya kamati kuundwa zinaanza kutolewa ajenda nje, kamati ndio itakuwa inasimamia masuala haya na kueleza ajenda hizo na sio kama inavyofanyika hivi sasa,” amesema Mbeto.
Mbeto amesema katika majadiliano hayo, yapo mambo yanayoweza kupita kama yalivyo lakini mengine yanaweza yasipite, hivyo wanatakiwa kutumia busara kuhakikisha siri za vikao zinalindwa.
Amesema jambo hilo linaashiria kama chama hicho kinaanza kutafuta huruma kwa wananchi, lakini kikiwa na nia ya kutaka kuvuruga mazungumzo hayo kwa kuwa, wanaaminisha watu mambo ambayo bado yapo kwenye majadiliano.
Akizungumza kumjibu Mbeto leo Jumanne Julai 14, 2026 katika kikao cha ndani na wanachama wa ACT- Wazalendo wa Jimbo la Konde na Micheweni Pemba, Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa bila kumtaja jina, amehoji kama alishiriki mazungumzo hayo.
“Wewe haya mazungumzo ulishiriki? Kama hukushiriki, hukuwamo, hiyo miiko, kanuni na maadili kakwambia nani? amehoji Jussa.
Jussa amesema masuala yanayohusu nchi na wananchi, hawawezi kuyaficha kwa sababu yanagusa umma huku akihoji yakifichwa nani ataambiwa?
“Sisi hatukuunganisha vyama. Wao wana chama chao na sisi tuna chama chetu, hawawezi kutupangia tufuate wanavyotaka wao,” amesema Jussa.
Naye, Othman amesema chama hicho hakina wasiwasi kwa sababu wanachokitafuta au kukipigania kina heri kwa Wazanzibari.
Wadau wafafanua
Umoja wa vyama 12 vya siasa kisiwani Zanzibar, licha ya kupongeza hatua ya makubaliano ya tamko la pamoja, vimewasihi viongozi wa vyama hivyo na wananchi kujiepusha na kauli za chuki, uchochezi na mengine yanayoweza kuharibu mustakabali huo.
Umoja wa vyama 12 vya siasa Zanzibar unaundwa na Chama cha Demokrasia Makini (Makini), Sauti ya Umma (Sau), Chama cha Kijamii (CCK), United People's Democratic Party (UPDP) na Alliance for Democratic Alliance-Tanzania Democratic Alliance (Ada-Tadea).
Vingine ni Democratic Party (DP), Tanzania Labour Party (TLP), NCCR-Mageuzi, United Democratic Party (UDP), National Reconstruction Alliance (NRA), National League for Democracy (NLD) na Union for Multiparty Democracy (UMD).
Katibu wa umoja huo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Makini, Ameir Hassan Ameir amesema vyama hivyo vinapaswa kutambua Zanzibar sio mali yao, bali ni kwa ajili ya wote, hivyo kinachofanyika lazima wazingatie masilahi ya nchi badala ya maslahi ya vyama.
“Tunatoa wito kwamba tamko hili halibaki kuwa maandishi pekee, bali litekelezwe kwa vitendo, kwa uaminifu na kwa uwazi na nia njema ya kujenga bila kuendeleza malumbano,” amesema.
Kuhusu madai ya kuvujisha siri, amesema iwapo kuna makubaliano ambayo yamefikia ni vema yakalindwa na wao wapo tayari kushiriki pale watakaposhirikishwa kwa misingi ya utawala bora.
Mkurugenzi wa Matukio na Siasa wa Chama cha Wananchi (Cuf), Ali Makame Issa amesema maridhiano hayo ni mazuri lakini wanapaswa kuzingatia misingi ya waliyokubaliana.
Hata hivyo, ameshauri badala ya kuendelea kuvutana licha ya nia njema hiyo, ni vyema ACT-Wazalendo wakaingia ndani ya Serikali ili wakatekeleze matakwa hayo wakiwa ndani ya Serikali jambo litakalojenga uaminifu zaidi.
Mdau wa siasa Zanzibar, Khamis Hassan Khamis amesema haoni sababu ya vyama hivyo kuendelea kuvutana jambo linaloweza kuashiria kuna masilahi binafsi.
“Ile sio mali ya vyama bali ni mali ya wananchi na Zanzibar, kwa hiyo hakuna sababu ya kuvutana au kutengeneza usiri mkubwa, hata hivyo kama wamekubaliana, yale yaliyomo yasisemwe ni vyema kila upande ukazingatia wananchi wanachotaka ni umoja na maridhiano ya kweli,” amesema.
Historia ya mwafaka Z’bar
Zanzibar imekuwa na takribani miafaka mikubwa mitano tangu mwaka 1995. Kila mmoja ulifanyika kati ya Rais wa Zanzibar na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani.
Mwafaka wa kwanza ulikuwa mwaka 2001 kati ya Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad, wakati huo akiwa Katibu Mkuu CUF, baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2000 na Umoja wa Mataifa ulisimamia mazungumzo hayo.
Mwafaka wa pili ulikuwa mwaka 2010, nao ulihusisha Rais Amani Karume na Maalim Seif akiwa CUF na matokeo yake waliunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Mazungumzo ya mwaka 2016 yalihusiaha Dk Ali Mohamed Shein na Maalim Seif baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2015 kufutwa na ZEC.
Mazungumzo baada ya mwaka 2020 yalihusisha Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na Maalim Seif wakati huo akiwa kiongozi wa ACT- Wazalendo na mazungumzo ya sasa 2025/26 yakihusisha Rais Mwinyi na Othman, Mwenyekiti wa ACT -Wazalendo.