CCM Mbeya yaapa kupambana na wanaowabeza viongozi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 49 ya Chama hicho iliyofanyika jijini Mbeya
Muktasari:
- Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mkoani humo (Mnec), Ndele Mwaselela amesema atakuwa tayari kutoka hadharani kubainisha maendeleo aliyofanya Rais Samia.
Mbeya. Wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kikisherekea miaka 49 tangu kuanzishwa kwake, wanachama wa chama hicho mkoani Mbeya wamesema hawatakubali kubezwa kwa viongozi wake akiwamo mwenyekiti wao, Rais Samia Suluhu Hassan.
Wanachama hao wamesema watakuwa tayari kubishana kwa hoja na wanaobeza utendaji wa chama hicho na kuwasilisha kazi zilizofanywa na Rais Samia na kusisitiza kuwa CCM ndiyo kinara wa kupinga ufisadi na ubadhilifu na yeyote anayebainika hatua za kisheria huchukuliwa.
Akizungumza leo Februari Mosi, 2026 katika sherehe za chama hicho Wilaya ya Mbeya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mkoani humo (Mnec), Ndele Mwaselela amesema atakuwa tayari kutoka hadharani kubainisha maendeleo aliyofanya Rais Samia.
Amesema Rais Samia amekuwa mbele kupambana na ufisadi, kukemea vitendo vya rushwa, upotevu wa mali za umma na kudhulumiwa haki za wananchi na kwamba wanaobeza kazi hizo CCM haitakuwa tayari kuwanyamazia.
“Tuendelee kumuunga mkono Rais Samia ili aendelee kuwa dira kwa wananchi, madiwani na wenyeviti serikali za mitaa tutekeleze kwa vitendo kuwasikiliza na kutatua kero za wananchi,” amesema Mwaselela.
Viongozi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Mjini, wakiwa katika sherehe za kuadhimisha miaka 49 ya Chama hicho.
Ameongeza kuwa chama kuanzia ngazi za shina hadi mkoa, hawatakubali kubezwa kwa viongozi wao, akieleza kuwa uchonganishi wowote wa propaganda kwa CCM na wananchi wake hawatatupa nafasi yoyote.
Mnec huyo amewataka viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi za matawi kutoka hadharani kujibu kwa hoja kazi zinazofanywa na CCM, akibainisha kuwa maendeleo yanayofanywa hayana uchama, ukabila wala itikadi za vyama.
“Ni wajibu wetu kuwatetea viongozi wetu, anayembeza mwenyekiti wetu anakibeza chama kwa ujumla, binafsi nitakuwa mbele kutoka hadharani kumlinda na kutangaza kazi nzuri anazofanya,” amesema Mnec huyo.
Kwa upande wake, Erick Kanuti ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya chama hicho, Wilaya ya Mbeya, amesema katika miaka 49 wanajivunia uongozi bora wenye amani tangu kuwapo chama hicho.
“Hatuna ukabila, udini na tumeweza kuishi bila itikadi zozote, lakini changamoto kubwa ni nidhamu kwenye uongozi, baadhi ya wanasiasa hawana heshima kwa mamlaka, kila mtu amekuwa kama kiongozi,” amesema Kanuti.
Naye Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Iganzo, Joseph Cherehani amesema kiongozi ni taasisi na CCM imekuwa sehemu ya kuandaa viongozi kuanzia ngazi ya chini kwa misingi ya maadili na utawala bora.
“Tunajivunia, pia, kuwa madarakani tangu kuanza chama chetu, kila anayepita anaacha alama yake ya maendeleo na ndiyo maana kila uchaguzi wanatuchagua wananchi kuendelea kushika dola,” amesema Cherehani.