Chadema: Hatutalipa kisasi

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amefichua siri ya kaulimbiu ya ‘No Fear, no hate’ akisema inalenga kujenga Taifa lenye furaha, demokrasia, uhuru, utangamano, ustawi na maendeleo ya watu bila kujali tofauti yoyote.

Mwanza. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amefichua siri ya kaulimbiu ya ‘No Fear, no hate’ akisema inalenga kujenga Taifa lenye furaha, demokrasia, uhuru, utangamano, ustawi na maendeleo ya watu bila kujali tofauti yoyote.

Akihutubia katika uzinduzi wa mikutano ya hadhara viwanja vya Furahisha jijini Mwanza juzi, Mbowe alituma ujumbe kwa viongozi, makada na wanachama wa vyama vyote vya siasa, kikiwemo chama tawala, kuwa Taifa haliwezi kuongozwa kwa misingi ya visasi na kugawa watu kwa sababu ya tofauti zao kiitikadi.

Huku akifichua matamanio yake ya kustaafu siasa akiacha Tanzania ikiwa Taifa lenye umoja na mshikamano, Mbowe alisema:

“Hatuwezi kugawanya Taifa vipande halafu tutegemee ustawi wa pamoja. Nayasema haya bila kujali iwapo nawafurahisha wana Chadema, CCM au mtu yoyote.”

Alisema nia ya umoja, ushirikiano na ustawi wa Taifa ndio ilimfanya azibe masikio asisikie kauli za baadhi ya watu, wakiwemo viongozi na makada ndani na nje ya Chadema waliomtuhumu kulambishwa asali alipoamua kutafuta na kushiriki vikao vya maridhiano.

Alitumia mkutano huo wa kwanza wa hadhara kuwashukuru na kuwapongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdullahman Kinana kwa kusimamia maridhiano  ya kisiasa kati ya CCM na vyama vya upinzani, licha ya upinzani na mpasuko uliojionyesha wazi kati ya wanasiasa wa pande zote.

“Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni, bila kificho nasimama mbele ya jamii ya Mwanza na nchi kumshukuru Rais Samia Hassan kwa namna ambavyo amekuwa mvumilivu nikimshawishi kuwa nchi inahitaji maridhiano,” alisema.

Aliongeza: “Nasimama mbele ya jamii ya Mwanza na dunia kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo alikuwa mvumilivu, kwenye vikao vingi nikimshawishi atambue uwepo wa vyama vingi na akakubali; Madam President alisimama kuiunga mkono hoja  yetu Chadema halafu nakutana na (baadhi) wana Chadema wanamuona alikosea; this is madness (huu ni uendawazimu),”

Mwenyekiti huyo aliyetumia saa moja na dakika 10 kuongea akianza saa 11:03 jioni hadi saa 12:13 alisisitiza chama hicho kitaendelea kusimamia misingi yake, huku akiahidi chama hicho kitaendelea kuikosoa Serikali pale kinapoona mambo hayaendi yanavyotakiwa.

“Chochote tulichoafikiana na CCM kuijenga Tanzania yenye maridhiano hakujamaanisha kuwa chama kimoja tutaendelea kuwa chama kikuu cha upinzani hadi ambapo tutakuwa chama tawala katika nchi yetu. Misingi ambayo tumeizungumza,” alisema.

Alisema ukweli kwamba siasa haistahili kuwa ya kutukanana na kudhalilishana, wala kuondoa haki na wajibu wa vyama vya upinzani kuwakosoa na kuwaambia ukweli viongozi wa Serikali na chama kilichoko madarakani.

“Naomba tusamehe ya nyuma twende mbele lakini nawaambia wana Chadema jambo la kudaiwa kulamba asali liliniumiza siyo mimi tu hata, watoto wangu na mke wangu, kwa sababu wanajua nimepoteza fedha kiasi gani kutokana na harakati zangu za kisiasa, halafu anatokea mtu anasema nimekula asali,” alisema.

Mkutano wa juzi ni wa kwanza kuhudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa ndani na nje ya Mwanza na jana alihutubia tena mjini Musoma, Mkoa wa Mara ikiwa ni kuitikia ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara ambayo Rais Samia Suluhu Hassan aliitangaza Januari 3, 2023.


Chaguzi zijazo

Mbowe alitumia mkutano huo kusisitiza msimamo wa Chadema kuwa chaguzi zijazo, ikiwemo ule wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa 2025 zinapaswa kufanyika chini ya Katiba Mpya na tume huru ya uchaguzi.

“Lazima turidhiane Katiba Bora ya nchi yetu, tume huru ya uchaguzi. Tusirudi tena katika chaguzi za kihuni za watu wanaoiba uchaguzi,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Yeyote atakayehujumu uchaguzi lazima awajibishwe, tutakwenda kwenye uchaguzi Mkuu na Serikali za Mitaa pale ambapo sheria zitasimama kwa wenye haki na walioshinda, ili kwa pamoja tujenge taifa linalotengeneza kesho iliyo bora”.

Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, alisema anafarijika kuona vikao vya mwafaka kati ya Chadema na CCM vimezaa matunda, licha ya awali kubezwa na baadhi ya wanasiasa wakiwemo wa upinzani na CCM pia.

Alisema waliostahili kuonyesha upinzani dhidi ya mwafaka wa kisiasa unaoweka uwanja sawa na haki kwa vyama vyote, walipaswa kuwa wana- CCM ambao mwafaka huo umewaondolea haki ya pekee ya kufanya siasa waliyoifaidi kwa takribani miaka saba tangu mikutano ya kisiasa ilipozuiwa kinyume cha sheria mwaka 2016.

“Nyinyi (wana -Chadema) badala ya kunipongeza mnakuja na mawazo ya kiharamia eti Mbowe kalamba asali, hataki katiba mpya, hataki tume huru,” alisema akionyesha hisia ya kuguswa na kuchukizwa na tuhuma hizo.


Siri majadiliano ya mwafaka

Mwenyekiti huyo aliendeleza msimamo wa kutoweka wazi ajenda na majadiliano kati ya Chadema na CCM, akifichua kuwa usiri huo ni kati ya makubaliano na misingi iliyokubalika kati ya pande hizo mbili kabla, wakati na baada ya majadiliano.

Alisema ataendelea kuonyesha na kueleza hisia zake na za wana- Chadema kuhusu madhila na maumivu ya muda mrefu waliyopitia huku akiendelea kutambua, kuheshimu na kuthamini ustahimilivu na nia njema ya Rais Samia na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Abdulrahman Kinana katika kupigania misingi ya kujenga nchi yenye umoja na mshikamano licha ya upinzani kutoka chama chao.

“Tulipoamua kuingia kwenye majadiliano ya mwafaka, sikuangalia hisia zangu, bali mahitaji na maslahi ya chama changu; ndiyo maana nilienda Ikulu kumuona Rais japo wengi walilalamika wakiwemo (baadhi ya) viongozi waandamizi wa chama changu,” alifichua Mbowe.

Huku akiapa kutotumia fursa ya mikutano ya hadhara na majukwa ya kisiasa kutoa kauli zisizo za staha kwa Rais Samia, kiongozi huyo wa upinzani alisisitiza msimamo wa yeye na makada wengine wa Chadema kuendelea kumkosoa na kumshauri Mkuu huyo wa nchi huku wakitoa maoni na njia mbadala wa kutatua matatizo ya wananchi.


Hali ilivyokuwa mtaani

Juzi, mji ulizizima! Ndivyo baadhi ya wakazi wa jiji la Mwanza walivyosikika wakisema jana wakati msafara wa viongozi, makada na wanachama wa Chadema walipokuwa wanapita barabara ya Kenyatta kwenda viwanja vya Furahisha kulikofanyika mkutano huo.

Mkutano huo ulikuwa pia ni sehemu ya kumbukizi ya miaka 30 tangu chama hicho kikuu cha upinzani kisajiliwe rasmi katika orodha ya vyama vya siasa nchini mwaka 1993.

Pia ulikuwa wa kwanza baada ya kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara ya kisiasa uliowekwa mwaka 2016 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.

Kabla ya mkutano huo uliohutubiwa na viongozi mbalimbali Jiji la Mwanza na vitongoji vyake kulikuwa na hamasa na shamrashamra za aina yake kutoka kwa wanachama na makada wa chama hicho wakionyesha furaha ya kurejea kwa mikutano ya hadhara.

Mbowe na viongozi wenzake wa kitaifa waliingia kimya kimya jijini Mwanza na kufikia katika moja ya hoteli za kitalii katikati ya jiji.

Walianza safari ya kwenda viwanja vya Furahisha kwa msafara wa magari zaidi ya 10 iliyoongozwa na gari nne za polisi; mbili zikitangulia mbele na nyingine ikiimarisha ulinzi nyuma.

Kutoka hotelini, Mbowe akiongozana na Katibu Mkuu, John Mnyika na wajumbe kadhaa wa Kamati Kuu ya chama hicho.