Chadema yahoji mamilioni yake kuzuiwa, Ofisi ya Waziri Mkuu yaeleza
Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 17, 2026 jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk Jim Yonazi, amejitenga na suala hilo akidai lipo chini ya mamlaka ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Dar es Salaam. Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika ameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuingilia kati suala la kuzuiwa kwa fedha za ruzuku za chama hicho kiasi cha Sh500 milioni na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kinyume na kisheria.
Amesema fedha hizo ni halali kwa Chadema na zinahusu kipindi cha Juni hadi Oktoba 2025. Fedha hizo zinatokana na uwakilishi wa chama hicho bungeni.Huku akieleza wasiwasi wao ni kuwa fedha hizo zinaweza kurejeshwa Hazina kutokana na mwaka wa fedha wa Serikali kuelekea ukingoni.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dk Jim Yonazi, ambaye katika majibu yake amejitenga na suala hilo akidai lipo chini ya mamlaka ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Kama wanadai fedha hizo, ni wajibu wao kutambua kuwa ofisi inayohusika ni Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na si Ofisi ya Waziri Mkuu kama wanavyodai, hatuwezi kuongilia,” amesema Dk Yonazi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumatano, Juni 17,2026 Mnyika amesema Chadema imekuwa ikidai fedha hizo kwa muda mrefu kupitia barua mbalimbali kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na kupitia mikutano ya hadhara, lakini hadi sasa hakujaingiziwa kwenye akaunti ya chama hicho.
“Tunadai fedha zetu Sh500 milioni kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambayo imezizuia kuanzia Juni hadi Oktoba 2025. Fedha hizo zipo katika ofisi hiyo kama sehemu ya njama haramu za kuidhibiti Chadema na kuinyima fedha zake halali,” amesema Mnyika.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo ina jukumu la kusimamia masuala yanayohusiana na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, inapaswa kuingilia kati ili kuhakikisha chama hicho kinapata haki yake, kwani juhudi zake za kufuatilia suala hilo hazijazaa matunda.
“Tunaiomba Ofisi ya Waziri Mkuu kuchukua hatua za haraka kuhakikisha fedha hizo zinaingizwa katika akaunti ya chama. Tunaona kuna njama za kuchelewesha mchakato huo hadi mwisho wa mwaka wa fedha.
“Tunafahamu kuna mchezo unaofanyika ili muda upite hadi Juni 30, 2026, mwaka wa fedha ufungwe na fedha zirudishwe Hazina, kisha waelezwe kuwa haziwezi kutolewa tena,” amesema.
Mnyika amedai kuendelea kuzishikilia fedha hizo ni kinyume cha sheria, kwani hapo awali Ofisi ya Msajili ilikuwa ikieleza kulikuwa na zuio la mahakama, lakini zuio hilo liliondolewa mwezi Aprili mwaka huu bila fedha hizo kuingizwa katika akaunti ya chama.
“Kabla ya hapo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa walikuwa wanadai hawamtambui Katibu Mkuu. Mahakama iliweka zuio dhidi ya uamuzi wa Msajili wa kutomtambua Katibu Mkuu, hivyo Sekretarieti ya chama inatambulika. Tunajua huu ni mchezo wa hujuma kwa sababu fedha zetu bado hazijaingizwa kwenye akaunti ya chama,” amesema.
Mnyika amesema hapo awali Chadema ilikuwa ikitegemea ruzuku kama chanzo kikuu cha fedha za kuendesha shughuli zake za kitaifa. Kwa mujibu wake, kuanzia mwaka 2020 chama kilikuwa kinapokea Sh107 milioni kila mwezi.
Amefafanua kati ya mwaka 2015 na 2020, Chadema ilikuwa ikipokea ruzuku ya Sh323 milioni kwa mwezi, ambapo asilimia 85 ya fedha hizo zilitumika katika shughuli za uendeshaji wa chama, huku asilimia 15 iliyobaki ikitokana na vyanzo vingine vya mapato.
Wakati huo huo, Mwananchi ilimtafuta Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ili kupata ufafanuzi kuhusu madai hayo ya Chadema Hata hivyo, simu yake ilipokelewa na msaidizi wake, ambaye amesema kuwa alikuwa kwenye kikao. Jitihada za kumtafuta zinaendelea.