Chadema yatoa siku 10 Serikali kueleza walipo waliotekwa
Muktasari:
- Chadema imetoa siku 10 hadi Septemba 21, 2024, kwa Serikali kueleza walipo watoto, viongozi na wanachama wake waliodaiwa kutekwa.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), kimetoa muda hadi Septemba 21, 2024 kwa Serikali kueleza wapi walipo watoto, viongozi na wanachama wa chama hicho wanaodaiwa kutekwa na wengine kupotea huku kikisisitiza kuwa jambo hilo lazima lifike ukomo.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Septemba 11, na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, katika kikao cha viongozi wa kanda zote za Dar es Salaam na Pwani kilichofanyika makao makuu ya chama hicho Mikocheni, Dar es Salaam.
“Lazima jambo hili lifike mwisho kwa kuwa wao wamekataa kulifikisha mwisho, sisi tutawalazimisha lifike mwisho na ili tufanikishe hili, tunahitaji kuwa kitu kimoja, kila mmoja wetu anahitaji kuwa bega la kukulilia mwenzake, na tukubaliana kwamba kila damu ya mwana Chadema inayopotea tutaitetea kwa nguvu kubwa.
“Tunaipa Serikali mpaka siku ya Jumamosi tahere 21, mwezi huu wa tisa watueleze watoto wetu, viongozi wetu na wanachama wetu niliowataja hapa wako wapi... Tumetoa mpaka tarehe 21 mwezi huu,” amesema Mbowe huku akisiistiza kuwa wanataka kuona viongozi wakiwajibika.
Mbowe alikuwa anamaanisha Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke, Deusdedith Soka na Katibu wake, Jacob Mlay pamoja dereva wao wa pikipiki, Frank Mbise waliodaiwa kutekwa baada ya kupigiwa simu wafuatilie polisi pikipiki ya soka iliyokuwa imeibwa.
Suala vijana hao lilifikishwa mahakamani na mawakili wakitaka korti iamuru polisi iwaachiwe huru au wapewe dhamana, lakini mahakama ikasema hakuna uthibitishwa kwamba wanashikiliwa na jeshi hilo.
Vilevile, Mahakama ililiagiza Jeshi la Polisi liwatafute vijana hao, suala ambalo msemaji wa jeshi hilo alishasema utekelezaji wake unaendelea.
Endelea kufuatilia Mwananchi.