Wametekwa au wamepotea?

Muktasari:

  • Matukio hayo yameibuka kuanzia mwaka 2021 na kuendelea, huku yakiibua taharuki kwa wananchi, wakilihoji Jeshi la Polisi lenye dhamana ya ulinzi wa wananchi na mali zao kuhusu kinachoendelea juu ya hatima ya wapendwa wao.

Dar/mikoani. Kufuatia matukio ya watu kutoweka na wengine kutekwa nchini, baadhi ya wadau wameitaka Serikali kuwajibika.

Matukio hayo yameibuka kuanzia mwaka 2021 na kuendelea, huku yakiibua taharuki kwa wananchi, wakilihoji Jeshi la Polisi lenye dhamana ya ulinzi wa wananchi na mali zao kuhusu kinachoendelea juu ya hatima ya wapendwa wao.

Leo Alhamisi Februari Mosi, 2024 Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime hakupatikana kuzungumzia suala hilo kila alipotafutwa kwa simu yake ya kiganjani. Na hata alipotumiwa ujumbe mfupi kujua kinachoendelea juu ya matukio hayo hakujibu.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alipopigiwa simu, alikata na kumjulisha mwandishi kwa ujumbe ulioandikwa: “Nipo kwenye live event (tukio mubashara).”


Waliotekwa

Miongoni mwa matukio hayo ni la kutekwa kwa aliyekuwa mfanyabiashara na fundi simu eneo la Kariakoo Dar es Salaam, Innocent Elias Liveti (34) maarufu Macheni.

Kwa mujibu wa mashuhuda na picha za video zilizochukuliwa na kamera za usalama, Desemba Mosi, 2023 saa 1:30 asubuhi Liveti alikuwa amekaa mbele ya duka lake lililopo Mtaa wa Narung'ombe, walitokea watu wawili waliovalia kofia na kuingia naye ndani ya gari na kuondoka naye.

Hadi sasa zimepita siku 62, Liveti hajapatikana. Tukio lingine ni la kutekwa kwa mfanyabiashara Mussa Mziba (37) aliyekuwa akimiliki kampuni ya Mziba Empire Investment Ltd yenye ofisi zake Mikocheni Dar es Salaam.

Mziba alitekwa na watu wawili waliofika ofisini kwake saa 2 usiku Desemba 7 wakijitambulisha kuwa ni maofisa Polisi. Hadi sasa ni siku 54, Mziba hajulikani alipo.

Matukio hayo yalitanguliwa na kutoweka kwa Charles Wetinyi aliyedaiwa kukamatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi eneo la Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara Oktoba 23, 2023. Amefikisha siku 102 hajulikani alipo.

Pia, Wilson Damas alitoweka tangu kampeni za uchaguzi mwaka 2020 sasa ni zaidi ya miaka mitatu hajulikani pamoja na Richard Kayanda wote wakazi wa Nyandoto Tarime, Mkoa wa Mara.

Wengine waliopotea kwa pamoja Desemba 26, 2021 ni waliokuwa mafundi simu na wafanyabiashara katika soko la Kariakoo, Dar es Salaam walitekwa na watu waliokuwa wamevaa sare za polisi ambao hadi sasa ni siku 403 hawajulikani walipo.

Vijana hao ni pamoja na Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe na siku ya mwisho mmoja wao alituma ujumbe wa mfupi wa simu ukieleza wamekamatwa maeneo hayo wakiwa kwenye gari IST nyeusi na wanapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Mzazi wa Edwin, Longili Martin akizungumza na gazeti hili jana alisema tangu walivyoitwa na kufanya mazungumzo jijini Dodoma na Mkuu wa Jeshi la Polisi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Julai mwaka jana hawana mawasiliano tena na viongozi hao.

“Hakuna mawasiliano tena simu za viongozi hao kila tukipiga hazipatikani, tumebaki tunahangaika kuwatafuta watoto wetu na muda unazidi kwenda na tunashindwa sehemu ya kwenda,” alisema.


‘Ni utashi’

Katikati ya mijadala ya kutoweka kwa wananchi ikiwemo wananchi kujitokeza kwenye ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda kueleea jinsi wapendwa wao walivyotoweka, jana usiku, kulifanyika mjadala wa ‘Nini kifanyike kukabili matukio ya kutoweka kwa watu nchini?”

Mjadala huo uliandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd kupitia jukwaa lake la mijadala la Mwananchi Space katika mtandao wa X (zamani Twitter) ambapo mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Luqman Maloto alisema kukabiliana na matukio hayo ni suala la utashi wa Serikali.

Akifafanua, Maloto alisema matukio hayo yamekithiri kwa kuwa wanaoyatekeleza hawachukuliwi hatua.

“Hakujawa na utayari wa kuhakikisha haya mambo ya kuteka watu yanafika mwisho na yatazidi kuongezeka kadiri Serikali inavyozidi kukaa kimya, itafika wakati mtu ana nia mbaya na mali za mtu atamteka.

“Siku Serikali ikiamua au Rais aseme mambo haya yafike mwisho ni suala la kutamka tu.Alitamka hataki kesi za kubambikia zikafutwa,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema matukio hayo yamebainisha watu wanaotoweka sio maarufu bali ni wale wenye ugomvi au kesi mahakamani.

“Tumepata kesi nyingi na zimekuwa zikiongezeka, LHRC tumegundua uwepo wa watu wengi kutoweka na hao wanaotoweka sio watu maarufu, ni wale wenye ugomvi au kesi ipo mahakamani. Mwingine anahojiwa na polisi, anatoweka, tumepata kesi nyingi na zimekuwa zikiongezeka,” alisema.

Alisema suala hilo ni changamoto kubwa na ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

“Januari tumerekodi matukio mawili na Desemba tulirekodi mengine, nini kifanyike Serikali ina nafasi kubwa ya kuhakikisha usalama wa watu wake, Katiba inatoa suala la ulinzi na usalama Serikali ina wajibu wa kulinda watu wake.”

Naye mchambuzi wa Masuala ya kijamii, Dk Faraja Kristomus akizungumza katika mjadala huo, alisema kwa Tanzania mazingira yamekuwa tofauti kutokana na uhusiano wa kisiasa, kijamii na biashara.

“Tanzania tunaweza kuweka matukio haya katika mrengo wa kisiasa, sasa hivi matukio haya tunaweza kutarajia kwa sababu tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani.”

Pia, alisema kundi la pili ni migogoro kwenye jamii kwa sababu Jeshi la Polisi limenyooshewa kidole kutokuwa na mifumo ya kudhibiti matukio haya basi wahalifu wanaweza kutumia mwanya uliopo kuwateka maadui zao au wapinzani wao.


Malalamiko ziara ya Makonda

Akiwa katika mikoa ya Singida, Simiyu na Shinyanga, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda alikumbana na malalamiko ya wananchi kupoteza ndugu zao wanaodaiwa kutekwa miaka ya 2021, 2022 na 2023.

Akiwa mkoani Singida, Januari 29, mkazi wa wilayani Singida, Mwanahamisi Sombi, alimuomba Makonda kuingilia kati kuhusu kutoweka ndugu wa familia moja, Haruna Iddi (50) na Juma Iddi (45) waliopotea katika mazingira yenye utata Desemba 28, mwaka jana, saa 10 jioni katika maeneo ya Mwenge.

Akizungumzia suala hilo katika mkutano huo wa Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba alisema: “Jambo hili nalifahamu sana, mtu huyo amekuja ofisini kwangu mara mbili, baadaye nikamjumuisha RPC ambaye amemjulisha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura walimtafuta kwenye vituo vyote vya polisi nchini hawakufanikiwa.”

Malalamiko kama hayo yalitolewa mkoani Shinyanga katika eneo la Tinde, ambapo Nyangeta Malawa alisema mume wake John Chacha alitoweka Desemba 7, 2021.

Alisema tukio hilo lilitokea katika ofisi za ardhi za kata hiyo, ambako alipewa taarifa na ofisa mtendaji kata kuwa mume wake amechukuliwa na watu wasiojulikana.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, alitakiwa na Makonda kutoa ufafanuzi ili umma ujue.

"Nilipofika Agosti 2023 nilikuta malalamiko haya na aliyekuwa anakuja ofisini ni shemeji yake, aliyenipa malalamiko,” alisema.

Mwingine aliyelalamika kupotelewa na kijana wake, Issa Hamis, ni Mariam Ndala aliyesema alitoweka tangu Novemba 25, 2022.

Alidai amekwenda polisi lakini hakuna ushirikiano, licha ya Kamanda Magomi kuwa rafiki yake na mwanawe.

Kamanda Magomi kwa maelekezo ya Makonda, alisema wana taarifa ya kupotea kwa Issa, ambaye ni fundi magari.

"Jeshi la Polisi kupitia mitandao ya kijamii tulifungua taarifa na tumeendelea kufuatilia katika mitandao, simu yake ilizimikia wapi na tulipeleka taarifa kwa kampuni za simu lakini hajufanikiwa," alisema.

Hata hivyo Mariam alipinga maelezo ya Kamanda Magomi, akisema siku moja kabla ya tukio walikuwa wote na mwanaye akimtengenezea gari.

Lakini Kamanda Magomi alisema hamfahamu Issa na taarifa za kupotea kwake zilitolewa kituo kikuu cha polisi na ofisini kwake lilikwenda jalada.

Msafara wa Makonda ukiwa Maswa mkoani Simiyu, alipokea malalamiko kutoka kwa Eliwaza Makwale kwamba, Desemba 23, 2022 mume wake alitoweka saa 10 jioni, akichukuliwa na watu wasiojulikana akiwa eneo lake la biashara.

Makonda alipomuita Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Maswa (OCD), Maganga Ngosha alisema amefika wilayani humo mwaka jana, na amekuta jalada hilo na wanaendelea kulifanyia kazi.

Mbali na matukio ya miaka ya hivi karibuni, kulikuwa na matukio ya watu kutoweka, ambapo Novemba 2016 aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane alipotea na hadi sasa hajapatikana.

Mwaka 2017 Diwani wa Kibondo, Simon Kangoye alitoweka na hakuwahi kupatikana na mwaka huo huo, aliyekuwa mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda naye alitoweka na hajapatikana hadi sasa.