Ndugu wa wafanyabiashara waliopotea waiangukia Polisi

Mmoja wa wafanyabiashara waliopotea, Juma Iddi (kushoto) na Haruna Iddi (kulia).

Muktasari:

  • Familia ya wafanyabiashara wawili wa mbao waliopotea mwaka jana, wameliomba Jeshi la la Polisi nchini kusaidia kuwatafuta ndugu baada ya wao kufanya hivyo  bila mafanikio, huku wakiwa hawana taarifa yeyote ya kinachoendelea kutoka katika jeshi hilo, licha ya kuwasilisha taarifa ya kupotea kwao.

Singida. Ndugu wa wafanyabiashara wawili wa mbao waliopotea mwaka jana, wameliangukia Jeshi la Polisi nchini, wakitaka liwasaidie kuwatafuta ndugu zao.

Familia hiyo imesema kuwa imewatafuta ndugu zao hao bila mafanikio, hivyo inaliomba jeshi hilo kuwasaidia kufanya hivyo.

Wafanyabiashara hao wa mbao Juma Iddi (45) na Haruna Iddi (50) walitoweka mnamo Desemba 28, 2023  saa 10 jioni katika maeneo tofauti ya Mwenge na Mghanga, mjini Singida

Akizungumza na Mwananchi Digital, mmoja wa wanafamilia hao, Seif Juma amesema wao kama familia hawana tena cha kufanya zaidi ya kuvisikiliza vyombo vya ulinzi na usalama baada ya kuwatafuta bila mafanikio tangu mwaka jana.

Amesema licha ya kutoa taarifa Polisi hadi sasa hawajapata mrejesho wowote kutoka jeshi hilo juu ya kupotea kwa ndugu zao.

"Hatuna tena cha kufanya tumewaachia Polisi watusaidie kuwatafuta ndugu zetu, mpaka leo hii hawajatupa ushirikiano. Hakuna chochote walichotuambia kuwa kinaendelea kwa hiyo tupo tu na majonzi hatujui walipo," amesema Seif.

Januari 3, 2024, mmoja wa mashuhuda, Hassan Seif alisema akiwa Mwenge mkoani Singida, alishuhudia mmoja wa wafanyabiashara hao akichukuliwa na watu wawili walioshuka kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye rangi nyeupe.

Alidai baada ya kumpakia kwenye gari hilo liliondoka kwa mwendo wa kasi kutoka kwenye eneo hilo.

Awali Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa alisema wamefanya taratibu zote za kipolisi na kuwasilisha makao makuu.

"Kuhusu hao wafanyabiashara tulishafanya taratibu zote za kipolisi na tumeshawasilisha makao makuu. Kwa hiyo anayetakiwa kutolea maelezo ni Msemaji wa Jeshi la Polisi ngazi ya Taifa Kamanda David Misime na siyo sisi,” alisema.

Hata hivyo alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Misime jana hakupatikana kwa siku nzima baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu.

Juhudi za kumtafuta Misime kulizungumzia suala hilo zinaendelea japo kuanzia saa tatu asubuhi ya leo, simu yake haikuwa ikipatikana.