Waziri Tax: Mtanzania kutekwa Nigeria ni viashiria vya ugaidi

Muktasari:

  • Mtanzania huyo Melkiori Mahinini (27) ambaye ni Frateri wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers), mzaliwa wa Parokia ya Kabanga, Jimbo la Kigoma, alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Agosti 3 mwaka huu, katika jimbo la Minna huko Nigeria akiwa na mwenzake, Padri Paul Sanogo, raia wa Burkina Faso.

Arusha. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, amesema kuwa utekaji wa Mtanzania huko nchini Nigeria ni viashiria vya ugaidi.

Dk Tax ameyasema hayo jana Agosti 9, 2023 jijini Arusha, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ya kutembelea miradi ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).

"Ni kweli kuna Mtanzania mwenzetu ametekwa huko Nigeria na tunatoa pole kwa familia yake na Kanisa Katoliki nchini, na ili linatokana na matatizo ya kiusalama katika nchi na ugaidi," amesema waziri huyo mwenye dhamana ya mambo ya nje.

Amesema kuwa hadi sasa hakuna sababu ya msingi iliyotolewa na watekaji hao, zaidi ya kudai pesa ili kuwaachia.

"Huu ni uhalifu kama aina zingine za uhalifu na Tanzania tumekuwa tukipigana sana kuhakikisha tunapambana na hili tatizo, hivyo  tunapaswa kama wananchi tusaidiane kuhakikisha kwamba viashiria vyote vinavyoweza kuatarisha usalama wa nchi tunapambana navyo" amesema Dk Tax na kuongeza...

"Lakini pia tutoe taarifa kwenye taasisi husika tunapoona viashiria hivi ili tuweze kutatua matatizo ya namna hiyo mapema katika kuwaokoa wenzetu lakini pia kabla hayajaota mizizi."

Aidha Mtanzania huyo Melkiori Mahinini (27) ambaye ni frateri wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) mzaliwa wa Parokia ya Kabanga, Jimbo la Kigoma, alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Agosti 3 mwaka huu, katika jimbo la Minna huko Nigeria akiwa na mwenzake, Padri Paul Sanogo, raia wa Burkina Faso.

Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dk Benson Bana amesema Serikali kwa kushirikiana na taasisi husika wanachukua hatua mbalimbali kuhakikisha Mtanzania huyo, pamoja na mwenzake wa Burkina Faso wanaachiwa huru.

"Taarifa tulizopata, watekaji wanataka Naira 100 milioni (sawa na Sh325.1 milioni) ili kuwaachia huru wote wawili na tumepiga hesabu kila mmoja anatakiwa kulipiwa karibu Dola 70,000 za Marekani 70,000 (zaidi ya Sh170 milioni)," amesema.