Simulizi mfanyabiashara Dar alivyotekwa

Mmiliki wa kampuni ya Mzibaz Emprire Investment Ltd, Mussa Mziba aliyetoweka Desemba 7, 2023 Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Ni zaidi ya mwezi mzima sasa, mfanyabiashara Mussa Mziba (37) haonekani nyumbani kwake, ofisini kwake wala mitaani. Mkewe na watoto, ndugu jamaa na marafiki wameshikwa na taharuki, wasijue aliko ndugu yao, na kama yuko hai ama ameuawa na kama yuko hai, anafanya nini na wapi?

Kwa mujbu wa wasaidizi wake, Mziba aliyekuwa akimiliki kampuni yake ya Mziba Empire Investment Ltd, alichukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni maofisa wa Polisi, wakidai kuwa wanakwenda kufanya mahojiano naye katika kituo cha Polisi Oysterbay Desemba 7, 2023 saa 2 usiku.

Hata hivyo, mkewe Dorcas Tarimo na wasaidizi wake walipofuatilia katika kituo hicho kesho yake, hawakumpata huku polisi wakikana kuwatuma maofisa hao kumkamata.

Jana Kamanda wa Polisi Kinondoni, Mtatiro Kiktwiki alipoulizwa na Mwananchi alisema bado hawajapata taarifa za Mziba.

“Mpaka sasa uchunguzi wa jambo hili unaendelea. Hata Kamishna wa Kanda Maalum alishalizungumzia suala hili, tunaendelea kulifanyia kazi,” alisema Kamanda Mtatiro.


Alivyotoweka

Akizungumzia tukio la kuchukuliwa kwa Mziba, msaidizi wake, Crispin Malando alisema siku hiyo baada ya kazi za siku nzima, walifanya kikao ofisini kwao Mikocheni.

“Siku hiyo tulitingwa sana, lakini baadaye tukawa na kikao cha jioni. Kwa hiyo mizunguko ya mchana alikuwa anatumia gari tofauti na niliyotumia mimi.

“Jioni yake akanipigia simu akaniuliza uko wapi? Nikamwambia niko Mikocheni, akasema nakuomba ofisini, nikamuuliza mbona umeme umekatika? Akasema njoo kuna jambo muhimu sana la kujadili. Akaniambia kama uko mbali acha gari chukua pikipiki, nikamwambia niko karibu tu,” alisema.

Alipofika ofisini, anasema walifanya kikao kilichoisha saa 2 usiku, kisha wakaanza kutoka ofisini.

“Mara nyingi tuna mtindo wa kupanda gari ndani ya uzio wa ofisi, halafu mlinzi anafungua mlango tuaondoka, lakini siku hiyo, alimwambia dereva atoe gari nje, kuna maagizo alikuwa anampa mlinzi wetu,” alisema.

Aliendelea kueleza kuwa, alipotoka nje ya geti aliona magari mawili yameegeshwa karibu na uzio wa ofisi yao, moja ilikuwa Toyota Rav 4 nyeupe na Toyota Wish.

“Akatoka mtu mmoja kwenye moja ya yale magari. Wakati bosi anafungua mlango wa gari lake, yule mtu aliyetoka kwenye gari akaita Mussa, bosi akashtuka, akaitika na kuelekea kwa yule mtu, wakawa wanaongea.

“Kwa kuwa umeme ulikuwa umekatika Mikocheni yote, yule mtu akatoa vitambulisho, bosi akawa anamulika vile vitambulisho kwa tochi, akamwomba waingie ofisini wajadili hayo mambo, lakini jamaa akamwambia haina haja, yeye yuko na wenzake watatu walikuwa pembeni, akataka waende kuyazungumza Polisi Oysterbay.

“Bosi naye nadhani aliona Oysterbay Polisi ni salama kwake, akakubali. Wakaingia kwenye gari, lakini dereva wake akamfuata akauliza, vipi? Bosi akasema usijali nazungumza na washkaji nawapa maelekezo kwamba wapi mnanifuata,” alinukuu maneno ya mwisho ya bosi wake.

Wakati magari yanaondoka, anasema kati ya wale watu waliokuja na magari, mmoja wao alibaki.

“Mlinzi wetu ana pikipiki na alikuwa akisubiri kumpeleka mgeni wetu mahali. Yule mtu akamfuata mlinzi, akamwambia samahani, naomba nipeleke nifuate zile gari, yule mgeni akasema kwa sababu yale magari yameondoka na bosi, mpeleke, halafu mimi nitaangalia utaratibu mwingine.

“Yule mlinzi akamchukua yule mtu wakawa wanatembea kufuata yale magari ambayo hata hivyo yalishatokomea.”

Anasema wakati wanatembea, yule jamaa aliyempakiza alikuwa akifanya mawasiliano na wenzake… “Wapi? tunapandisha hivi. Walipofika Shoppers yule jamaa akapiga tena simu “Wapi?’ jamaa wakamjibu wako hospitali ya Kairuki, kwa hiyo wakabadilisha njia wakaenda hadi hospitali ya Kairuki, akamshusha pale. Alitembea mbele kidogo akapanda gari nyingine iliyokuwa ikimsubiri."

Malando alisema muda mfupi baada ya bosi wao kuondoka, simu zake zikawa hazipatikani.

“Tumejaribu kupambana, tumetoa taarifa kwenye vyombo vya usalama, tuliripoti Polisi Oysterbay, faili likafunguliwa na Ofisa upelelezi wa wilaya (OC-CID), ikaundwa timu wakaja pale ofisini kukagua kamera na kutuhoji.

“Baada ya wiki moja, tukaitwa Polisi Oysterbay mimi, dereva na mlinzi kwa ajili ya mahojiano, tukapelekwa kituo kikuu cha polisi, tukakaa siku nne, wanatuuliza tu maswali,” alisema.


Kauli ya mkewe

Mkewe, Dorcas Mringo alisema alizungunmza na na mumewe dakika chache kabla hajatoweka.

“Niliongea na mume wangu muda wa saa 2:27 usiku, alikuwa na mfanyakazi mwezake, dereva wake walikuwa wametoka ofisini,” alisema.

Hata hivyo, mumewe hakurudi na ilipofika kesho yake alimuuliza dereva wake.

“Akanieleza kilichotokea, ila wakanitoa wasiwasi wakisema watakwenda vituo vya Polisi kuangalia. Wakaangalia siku nzima ya Ijumaa, hawakumpata. Ilipofika Jumamosi tukaanza kuangalia hospitali mbalimbali. Niliwapigia kaka na dada zake, nikawaambia simuoni mume wangu,” alisema.

Jumapili Desemba 10, 2023 walikwenda Polisi Oysterbay kuripoti rasmi na kupewa namba (RB): KIN/CID/PE168/2023.

“Likafunguliwa jalada la upelelezi kwa Ofisa Upelelezi wa Wilaya. Kesho yake wakasema watachukua maelezo ya mtu aliyekuwa karibu na mume wangu, hivyo nikamwita Malando aliyekuja kuandika maelezo.

“Baada ya siku mbili nikaenda kwa RCO tukatoa tena maelezo mengine na aliagiza apelekewe faili kutoka kwa OC CID. Akachukua namba za Mussa alizokuwa akitumia akasema atawapa watu wa Cyber Crime (kitengo cha makosa ya mitandao) wafuatilie,” alisema.

Tangu wakati huo, Dorcas anasema hawajapata taarifa zozote na polisi wanasema wanaendelea na uchunguzi.


Matukio mengine

Kutoweka kwa Mussa Mziba kumekuja sambamba na tukio la kupotea kwa watu watatu waliokuwa wakisafiri kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam.

Watatu hao ilielezwa walisafiri kwa gari moja kutoka Kyela mkoani Mbeya kwa shughuIi za kibiashara lakini tangu Desemba 6, 2023 hawajulikani walipo na hawapatikani kwa simu.

Desemba 28, 2023 ndugu wawili mkoani Singida, Juma Iddi (45) na Haruna Iddi (50) walitoweka, saa 10 jioni katika maeneo tofauti ya Mwenge na Mghanga, mjini Singida.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa alisema wameshafungua jalada la uchunguzi juu ya tukio hilo na upelelezi utakapokamilika taarifa kamili itatolewa.

Hata hivyo, alipoulizwa juzi, alisema kwa sasa anayetakiwa kutolea maelezo juu ya hilo ni Msemaji wa Jeshi la Polisi ngazi ya Taifa.

Jana Mwananchi lilipomtafuta msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, alimtaka mwandishi arudi tena wa RPC wa Singida.

Hata ndugu wa wafanyabiashara hao wamekuwa wakisema wameliachia Jeshi la Polisi suala hilo.

Matukio hayo yalitanguliwa na kutoweka kwa Charles Wetinyi aliyedaiwa kukamatwa na watu waliojitambulisha kuwa Polisi eneo la Mugumu wilayani Serengeti Mkoa wa Mara Oktoba 23, 2023.

Tukio hilo liliibuliwa na Mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche kupitia ukurasa wake wa X akilituhumu Jeshi la Polisi kumteka Wetinyi.

Kufuatia tuhuma hizo, Heche aliitwa ofisi ya Ofisa Upelelezi wa Mkoa (RCO) Desemba 19 na alifika na kuhojiwa na kuachiwa.