KUELEKEA MWISHO WA MWAKA 2018; Matukio ya utekaji, kupotea watu yalishtua Taifa, dunia

Moja ya mambo yaliyolishtua Taifa 2018 ni matukio ya watu wakiwamo wafanyabiashara, viongozi wa dini, wanafunzi na watoto kutekwa na watu wasiojulikana au kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Kutopatikana kwa baadhi ya watu waliotekwa au kupotea kuliongeza hofu huku vyombo vya dola vikiapa kufanya kila linalowezekana kumaliza matukio hayo.

Kutokana na matukio hayo, vyombo vya dola hususan Jeshi la Polisi lilijikuta katika wakati mgumu baada ya kulaumiwa na wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu kwa madai kuwa wameshindwa kuwakamata wahusika au washukiwa.

Tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu Mohammed Dewji maarufu ‘Mo’ Oktoba 11, ndilo lililotikisa zaidi na kumulikwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi na kuibua maswali mengi ya nani waliomteka na walitaka nini kutoka kwake.

Mo alitekwa alfajiri ya Oktoba 11 alipokuwa akienda mazoezini katika Hoteli ya Coloseum jijini Dar es Salaam na alipatikana siku tisa baadaye.

Katika tukio hilo, Mo aliyekuwa na desturi ya kufanya mazoezi katika hoteli hiyo alivamiwa na watu wasiojulikana alipokuwa akishuka kwenye gari lake aina ya Range Rover. Walifyatua risasi hewani kisha kumchukua mfanyabiashara huyo na kutokomea naye wakitumia gari walilokuwa nalo. Hata hivyo, baada ya siku tisa za utafutaji wa polisi, Mo alipatikana akiwa ametelekezwa kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.

Siku moja kabla ya kupatikana kwake, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro alisema wamebaini gari aina ya Hilux Surf lililomteka mfanyabiashara huyo kupitia kamera za ulinzi (CCTV) za hoteli aliyokwenda kufanya mazoezi.

Siku Mo alipopatikana gari hilo pia lilikuwa limetelekezwa katika viwanja hivyo likiwa na silaha ndani yake.

Hata hivyo, tukio hilo liliacha maswali mengi hasa picha iliyoonyeshwa na IGP Sirro ya gari lililodaiwa kutumika kumteka Mo ikionekana kutofautiana kidogo na gari husika

Maswali mengine yaliyogonga vichwa vya watu ni siku gari hilo lililodaiwa kutokea nje ya mipaka ya Tanzania kupita mipakani bila kutambuliwa.

Isitoshe, wapoa waliohoji iweje gari hilo likatize katika mitaa ya Dar es Salaam bila kukamatwa ilhali polisi walikuwa wameimarisha ulinzi.

Mtoto mchanga atoweka

Mtoto Shaaban Ngunda mwenye umri wa miezi sita alipotea Novemba 6 katika mazingira ya kutatanisha eneo ya Mbagala Charambe wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.

Mama mdogo wa Ngunda, Siri Nongwa aliliambia Mwananchi kuwa mtoto huyo alikuwa hajaonekana tangu alipochukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwa mtu aliyemtaja kwa jina la Mama Rose, anayeishi mtaa wa Ubungo Mbagala - Charambe.

Siri alisema ingawa suala hilo bado linafanyiwa uchunguzi na polisi, familia ilikuwa katika mkakati wa kuomba kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuomba kusaidiwa ili kumpata mtoto huyo.

Sheikh atekwa chuoni

Tukio jingine ni la kupotea kwa Mkuu wa Chuo cha Nyakato Islamic kilichopo chini ya Taasisi ya Elimu ya The Registered Trustees of Islamic, Sheikh Bashir Gora Desemba 6.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shanna alikiri kupokea taarifa za kupotea kwa sheikh huyo, hivyo ameagiza kuimarishwa kwa uchunguzi wa mipaka yote ya Mkoa wa Mwanza ili kuhakikisha kiongozi huyo anapatikana mapema iwezekanavyo.

“Ni kweli tumezipata taarifa za kupotea kwake, lakini unajua mtu akipotea huwezi kujua tatizo ni nini na hatujui kwa nini hapatikani na tumemtafuta kila mahali hapatikani, tumeshafunga mitambo yetu kwenye maeneo yetu yote,” alisema Shana siku chache baada ya tukio hilo.

Akizungumza hivi karibuni, Katibu wa bodi wa taasisi hiyo, Sadik Mchola alisema tukio hilo lilitokea Desemba 6 chuoni hapo ambapo alifika kijana mmoja kuulizia nafasi za kujiunga na chuo kwa ajili ya mdogo wake.

Alisema, “Kijana huyo alitukuta ofisini, sheikh akamwambia aje Januari mwakani atapewa utaratibu, kijana aliondoka lakini baada ya muda kidogo akarudi tena kuulizia malipo, sheikh akamwambia Januari ndiyo tutakueleza kila kitu, akaondoka,”

“Baada ya hapo wakawa wanazungumza na sheikh huku anamsindikiza (kutoka ndani ya ofisi) kumbe walikuwa wameegesha gari yao nyuma ya chuo, walipoikaribia alitoka kijana mwingine kwenye gari hiyo wakambeba sheikh na kumuingiza ndani kisha gari likaondoka kwa spidi kali.”

Lugola azungumza

Wakati tukio la kutekwa kwa Mo likirindima, Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna watu wapatao 75 wametekwa katika kipindi cha miaka mitatu.

Kauli ya Lugola ilikuja zikiwa zimepita siku nne tangu alipotekwa mfanyabisahara huyo, ambapo alisema bado uchunguzi unaendelea.

Alisema licha ya juhudi za Jeshi la Polisi nchini, mwaka 2016 kulikuwa na matukio ya watu tisa kutekwa, lakini watano walipatikana wakiwa hai kwa ushirkiano na wananchi. “Watu wanne hawakupatikana. Katika kipindi hicho watuhumiwa sita walikamatwa, watano walifikishwa mahakamani na mmoja aliuawa na wananchi,” alisema Lugola.

Alisema mwaka 2017 watu 27 walitekwa ambapo Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwapata 22 wakiwa hai na wawili wakiwa wamekufa huku watu watatu hawakupatikana. “Katika kipindi cha Januari hadi Oktoba 11, 2018 watu 21 walitekwa ambapo kati yao 17 walipatikana wakiwa hai na wanne hawakupatikana hadi sasa. Watuhumiwa 10 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.”.

Kuhusu utekaji wa watoto, alisema kati ya 2016 hadi 2018 watoto 18 miongoni mwao wa kiume sita na wa kike 12 walitekwa.

“Watoto 15 walipatikana wakiwa hai, watoto wawili walipatikana wakiwa wamefariki na mtoto mmoja bado hajapatikana,” alisema Waziri Lugola.

Lugola alitaja sababu za utekaji huo kuwa ni za kisiasa, kiuchumi, kulipiza visasi, wivu wa kimapenzi na ushirikina.

Hata hivyo alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu sababu za kisiasa, alisema ni sababu za jumla tu kwa sababu hawajawapata watu wa aina hiyo.