Mwarobaini kutoweka kwa watu Tanzania watolewa

Muktasari:

  • Wadau mbalimbali wameelezea matukio ya kutoweka kwa watu nchini Tanzania katika mazingira ya kutatanisha ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara sambamba na kutoa ushauri juu ya kumaliza changamoto hiyo.

Dar es Salaam. Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania, Luqman Maloto amesema matukio ya watu kutoweka katika mazingira ya kutatanisha yanasababishwa na suala zima la utashi.

 Maloto ametoa kauli hiyo kipindi ambacho kumeibuka kesi za watu kupotea maeneo mbalimbali nchini hali inayoibua wasiwasi na maswali kwa jamii.

Hilo linathibitishwa hata katika ziara ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda anayoifanya hivi karibuni na kukutana na taarifa za watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha mikoa Simiyu, Shinyanga na Singida.

Leo Jumatano ya Januari 31, 2024, kumefanyika mjadala Mwananchi Space wenye mada isemayo, ‘nini kifanyike kukabili matukio ya kutoweka kwa watu nchini?.”

Akichangia mada hiyo, Maloto amesema kuna vitu vinapaswa kutazamwa kwanza na kwamba  mtu akifanya tukio halafu hatua haichukuliwi ni sawa na mtoto afanye kosa na asiadhibiwe, hivyo wengine watafanya makosa hayo.

“Kwa hiyo kwa sababu kumekuwa na historia ya matukio haya kwa miaka mingi, kuna watu wameona ni rahisi watu kutekwa na haifuatiliwi. Wanasema watu wakitekwa Tanzania wananchi wataishia kupiga kelele na kutulia,” amesema Maloto.

Akitolea mfano Maloto kuhusu majibu kuhusu kupotea kwa Mwandishi wa Mwananchi, Azory Gwanda, wa Kibiti, Mkoa wa Pwani Desemba 2017 amesema kulikuwa na majibu tofauti  kutoka serikalini juu ya kupotea kwa Azory ambaye mpaka sasa hajawahi kupatikana.

Maloto amesema mkwamo wa mambo hayo ni utashi, kwa kuwa unaweza kuwalaumu polisi kwa sababu ni walinzi wa raia na mali zao au Bunge.

 “Hakujawa na utayari wa kuhakikisha haya mambo ya kuteka watu yanafika mwisho na yatazidi kuongezeka kadiri Serikali inavyozidi kukaa kimya, itafika wakati mtu anania mbaya na mali za mtu atamteka.

“Siku Serikali ikiamua au Rais aseme mambo haya yafike mwisho ni suala la kutamka tu,  alitamka hataki kesi za kubambikia zikafutwa,” amesema.

Mei 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa agizo la kulitaka Jeshi la Polisi kujichunguza na kufuta kesi zote za kubambikizia wananchi makosa, yakiwamo ya uhujumu uchumi,

Akizindua kiwanda cha kushona nguo cha Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, Rais Samia alisema kumekuwepo na suala la ubambikiaji wa kesi na kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) walifuta kesi 147 walizobambikia watu makosa na akaagiza polisi nao wajikague.

“…nimezitaka taasisi zote, ikiwamo Jeshi la Polisi ambalo uchunguzi unaanza kwenu kufanya chunguzi za kesi mbalimbali zilizopo ili kuharakisha kesi kusikilizwa na aidha kufutwa au mtu kuhukumiwa ipasavyo.

“Lakini pia, niongee na Polisi, nanyi mpunguze kesi za kubambikiza. Kuna mlolongo mkubwa wa kesi ya kubambikiza, ukipungua na mahabusu kule ndani watapungua kwa sababu wengi wapo, wanasubiri kuhukumiwa kesi haziendi na ushahidi hakuna," alisisitiza Rais Samia.

LHRC waeleza hali ilivyo

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga kwenye mjadala huo amebainisha watu wanaotoweka sio maarufu bali ni wale wenye ugomvi au kesi mahakamani.

“Tumepata kesi nyingi na zimekuwa zikiongezeka, watu kupotea ni kulazimishwa kupotea, LHRC tumegundua uwepo wa watu wengi kutoweka na wanaotoweka sio watu maarufu, ni wale wenye ugomvi au kesi ipo mahakamani akatoweka, mwingine anahojiwa na polisi katoweka, tumepata kesi nyingi na zimekuwa zikiongezeka.”

Henga amesema suala hilo ni changamoto kubwa na ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

 “Januari tumerekodi matukio mawili na Desemba tulirekodi mengine, nini kifanyike Serikali ina nafasi kubwa ya kuhakikisha usalama wa watu wake, Katiba inatoa suala la ulinzi na usalama Serikali ina wajibu wa kulinda watu wake.”

Pia, amesema mtu akienda kufuatilia ndugu zake kupotea basi apate ushirikiano, akienda polisi anapelekwa huku mara kule, sasa mamlaka zinazohusika zifanye kazi yake watu wapatikane.

Awali, Mwandishi Mwandamizi wa Mwananchi, Elias Msuya akichokoza mada hiyo amesema kwa muda mrefu kumekuwa na matukio ya watu kupotea na kutekwa tangu yalipoanza kuvuma mwaka 2016.

Akitolea mfano amesema aliyekuwa msaidizi wa Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Ben Saanane alipotea na juhudi zilizofanyika kumtafuta zilishindikana na hata Jeshi la Polisi lilisema linamtafuta lakini juhudi zake hazikuzaa matunda mpaka sasa.

“Hata mwaka 2017 Diwani wa Kibondo, Simon Kangoye aliwahi kutoweka na hakuwahi kupatikana, pia kumewahi kutokea malalamiko ya watu kunyanyaswa na kuteswa na yakatulia matukio hayo, lakini mwaka 2023 matukio hayo yaliripotiwa, kuna mfanyabiashara anaitwa Musa Mziba alichukuliwa eneo lake la kazi na watu waliojitambulisha polisi na mpaka sasa hakupatikana.

“Pia, kuna tukio la kutoweka na Mwandishi wa Mwananchi mwaka 2017, Azory Gwanda alichukuliwa na watu wasiojulikana na mpaka sasa hajapatikana.

“Kwa hiyo hili jambo linazua taharuki na kukosa majibu kwa vyombo vya dola, sababu ndio lina jukumu la kulinda watu na mali zao, kwa hiyo watu wanapopotea hivi ni wakati wa vyombo vya dola kutoa majibu yanayoeleweka,” amesema Msuya.

Akitoa rai, Msuya amesema jambo ambalo wananchi wanapaswa kujifunza ni haki yao, amesema mtu anapokamatwa ana haki ya kujua kwanini anakamatwa na anapofikishwa kituoni ana haki ya kuwajulisha ndugu zake, watu wamejikuta wakikamtwa bila kujua wanaowakamata ni polisi au ni kina nani.

“Vilevile tunapaswa kuimarisha ulinzi shirikishi na watu kujilinda, kama unakutana na mtu kwenye mazingira hatarishi, anakuambia ingia kwenye gari ni vyema ukataarifu watu wako au ukakimbia kuliko kuingia kwenye gari ambalo hata hulifahamu.

“Polisi, pia wanapaswa kutoa elimu ya kutosha ya uraia ili watu wasiingie kwenye mtego wa kutekwa au kukamatwa.”

Wakati Msuya akimaliza kuzungumza, mchangiaji mwingine Mustapha Mtupa amejazia kwa kuonyesha namna nchi za wenzetu zinavyotengeneza mifumo rafiki ya kupambana na matukio ya namna hiyo ili Tanzania iweze kuyatumia.

“Kwa nchi zilizoendelea utakuta kuna kamera za barabarani, kama kutatokea tukio lolote waweze kufanya upelelezi kwa urahisi matukio hayo yanapotokea.

“Sisi tunashindwa hata muelekeo watu walikopelekwa kwa hiyo Serikali ifunge mifumo CCTV kamera maeneo yenye utata zaidi ambayo matukio haya yanatokea kwa kiwango kikubwa,” ameshauri Mtupa.

Amesema matukio hayo pia huendana na kasi ya maendeleo, ingawa haikubaliki watu kupotea kizembe, lazima kuwe na njia za kukabiliana nayo.

Mchambuzi wa Masuala ya Kijamii, Dk Faraja Christomus amesema kwa Tanzania mazingira yamekuwa tofauti kutokana na mahusiano ya kisiasa, kijamii na biashara.

“Tanzania tunaweza kuweka matukio haya katika mrengo wa kisiasa, sasa hivi matukio haya tunaweza kutaraji kwa sababu tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani, wanasiasa wanaweza kutumia njia hii kuwanyamazisha wapinzani wao, wanaweza kutumia njia hizi kupata fedha kuingia kwenye uchaguzi.

“Pia, wanaweza kuteka sababu za kishirikiana, miaka ya nyuma watu wenye ualbino walitekwa sababu ya imani za kishirikina, wanasiasa wenye tamaa za madaraka wakatumia njia hizi,” amesema Dk Christomus.

Pia, amesema kundi la pili  ni migogoro kwenye jamii kwa sababu Jeshi la Polisi limenyooshewa kutokuwa na mifumo ya kudhibiti matukio haya basi wahalifu wanaweza kutumia mwanya uliopo kuwateka maadui zao au wapinzani wao.

Aidha, amesema kama jamii tunapaswa kuchukua tahadhari kwasababu tunaandamwa na vitisho vinavyosababisha kutekwa au kupotezwa, mtu anaweza kumteka mtu kwa kutaka mali zake.

“Tunapaswa kupanua wigo wa matukio haya ili tusitafute suluhu ya tatizo moja kumbe tunatakiwa kutafuta suluhisho mtambuka,” amesema Dk Christomus.