Hofu vijana watano wakitoweka kiutata Dar

Muktasari:

  • Familia zilizopotelewa na ndugu zao watano katika mazingira ya kutatanisha tangu Desemba 26, 2021 maeneo ya Kariakoo ‘Kamata’ wamepanga kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani awasaidie.

Dar es Salaam. Familia zilizopotelewa na ndugu zao watano katika mazingira ya kutatanisha tangu Desemba 26, 2021 maeneo ya Kariakoo ‘Kamata’ wamepanga kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani awasaidie.

Kwa mujibu wa familia hizo, wamefikia hatua hiyo baada ya kushindwa kupata msaada kutoka kwa Jeshi la Polisi tangu waliporipoti jambo hilo Desemba 27, 2021.

Waliopotea ni Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe.

Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya ndugu wa waliopotea walisema leo wanatarajia kufanya kikao cha pamoja ambacho ni maandalizi ya kwenda kumuona Waziri wa Mambo ya Ndani.

Naye Sylvia Quentin ambaye ni Mama mzazi wa Tawfiq Mohamed, alisema siku ya mwisho mmoja wao alituma ujumbe mfupi wa simu (sms) kuwa wamekamatwa eneo la Kariakoo wakiwa kwenye gari aina ya Toyota IST nyeusi na wanapelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo ndugu hao walianza kuwafuatilia, ikiwamo kuzunguka kwenye vituo vingine vya polisi bila mafanikio, ndipo walianza kuzungukia kwenye hospitali mbalimbali katika vyumba vya kuhifadhia maiti, hata hivyo hawajawapata ndugu zao.

Mwananchi lilipomtafuta Kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro juu ya tukio hilo alikiri kupata taarifa hizo na kwamba wanaendelea kuchunguza na kuwatafuta.

“Hao watu walishafika na stori hizo nilishazisikia, waliniambia walikuwa watano, si kwamba kila anayepotea anakuwa amechukuliwa na Polisi na si kila anayepotea anakuwa amekufa, mara ngapi watoto wanapotea na baadaye wanaonekana? Kwa hiyo mtu akipotea utulivu unahitajika,” alisema.

“Nilipokuwa Mkoa wa Shinyanga na Mwanza kila siku watu walikuwa wanapotea, kumbe walikuwa wanakwenda zao machimbo na wanakaa miezi sita baada ya kudanganywa kule kuna madini na anaji off kwenye simu mnamkuta baada ya miaka minne mitano. Sisi Polisi tukiwakamata watu tunatangaza, sasa huwezi uwang’ang’ania,” alisema.

Wakizungumza Dar es Salaam jana na gazeti hili, baadhi ya wazazi na ndugu waliopotelewa, Sylvia Quentin, Omary Mohamed na Longili Martin walisema vijana wao waliokuwa wanajihusisha na biashara ya kuuza simu kwa rejareja Kariakoo Mtaa wa Agrey walipotea wakiwa njiani kuelekea ufukweni Kigamboni kusherehekea Sikukuu ya Krismasi.

“Tumepitia vituo vya polisi, hospitali na hata vyumba vya kuhifadhia maiti lakini bado hatujabahitika,” alisema Longili Martin, aliyepotelewa na mtoto wake Kunambi.

Martin, mkazi wa Gongolamboto alieleza kuwa mara ya mwisho aliwasiliana na Edwin Desemba 23 alipomkaribisha kwenda kusherehekea Krismasi pamoja, lakini alimweleza kuwa atakuwa na shughuli nyingi na kuahidi kujumuika nao kwenye sikukuu ya mwaka mpya.

Taabu Saidi aliliambia Mwananchi jana kuwa Desemba 26 mwanawe, Rajabu Mdoe alikwenda nyumbani kwake Kinyerezi, aliomba gari ili aende ufukweni Kigamboni na marafiki zake ambao hadi leo hawajaonekana.


“Nakumbuka ilikuwa majira ya saa 2 usiku, alipofika na kuchukua gari, ilipofika saa sita usiku niliamua kumpigia lakini simu yake ilipokelewa. Haikunisumbua, kwa sababu nilijua atarudi lakini nilitilia shaka alipokuwa hivyo hadi asubuhi,” alisema.


Alisema hata hivyo alijaribu kupiga simu yake asubuhi na haikupatikana:kwamba siku mbili baadaye marafiki wawili walifika kwake na kumtaarifu kwamba alikamatwa na polisi walipokuwa wanaenda ufukweni.