Prime
CUF hakujapoa, wachambuzi waja na suluhisho
Muktasari:
- Miezi michache baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kuondolewa uenyekiti na Mirambo Yusuf kurithi nafasi hiyo, CUF bado inakabiliwa na misuguano ya uongozi inayotia shaka uwezo wa chama kurejesha umoja na nguvu kama awali.
Dar es Salaam. Utulivu wa ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umeendelea kuwa changamoto, miezi minne baada ya kung’oka kiongozi wa muda mrefu, Profesa Ibrahim Lipumba.
Hii ni baada ya makada zaidi ya 70 wa chama hicho, kutinga katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupinga uchaguzi wa ndani uliofanyika Februari 21, 2026 ubatilishwe na kuitishwa upya.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miezi michache tangu Mwenyekiti mpya wa CUF, Mirambo Yusuf achaguliwe katika uchaguzo ambao pia ulikuwa wa marudio baada ya ule wa kwanza kubatilishwa, na kuahidi kufungua ukurasa mpya wa maridhiano na umoja ndani ya chama.
Makada hao wakiongozwa na Othman Dunga, wamewasilisha barua mbili kwa Msajili wakidai uchaguzi huo ulikiuka Katiba ya chama, kwa sababu baadhi ya wajumbe walioshiriki kupiga kura hawakuwa na sifa za kufanya hivyo.
Akizungumza mbele ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Juni 25, Dunga alisema uchaguzi huo haukufuata utaratibu wa Katiba ya CUF.
"Uchaguzi uliofanyika Februari 21 mwaka huu haukuzingatia misingi ya Katiba ya chama chetu. Hatujui uliitishwa na nani, na hata mchakato wa kuwapata viongozi ulienda kinyume na Katiba yetu. Ndiyo maana tumewasilisha maombi ya kufutwa kwa uchaguzi huo na kuitishwa mwingine," alisema.
Malalamiko hayo yalipokelewa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, ambaye alisema ofisi yake itayafanyia kazi kwa kusikiliza pande zote kabla ya kutoa uamuzi.
Hatua hiyo inaashiria kuwa CUF bado haijafanikiwa kuondokana na migawanyiko ya muda mrefu.
Desemba 18 na 19, 2024, CUF ilifanya mkutano mkuu uliompa ushindi Profesa Lipumba kuendelea kukalia kiti lakini liibuka kundi la wananchama likalalamika kuwa haukukidhi matakwa ya Katiba inayoelekeza mshindi wa uenyekiti sharti apate zaidi ya nusu ya kura za wajumbe wa mkutano huo.
Februari 13, 2026, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ilibatilisha uchaguzi huo.
Februari 21, 2026, uchaguzi wa marudio ulifanyika. Lakini Profesa Lipumba hakuchukua fomu ya kuomba kuchaguliwa tena.
Mgogoro mingine
Mwaka 2015 kipindi cha uchaguzi mkuu, Profesa Lipumba alijiuzulu aliyekuwa uenyekiti wa chama hicho na baadaye kurejea baada yam waka mmoja kwa nguvu, hatua iliyopingwa na kundi la aliyekuwa Katibu Mkuu, hayati Maalim Seif Sharif Hamad.
Mvutano huo ulisababisha viongozi na wanachama wengi kuhama na kujiunga na ACT-Wazalendo, hali iliyoathiri nguvu ya CUF katika siasa za upinzani nchini.
Profesa Lipumba aliendelea na uongozi hadi alipokabidhi ofisi Machi 29, 2026 kwa mwenyekiti mpya Mirambo Yusuf.
Hata hivyo, licha uongozi mpya kuahidi utulivu na mshikamano ndani ya chama, malalamiko mapya yameanza kujitokeza, jambo linaloonyesha kuwa changamoto kubwa inayokikabili chama hicho si tu mabadiliko ya viongozi, bali pia ujenzi wa maridhiano ya kudumu muda mrefu.
Hali hiyop inaelezwa na wachambuzi kuwa bila kutatua migogoro ya ndani, CUF inaweza kuendelea kupoteza ushawishi wake katika siasa za upinzani nchini.
Mchambuzi wa siasa, Hamduny Marcel amesema migogoro mingi ndani ya vyama vya siasa huanzia pale viongozi wanapounda makundi yanayoanza kushindana.
"Mara nyingi makundi ndani ya chama yanapoanza kugongana huzalisha migogoro. Pia namna viongozi wapya wanavyoshughulikia makundi yaliyokuwapo na tafsiri tofauti za wanachama kuhusu maamuzi ya chama, huchochea migogoro hiyo," amesema.
Amesema suluhisho ni viongozi kujenga utamaduni wa kumaliza tofauti zao ndani ya chama badala ya kuziacha zifikie hadharani na kudhoofisha taasisi.
Kwa upande wake, mwanahabari mkongwe nchini, Jesse Kwayu amesema migogoro ya CUF inafanana na ile iliyowahi kuvikumba baadhi ya vyama vya upinzani kama United Democratic Party (UDP), Tanzania Labour Party (TLP) na NCCR-Mageuzi.
Amesema migogoro mingi katika vyama hivyo ilitokana na tofauti za watu binafsi kuliko misingi ya itikadi.
"Vyama vyetu vingi vimeondoka katika siasa za itikadi na kubaki kwenye siasa za watu binafsi. Hapo ndipo migogoro huanzia. CUF inapitia changamoto kama zilizowahi kuzikumba UDP, TLP na NCCR-Mageuzi," amesema mwanahabari huyo.
Kwayu ameongeza kuwa CUF kinapaswa kujiuliza nani anayenufaika na migogoro hiyo na kwa nini migogoro hiyo imeendelea kujirudia, akisema majibu ya maswali hayo yanaweza kuwa sehemu ya suluhisho la kudumu kwa chama hicho.
Kwa upande wake, wakili na mchambuzi wa siasa, Aloyce Komba anasema tatizo linalokikabili CUF ni utamaduni wa vyama vya siasa kubebwa na majina ya watu badala ya ushawishi wa sera na itikadi.
Anasema vyama vingi vinaendeshwa kwa nguvu ya watu badala ya ushawishi wa sera na itikadi zake.
"Vyama vingine vinakuwa vyama dola, vinalindwa na dola. Siku kikiondoka madarakani tu, kinapotea. Chadema nayo ilikuwa hivyo, lakini tunawaona angalau wanajaribu kuifanya iguswe na watu. Hii CUF iliondoka na Maalim Seif. Suluhisho la haya ni kuondoa vyama kwenye majina ya watu na kuvijenga kupitia ushawishi wa sera na itikadi," amesema, huku akigusia pia umuhimu wa kurekebisha misingi ya Katiba ili kulinda vyama vya siasa dhidi ya kuingiliwa na mamlaka nyingine.