Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makada 73 CUF watinga kwa msajili kutaka Mirambo ang'olewe, Msajili awajibu

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza aliyevaa suti nyeusi akiwaongoza makada wa Chama cha Wananchi CUF, kwenda ofisini kwake.

Muktasari:

  • Wanachama hao wanaitaka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliomweka madarakani Mwenyekiti wa chama hicho, Yusuf Mirambo na wenzake.

Dar es Salaam. Makada 73 wa Chama cha Wananchi (CUF) wameandamana hadi Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kushinikiza kupatiwa majibu ya barua yao ya malalamiko, wakitaka kubatilishwa kwa uchaguzi mkuu wa chama uliomweka madarakani Mwenyekiti mpya, Yusuf Mirambo na wenzake.

Maandamano hayo yaliongozwa na Othman Dunga, ambaye alikuwa mshindani mkuu wa Mirambo katika uchaguzi uliofanyika Februari 22, 2026.

Makada hao waliwasilisha barua mbili za malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakitaka uchaguzi huo ufutwe kwa madai kuwa ulikiuka taratibu za katiba ya chama, ikiwemo kushiriki kwa baadhi ya wajumbe waliodaiwa kutokuwa halali kupiga kura.

Wanachama hao wanaitaka Ofisi ya Msajili kufuta matokeo ya uchaguzi huo na kuagiza kufanyika kwa uchaguzi mwingine utakaosimamiwa kwa kuzingatia katiba ya chama ili viongozi wapya wachaguliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.

Makada hao, waliobeba ujumbe wa kuomba mrejesho wa malalamiko yao, waliwasili katika Ofisi za Msajili wa Vyama vya Siasa zilizopo Posta, Dar es Salaam, leo Alhamisi, Juni 25, 2026 na kupokewa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza.

Awali, kabla ya kuwapokea, Nyahoza ameeleza kushangazwa na idadi kubwa ya makada hao kufika ofisini hapo bila taarifa rasmi na kufanya maandamano bila kibali cha Jeshi la Polisi, jambo alilodai kuwa ni kinyume cha sheria.

“Kwa kuwa mmefika hapa, na hii ni nyumba ya demokrasia, karibuni. Hata hivyo, msirudie kufanya hivyo tena. Kama lengo lilikuwa kufuatilia mrejesho wa barua yenu, hata mtu mmoja angeweza kufika na kuwakilisha wengine badala ya kuja kwa idadi kubwa kiasi hiki na kusababisha taharuki,” amesema Nyahoza.

Baada ya majibizano ya takribani dakika 10, Nyahoza aliwataka makada hao kuchagua wawakilishi wasiozidi 10 kuingia ofisini kwake, huku wengine wakibaki nje kutokana na udogo wa nafasi ya ofisi hiyo, wakati wote huo, makada hao walikuwa wakiimba nyimbo za chama chao.

Ndani ya ofisi hiyo, Othman Dunga, ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Bara katika uongozi uliovunjwa wa Profesa Ibrahim Lipumba, alipewa nafasi ya kuzungumza kwa niaba ya wenzake.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza akizungumza na makada wa Chama cha Wananchi CUF.

Katika maelezo yake, Dunga amesema kuchelewa kwa majibu ya malalamiko yao kunawaweka wanachama wa chama hicho katika hali ya sintofahamu.

“Uchaguzi uliofanyika Februari 22 mwaka huu haukuzingatia misingi ya Katiba ya chama chetu. Hatujui uliitishwa na nani, na hata mchakato wa kuwapata viongozi uliokiuka Katiba yetu. Ndiyo maana tuliwasilisha barua ya kuomba uchaguzi huo ufutwe na kuitishwa mwingine,” amesema Dunga.

Kwa mujibu wake malalamiko yao yamekuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu bila majibu, hali inayochochea migogoro ndani ya chama na kuzua hisia kuwa kuna upendeleo katika namna suala hilo linavyoshughulikiwa.

“Baada ya kuona hali hiyo, na baadhi yetu kuonekana kama tunatumika na makundi fulani, tuliamua kuandamana kufika hapa kuomba mrejesho wa malalamiko yetu. Tumechoka kusubiri; tunahitaji uongozi uliochaguliwa kwa ridhaa ya wanachama,” amesema.

Baada ya kupokea barua hiyo, Nyahoza aliwahakikishia kuwa ofisi yake itafanyia kazi malalamiko hayo na kutoa majibu baada ya kusikiliza pande zote husika.

“Mnapowasilisha malalamiko, huwa tunasikiliza pande zote kabla ya kutoa uamuzi. Leo mmefika nyinyi, lakini jana kada mwenzenu Romanus Mapunda naye alifika kuulizia suala hilohilo. Tulimsihi kuwa na subira, na ndivyo tunavyowaomba nanyi muendelee kuwa na imani na ofisi hii,” amesema Nyahoza.

Juni 23, 2026, Mwenyekiti wa CUF, Yusuf Mirambo, aliliambia gazeti hili kuwa tayari walishapokea nakala za malalamiko hayo kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kuyajibu ndani ya muda uliowekwa.

“Malalamiko yote tuliyajibu na kuyawasilisha kwa Msajili. Wanaolalamika wafuatilie ofisi hiyo kwa mrejesho. Kwa upande wetu, hoja zote zilijibiwa kikamilifu, na kama mwenyekiti nilijiridhisha kuwa majibu yote yalitumwa kwa wakati,” alisema Mirambo.


Walivyofika Ofisini kwa Msajili

Makada hao 73 waliwasili katika Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa majira ya saa 4:43 asubuhi wakiwa ndani ya daladala mbili walizokodi kutoka Magomeni, jijini Dar es Salaam.

Wakiwa safarini kuelekea Posta, walikuwa wakiimba nyimbo za chama na kuhamasishana kwa kauli za kutaka kuitishwa uchaguzi mwingine ili wapate viongozi wanaowaamini na wanaodai wamechaguliwa kwa mujibu wa katiba ya chama, tofauti na hali ilivyo sasa.