Dk Tulia: Utekelezaji wa ilani ni taswira ya uchaguzi ujao
Mbunge Mbeya Mjini ,Dk Tulia Ackson akizungumza na wafuasi wa chama cha Mapinduzi (CCM) wakiwepo Wajumbe wa nyumba kumi, Wenyeviti wa Serikali za mitaa na Madiwani jijini Mbeya.
Muktasari:
- Dk Tulia awataka viongozi ngazi ya kata na vijiji kuwaeleza wananchi mniradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Mbeya. Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema ushindi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) utategemea na utekelezaji wa ilani ya chama hicho ya mwaka 2020, huku akiwasihi wanaohusika kutozembea katika utekelezaji wa ilani hiyo.
Dk Tulia ambaye ni Mbunge wa Mbeya mjini na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ameyasema hayo leo Jumamosi Desemba 23,2023 wakati akizunguza na viongozi wa ngazi za kata ndani ya CCM wakiwepo madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wa nyumba kumi.
“Madiwani na wenyeviti mjitafakari kuhusiana na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi yam waka 2020 sasa tunakwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa nendeni kwa wananchi mkaeleze yale ambayo yamefanywa msije kuleta ugumu wa kuanza kuvutana mashati kwani hakuna atakayekubali hilo”,amesema.
Dk Tulia amewataka viongozi hao wakazungumze na wananchi kwani zipo kero ndogondogo ambazo zinatatulika.
“Kaitisheni mikutano ya wananchi kwani mpo baadhi ya wenyeviti mna visasi na na kuitisha mikutano ya kusemana ,hilo sio lengo la CCM kukuweka hapo hali hiyo inasababisha wananchi kutengeneza chuki dhidi ya Serikali na kuwepo kwa mazingira magumu ya kukubalika katika kipindi kingine cha uchaguzi,”amesema.
Wakati huo huo amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo wa maji kutoka mto kiwira, barabara njia nne kutoka Uyole mpaka Uwanja wa Ndege wa Songwe (SIA) na ujenzi wa vituo vya afya pamoja na zahanati.
“Leo ni siku ya pili nafanya vikao na viongozi ndani ya chama tufike wakati tubadilike twende tutatue kero za wananchi na kumsemea Rais Samia Suluhu Hassan anayoleta katika Jimbo la Mbeya mjini ”amesema.
Dk Tulia amesema kupitia mfuko wa jimbo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Mbeya wameweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo katika shule 83 za msingi jijini hapa.
Kwa upande wake Diwani viti maalum Kata ya Isanga na mjumbe wa mkutano mkuu ,Atupele Msai amesema wamepokea maagizo ya Spika wa Bunge ya kwenda kwa wananchi kueleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyoelekezwa na Serikali ya awamu ya sita.
“Tumesikia maelekezo sasa tunaelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na Mkuu Oktoba 2025 tunatakiwa kurejea kwa wananchi kuwaelekeza nini Serikali imefanya hususan katika sekta ya elimu, afya, barabara na miundombinu ya maji,”amesema.
Naye Mjumbe wa nyumba kumi, Grace Mapunda amesema wanakwenda kuitisha mkutano ya hadhara ya wananchi na kueleza mambo yaliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan.