Hashim Rungwe achukua fomu, Dk Magufuli leo

Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Adam Nyandu (kushoto) akimkabidhi mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe fomu za kugombea urais, Dar es Salaam jana. Kulia ni mgombea mwenza, Issa Abbas Hussen. Picha na Said Khamis

Muktasari:

Mgombea huyo anakuwa wa tatu kuchukua fomu za kugombea urais akitanguliwa na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila na Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe amewataka Watanzania kuchagua wabunge wengi kutoka vyama vya upinzani ili kuleta mabadiliko ya kweli na umakini katika uamuzi wa masuala ya msingi.

Rungwe alisema hayo jana baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kwamba hiyo itasaidia kuepuka majibu mepesi katika maswali magumu.

Mgombea huyo anakuwa wa tatu kuchukua fomu za kugombea urais akitanguliwa na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila na Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa.

Mgombea wa nne atakuwa ni Dk John Magufuli wa CCM ambaye anatarajiwa kuchukua fomu leo.

Rungwe aliingia katika ofisi hizo bila mbwembwe nyingi akiwa katika gari jeusi aina ya Mercedes Benz likifuatiwa na gari jeupe aina ya Toyota Noah lililopambwa kwa bendera nyingi za chama hicho likiwa na watu wasiozidi watano.

Baada ya kuchukua fomu, Rungwe alisema kilichomsukuma kuwania nafasi hiyo kubwa katika uongozi wa nchi ni kuwahamisha Watanzania walipokuwa baada ya uhuru kwa kuwaondolea hofu ya maisha.

Alisema Watanzania wengi wana hofu ya maisha, hakuna mwenye uhakika kutokana na kutokuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato ikiwamo ukosefu wa ajira huku wakiishi kwa kukamuliwa kila kukicha.

Alisema hataki kuahidi kutoa ajira bila kutaja zitakapotoka, bali Watanzania wataajiriwa kutokana na rasilimali zao, viwanda vyao, huku fedha zao za kodi zikitumika kuwaletea maendeleo.

Alisema hayo yatawezekana iwapo tu Watanzania wataamua kuweka watu makini katika nafasi za ubunge ambao si wengine, bali kutoka vyama vya upinzani watakaokuwa wakifanya uamuzi makini wenye kulinda haki na rasilimali zilizopo.

Aliwataka wanaowania urais kutambua kuwa Watanzania wana matatizo mengi yanayotakiwa kupatiwa ufumbuzi badala ya kukimbilia Ikulu kwa kudhani ni sehemu ya matanuzi.

“Kuna baadhi ya vijiji nimewahi kupita kuna mambo ya ajabu kuna watu hadi karne hii hawana nguo za kujisitiri, namaanisha kujisitiri, siyo kuvaa wapendeze na katika maeneo hayo kuna viongozi wakiwamo wabunge, wametawala kwa miaka kadhaa hakuna walichowafanyia, mkakati mkuu ni kuwatoa huko kwa mali zao wenyewe,” alisema Rungwe.

“Wanaong’ang’ania kwenda Ikulu wakidhani ni sehemu ya kufanyia matanuzi wanakosea kwani kuna mambo mengi yanatakiwa kufanyiwa kazi, jamani Ikulu siyo sehemu ya kujirusha ni kazi, ni kuwatumikia wananchi, maana wao ndiyo marefa wanaamua nani anacheza kikosi cha kwanza nani hachezi na wakikutoa mchezoni usikasirike.”

Alisema mchakato wa kumpitisha kuwania nafasi hiyo ulifanyika Aprili 4 akiwashinda wenzake wawili akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, Ally Omary Juma kutoka Zanzibar.

Alisema baada ya kupitishwa, alimchagua Issa Abbas Hussein kuwa mgombea mwenza na Mohamed Masoud Rashidi alichaguliwa kuwa mgombea urais Zanzibar.

Kwa upande wake, Hussein alisema ajira ndiyo changamoto kuu na chama chake kitaanza nayo ili kila Mtanzania afurahie maisha.

Alisema ajira hazitoki nje ya nchi, bali humuhumu nchini kwa kuboresha rasilimali zilizopo, kuzitunza na kuzikabidhi kwa wananchi wenyewe ili ziwasaidie.

Dk Magufuli kuchukua leo

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema Dk Magufuli atachukua fomu leo saa sita mchana akisindikizwa na viongozi waandamizi wa CCM, akiwamo Makamu Mwenyekiti, Philip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.

Alisema msafara wa Dk Magufuli kwenda NEC utaanzia Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba saa tano asubuhi na kupitia Barabara za Bibi Titi Mohammed, Morogoro na Ohio na kurudi kupitia njia hizohizo.

“Baada ya kuchukua fomu za kuwania urais, Dk Magufuli atarejea hapa Lumumba, kisha atazungumza na wananchi na kutoa neno la shukrani,” alisema Nape.