Prime
Hii hapa timu ya kuchora ramani ya katiba mpya Chadema
Muktasari:
- Kamati hiyo iliyopewa hadidu rejea nne na muda wa miezi mitatu kutekeleza jukumu hilo, inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala, ambaye ni Mwenyekiti wake, huku Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la (Bavicha), Wakili Deogratius Mahinyila, akiwa katibu wa kamati hiyo.
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza wajumbe 11 wanaounda kamati maalumu ya Kamati Kuu yenye lengo la kukwamua na kuendeleza mchakato wa kukusanya maoni ya upatikanaji wa katiba mpya, kabla ya mwaka 2027 ili kuchochea ustawi wa wananchi.
Kamati hiyo iliyopewa hadidu za rejea nne na muda wa miezi mitatu kutekeleza jukumu hilo, inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala, ambaye ni Mwenyekiti wake huku Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), Wakili Deogratius Mahinyila, akiwa katibu wa kamati hiyo.
Wajumbe wengine ni Wakili Ali Ibrahim, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa (Bazecha) Suzan Lyimo, Ruthy Moleli, Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Pamela Maasay, Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho, Wakili Gaston Garubindi, Zeud Mbano, Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, maarufu Boni Yai, pamoja na washauri wawili ambao si wanachama wa chama hicho, Wakili Mpale Mpoki na Wakili Jeremia Ntobesia.
Kamati hiyo imeundwa kufuatia utekelezaji wa maamuzi na maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema iliyokutana Aprili 28 na 29, 2026 katika makao makuu ya chama hicho, ambapo iliazimia kuanza mchakato wa kuharakisha upatikanaji wa katiba mpya kutokana na umuhimu wake kwa wananchi.
Akizungumza Dar es Salaam leo Jumatano, Juni 17,2026 na waandishi wa habari, Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema kamati hiyo imepewa siku 90 za kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia hadidu za rejea nne, ikiwemo kuandaa mkakati wa kukwamua mchakato wa katiba mpya.
Katibu Mkuu Chadema, John Mnyika akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Juni 17, 2026 jijini Dar es Salaam.
“Hadidu rejea ya pili ni kuandaa rasimu ya muswada wa sheria kwa niaba ya wananchi utakaoelekeza namna ya kukwamua mchakato wa huo.
"Ya tatu ni kuandaa mapendekezo kuhusu muundo wa chombo huru kitakachosimamia kura ya maoni ya katiba mpya. Ya nne ni kuhakikisha mapendekezo yote yanazingatia lengo la kuanza kwa mchakato huo mapema na kukamilika kabla ya mwaka 2027,” amesema Mnyika.
Amesema baada ya kuteuliwa, kamati hiyo ilianza kazi na sasa imetangazwa rasmi ili iweze kuendelea na shughuli zake kwa uwazi. Pamoja na kuwa ni kamati ya Kamati Kuu ya Chadema suala la katiba mpya ni la kitaifa, hivyo itashirikisha wadau mbalimbali nchini.
“Kamati itakutana na asasi za kiraia, taasisi za dini, wasomi, sekta ya habari, wachumi, wadau wa kisiasa, wataalamu wa sayansi na teknolojia pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii ili kuhakikisha nchi inapata katiba mpya,” amesema.
Mnyika amesema ndani ya kipindi hicho cha siku 90, kamati itawasilisha taarifa ya awali ndani ya wiki mbili kwa Kamati Kuu ya chama hicho, ambayo itatoa maelekezo endapo itabaini mapungufu yoyote.
“Natoa rai kwa Watanzania na wadau wa katiba mpya kuipa ushirikiano kamati hii ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa wakati na kuwasilisha mapendekezo ndani ya muda wa miezi mitatu waliyopewa,” amesema.
Amesema kazi za kamati hiyo hazitaathiri shughuli nyingine za chama, ikiwemo Operesheni Free Tundu Lissu na Katiba Mpya inayoendelea katika mikoa mbalimbali nchini.
“Kamati hii inaenda kufanya kazi ya kiufundi kwa kuzingatia hadidu rejea hizi nne. Katiba Mpya ni kipaumbele cha taifa, hivyo mchakato wake lazima uende kwa kasi ili kukidhi matarajio ya Watanzania,” amesema.
Mnyika amesema kuwa katika kutekeleza jukumu lake, kamati hiyo haitahusisha Serikali katika ukusanyaji wa maoni kuhusu namna ya kukwamua mchakato huo kwa kuwa Chadema haitambui Serikali iliyopo.
Amesema Watanzania wanahitaji katiba itakayoweka mfumo bora wa uongozi, utawala, uwajibikaji na haki, pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
“Tunasikitika kwamba suala la Katiba Mpya halijajumuishwa katika Bajeti Kuu ya Serikali wala katika mjadala wa Bunge unaoendelea. Kutokana na hali hiyo, Chadema imeamua kuchukua hatua za kukwamua mchakato huu,” amesema.
Chanzo cha kugharamia mchakato
Mnyika amesema fedha za kugharamia shughuli za kamati hiyo zitatokana na michango ya wananchi kupitia kampeni za Tone Tone na Chadema Digital.
“Napenda kutumia fursa hii kuwaomba wananchi waendelee kuichangia Chadema. Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, chama kilikuwa kinapata ruzuku ya takribani Sh107 milioni kwa mwezi, lakini kwa sasa hakipati ruzuku hiyo,” amesema.
Ameonya endapo wananchi hawatachangia, kuna hatari ya mchakato huo kukwama kutokana na ukosefu wa vyanzo vingine vya uhakika vya mapato.
“Tunawaomba Watanzania wanaotaka Katiba Mpya wachangie Operesheni Free Tundu Lissu, wachangie kazi ya kamati hii na shughuli za Chadema kwa ujumla,” amesema.
Ametaja chanzo kingine kuwa ni michango kutoka kwa asasi za kiraia kupitia ushirikiano katika shughuli mbalimbali zitakazofanywa na kamati hiyo.
“Pia nimewaeleza wajumbe wa kamati kuhusu changamoto ya rasilimali tulizonazo na kuwaomba wajitolee kwa uzalendo mkubwa kutokana na umuhimu wa kazi hii kwa Taifa. Tunawahakikishia Watanzania kwamba jukumu hili litatekelezwa kwa uwezo wote uliopo,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Rugemeleza Nshala, amesema amelipokea jukumu hilo kwa moyo wa dhati na yuko tayari kuhakikisha mchakato huo unasonga mbele kwa kuondoa vikwazo vilivyowahi kuukwamisha hapo awali.
“Jukumu hili ni heshima kubwa kwangu na kwa wajumbe wenzangu. katiba imekuwa kilio cha Watanzania kwa muda mrefu kiasi kwamba baadhi yao wameanza kukata tamaa. Tutafanya kazi kwa uzalendo mkubwa, tukishirikiana na wadau wote ili kuhakikisha wananchi wanapata katiba wanayoihitaji,” amesema Dk Nshala.