Hoja ya Dk Slaa ina mambo matatu ya kujadili
Muktasari:
Balozi Willibrod Slaa ametoa kauli kuhusu Rais Samia Suluhu Hassan, kuruhusu mikutano ya hadhara. Kupitia kauli hiyo inarahisisha kuiona kauli ya sura ya tatu ya Balozi huyo.
Balozi Willibrod Slaa ametoa kauli kuhusu Rais Samia Suluhu Hassan, kuruhusu mikutano ya hadhara. Kupitia kauli hiyo inarahisisha kuiona kauli ya sura ya tatu ya Balozi huyo.
Slaa ni daktari ya falsafa (PhD) wa Thiolojia, amemkosoa Rais Samia kwa mambo mawili. Mosi kuruhusu mikutano ya hadhara ya kisiasa, pili ushauri au mwongozo wa Rais Samia kuwa majukwaa ya kisiasa yasitumike kutukanana.
Mosi, Dk Slaa alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden kipindi cha uongozi wa Serikali ya Tano ya Dk John Magufuli. Alisema Rais Samia amefanya makosa kutoa kauli ya kuruhusu mikutano ya hadhara ya kisiasa.
Hoja ya Dk Slaa ni kuwa hakujawahi kuwa na katazo la mikutano ya hadhara, hivyo Rais Samia ameingia mkenge kutoa kauli ya kuiruhusu. Hapohapo kwa unyenyekevu anamsahihisha Rais, vilevile anawalaumu wanasheria wanaomshauri.
Katika hili la ama kuwepo au kutokuwepo kwa katazo la mikutano ya hadhara ya kisiasa, Dk Slaa ana hoja. Utafahamu usahihi au makosa yake baada ya kuijua hoja yake na kuitendea haki kiuchambuzi.
Pili, Dk Slaa amemkosoa Rais Samia kuwa kauli yake ya kutaka wanasiasa watumie lugha ya staha kufanya siasa majukwaani ni mbaya na uhatari wake unaweza kushabihiana na katazo la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa.
Hoja ya Dk Slaa ni kwamba kauli ya Rais inaweza kuleta mkanganyiko kuhusu tafsiri ya matusi na lugha ya staha. Polisi wanaweza kushusha wanasiasa jukwaani kulingana na tafsiri .
Hoja ya kwanza
Tunapomjadili Dk Slaa tusisahau kuwa ni Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vilevile alipata kuwa Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, kati ya mwaka 2005 na 2010.
Kwa kumwelewa Dk Slaa, aliposema hakujawahi kuwa na katazo la mikutano ya hadhara ya kisiasa, anatetea hoja yake kwamba kitu chochote kilichojengewa uhalali wa kikatiba na kisheria, hakiwezi kuzuiwa na tamko la kiongozi yeyote.
Dk Magufuli, akiwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2016, alitoa katazo la mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano ya amani. Alisema mikutano ingefanyika mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Ukiielewa kwa undani kabisa kauli ya Dk Slaa, zuio la Magufuli halikuwa halali, kwa maana hiyo makosa yalikuwa kwa vyama vya siasa vyenyewe kuishi ndani ya katazo, kisha kusubiri kuruhusiwa.
Hali halisi
Je, wanasiasa, hasa walio upande wa upinzani hawakujua kuwa katazo la mikutano ya hadhara ya kisiasa lilikuwa batili? Jawabu ni kwamba walifahamu ndio maana walijitahidi kupinga bila mafanikio.
Ukimwelewa Dk Slaa, ni kama anawaambia wanasiasa kuwa hawakupaswa kutulia na kusubiri ruhusa kwenye jambo ambalo ni halali kwao kulitenda kikatiba. Swali je, wapinzani walitulia?
Jibu ni kuwa hawakutulia. Tangu mwaka 2016 lilipotoka katazo la mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima hadi Uchaguzi Mkuu 2020, zilifanyika harakati kadhaa ambazo majibu ya upande wa pili yalitishia amani ya nchi.
Julai 27, 2016, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza kuanza kwa oparesheni ya mikutano na maandamano ya amani chini ya jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta). Mbowe alisema walitangaza hivyo kwa sababu nchi ilikuwa na viashiria vingi vya kuingia kwenye udikteta.
Ukuta ulianza Julai 27, 2016, kilele chake ambacho ndio siku ya kutoka barabarani rasmi, ilipangwa kuwa Septemba Mosi, 2016. Kadiri Septemba Mosi ilivyokuwa inakaribia, mambo mengi yenye kuogofya yalichukua nafasi.
Dk Magufuli alisema “wasimjaribu”, kisha akataka viongozi ndiyo wawe mstari wa mbele waone ambacho kingewapata.
Jeshi la polisi lilionya Ukuta, kisha video mfululizo zilifuata kuonesha askari polisi wakifanya mazoezi ya utayari.
Hali ilikuwa mbaya zaidi, baada ya Jeshi la Wananchi (JWTZ) nalo kutangaza maadhimisho yao Septemba Mosi. Kisha, askari wa JWTZ nao wakaanza kurusha video kuonyesha walivyokuwa wakijiweka sawa.
Tangazo la JWTZ lilieleza pia matumizi ya barabara ambazo wangezitumia. Kwa tafsiri ni kwamba Jeshi la Wananchi lilikuwa linawajulisha wanasiasa waliopanga kutekeleza kilele cha Ukuta Septemba Mosi kuwa siku hiyo wangekutana na askari wa JWTZ barabarani.
Kutokana na hali ilivyokuwa ushauri ulitoka kwenye makundi mbalimbali kumnasihi Mbowe kuahirisha Ukuta. Walikuwepo viongozi wa dini mpaka wazee na makundi mbalimbali yaliyoitakia mema nchi.
Waliotoa ushauri walikuwa wameshaona hatari endapo oparesheni Ukuta ingetekelezwa, kisha kukutana na Polisi waliotangaza kujiandaa kuwakabili wanasiasa, vilevile JWTZ waliodai kufanya maadhimisho yao barabarani.
Agosti 31, 2016, Mbowe alitangaza kuahirisha kwa mwezi mmoja kilele cha oparesheni Ukuta. Alisema kama chama na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walifikia uamuzi huo ili kutoa fursa kwa viongozi wa dini kukutana na Rais Magufuli, kuzungumza hali ya kisiasa.
Kwa mantiki hiyo, viongozi wa dini waliona dalili mbaya za kuvunjika kwa amani. Waliingilia kati. Walishauri Chadema na Ukawa waahirishe, kisha wao wakutane na Rais Magufuli, lengo likiwa kutafuta ufumbuzi.
Hakuna ufumbuzi ulipatikana. Hali iliendelea hivyo. Wabunge na madiwani waliruhusiwa kufanya mikutano kwenye maeneo yao lakini vibali vilikuwa havitolewi. Mikutano ya wabunge iliahirishwa kila mara. Hoja ikiwa “sababu za kiintelijensia”.
Februari 16, 2018, viongozi wa ngazi za juu Chadema, wakiongozwa na Mbowe, walifanya maandamano kutoka Makumbusho, Kijitonyama, kuelekea Magomeni, palipo na Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Kinondoni. Tukio hilo lilisababisha mauaji.
Chadema walilalamikia mawakala wao kucheleweshewa barua za utambulisho na hati za viapo, kuelekea uchaguzi mdogo wa ubunge, jimbo la Kinondoni. Aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia, alijiuzulu na kuhama chama kutoka CUF kwenda CCM, akidai anaunga mkono juhudi za Rais Magufuli.
Kisha, Mtulia akawa mgombea ubunge wa CCM, uchaguzi mdogo. Chadema waligombea kupitia Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar. Sasa ikiwa siku moja kabla ya uchaguzi, Chadema waliona wanahujumiwa. Walifanya maandamano.
Polisi walitumia risasi za moto kutawanya maandamano. Aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Akwilina Akwilini, alipigwa risasi akiwa ndani ya daladala, akapoteza maisha. Wafuasi wengi wa Chadema waliwekwa mahabusu wakiwa na majeraha ya risasi.
Machi 2020, viongozi wa juu wa Chadema, walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au faini ya jumla, Sh350 milioni. Wito wa michango ulitoka nchi nzima, fedha zilipatikana na viongozi waliachiwa baada ya kukamilisha malipo ya faini.
Tumjibu Dk Slaa
Ni kweli Dk Slaa yupo sahihi kusema katazo la mikutano lilikuwa batili kuanzia siku ilipotoka. Hata hivyo, mazingira yameonyesha kuwa kulikuwa na jitihada pamoja na harakati nyingi lakini matokeo yalikuwa mabaya.
Kama wito wa mikutano na maandamano ya amani kupitia Ukuta, uliyaamsha majeshi ya Polisi na JWTZ, Dk Slaa hakosei kusema katazo halikuwepo, ila anachopaswa kutambua ni kwamba aliyekataza kimakosa alikuwa na mamlaka makubwa hata ya kutumia jeshi kudhibiti.
Dk Slaa azingatie kuwa kama Chadema waliandamana, wakapigwa risasi na haikuwa kitu. Mwanafunzi Akwilina aliuawa kwa risasi, viongozi wa Chadema ambao hawakuwa na bunduki, ndio wakabebeshwa tuhuma.
Dk Slaa anasema maandamano ni haki ya kikatiba na hakuna katazo. Hapohapo anafahamu kuwa Mbowe na viongozi wa juu wa Chadema walishtakiwa na kuhukumiwa jela au kulipa Sh350 milioni.
Kama Mahakama ambacho ndicho chombo cha kutafsiri Katiba na sheria za nchi, kilipokea mashtaka dhidi ya viongozi wa Chadema na kuwatia hatiani kwa kuandamana pasipo kibali na kusabisha kifo cha Akwilina, je, bado unaweza kusema katazo halikuwepo na halikupaswa kutenguliwa.
Ikiwa wafuasi wa Chadema waliwekwa mahabusu wakiwa na majeraha ya risasi. Hawakupewa matibabu kwa wakati na polisi waliotenda unyama huo hawajawahi kuwajibishwa. Unaweza kusimama na kusema katazo halikuwepo?
Nyakati za mwanzo kabisa za urais wake, Rais Samia Suluhu Hassan, alipohutubia Bunge kwa mara ya kwanza, alisema madai ya Katiba yamsubiri kwanza ajenge uchumi. Kuhusu mikutano alisema angekutana na vyama vya siasa na kuona namna bora ya kuendesha siasa za nchi. Rais Samia alisema Katiba isubiri. Mikutano ingoje ajadili na vyama kuona jinsi ya kuendesha siasa za nchi. Polisi walisikia. Wanakumbuka agizo la Amiri Jeshi Mkuu wa zamani na mpya hajalitengua. Bila shaka ilitakiwa itoke kauli ambayo Rais Samia aliitoa.
Dk Slaa azingatie kuwa polisi wa Tanzania hawafanyi kazi kwa weledi. Bali maagizo. Kwa mantiki hiyo, bila kauli ya Rais Samia, pengine kungetokea mauaji mithili ya Akwilina au tofauti, kama vyama vingelazimisha mikutano.
Hoja ya pili
Kuna hoja kuhusu kauli ya Rais Samia kutaka vyama vitumie fursa ya mikutano kukosoana kwa staha kwamba ni mbaya.
Kwa kumsahihisha mbunge huyo wa zamani wa Karatu, alichokisema Rais Samia sio kibaya. Ndicho kinapaswa kusemwa.
Dk Slaa amejenga hoja kuwa polisi wanaweza kuwashusha chini wanasiasa kutoka kwenye majukwaa kutokana na tafsiri yao.
Dk Slaa amesahau kwamba Rais Samia aliwasisitizia polisi kuwa jukumu lao ni kuwalinda wanasiasa na sio kuwazuia. Sijui kwa nini amesahau?.
Kwa kujenga mantiki, kauli ya Rais Samia kuhusu kukosoana kwa staha ndiyo inatakiwa. Hoja kwa hoja. Watu wafanye utafiti waibuke na agenda au hoja nzuri.
Rais Samia alisema, wakimshambulia yeye binafsi, yeye atastahilimi, lakini chawa wake nao watajibu.
Mashambulizi binafsi ya watu yataipeleka wapi nchi? Kumpa Rais majina mabaya sio siasa. Tunataka kizazi cha siasa chenye kuyaelejea masuala na kujenga hoja. Sio kushambuliana binafsi. Slaa ajue hivyo. Nchi haitaki siasa za kihuni. Siasa za kutukanana.
Mwisho, huyo ndiye Dk Slaa wa sura tatu. Wa kupindi cha Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, alikuwa mkali kivitendo. Aliibua vibomu.
Wakati wa Magufuli, alinywea. Alipopewa ubalozi, alitokeza kulaumu wapinzani kuisema vibaya nchi kwa kuwa yeye na mabalozi wengine walipata tabu kuitetea nchi kwenye jumuiya ya kimataifa.
Slaa wa Samia, ambaye alishatangaza kustaafu siasa, anarudi kwa sura tofauti. Anakuwa mshauri wa siasa zilezile za kipindi chake wakati wa Kikwete.
Anataka zile “amshaamsha” zirudi. Ndio maana kuna wanaombeza, wanamuuliza, mbona kipindi cha Magufuli hukusema?
Binafsi namtetea. Slaa wa Magufuli alikuwa Balozi Sweden. Kinidhamu hakupaswa kutoa kauli ya kumpinga bosi wake. Hivi sasa yupo huru kushauri. Yupo nje ya mfumo. Hata hivyo, ushauri uendane na hali halisi.