HOJA ZA KARUGENDO: Unataka kuwalinganisha Mandela na Nyerere? La

Juzi, Wanataaluma wa Kikatoliki (CPT) walikuwa na kongamano la miaka 20 kifo cha Mwalimu Julius Nyerere. Mada nyingi zilijitokeza na jirani yangu alinitumia ujumbe kwenye simu: “Nakuomba uandike makala ya uchambuzi juu ya Maisha ya Mandela na ya Nyerere. Tuchambulie tujue, ni nani alikuwa juu ya mwingine na ni nani alimuhitaji mwingine zaidi.”

Siandiki makala hii kufanya uchambuzi nilioombwa. Kufanya hivyo ni kuwakosea haki mashujaa hawa wa Afrika. Nina imani wao hawakuishi maisha ya ushindani; hawakuishi maisha ya kujipima na wengine kwenye nchi zao, Afrika na kwingineko.

Hawa ni wazalendo waliotoa maisha yao kupigania uhuru wa nchi zao na uhuru wa Afrika nzima. Walitoa maisha yao kupigania heshima na haki ya utu wa Mwafika na binadamu wote.

Waliishi falsafa zao za ‘ubuntu’ na ‘Ujamaa na kujitegemea’. Hawa ni mfano wa kuigwa wa Umajumui wa Afrika na itatuchukua miaka mingi kuwapata wengine.

Hivyo tusifanye dhambi ya kuwashindanisha badala ya kujifunza kutoka kwao.

Mambo ya kujifunza

Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa Mandela na Nyerere. Kosa kubwa tunalolifanya ni kuimba sifa zao, bila kuiga na kujifunza kutoka kwao.

Tunaziimba sifa za Nyerere huku tukiendelea kuutukuza udini, ukabila na kutaka kuuvunja muungano, tumeukumbatia ubepari na kukaribisha ubeberu na tunamsaliti katika maisha yetu ya kila siku!

Tuangalie tunajifunza nini kutoka kwa Mandela. Tusifanye makosa yaleyale ya kuimba sifa za Mandela, wakati tunaendelea kumsaliti kwenye maisha yetu ya kila siku. Hadi leo hii yameandikwa mengi juu ya Mandela, na mimi yaongezea.

Mandela, alipohojiwa juu ya miaka 27 aliyoishi gerezani, alisema; “Kwa wengine, miaka hiyo inaonekana mingi, lakini kwa sisi tuliokuwa gerezani, ilipita haraka sana”.

Mwandishi aliyekuwa akihojiana naye, alitaka kujua maana yake na Mandela alijibu:

“Unajua kule gerezani tulikuwa tumefungwa wazalendo wengi na tulikuwa wasomi, hivyo tulitumia muda mwingi tukitafakari na kupanga maisha ya baadaye ya Afrika Kusini. Kutafakari huku, kulitufanya tusione urefu wa miaka mingi tuliyokaa gerezani”.

“Kifungo ndicho kilinifanya kutambua kwamba mwanadamu anahitaji muda wa kutafakari. Nilishangaa ni kwa nini kabla ya kufungwa sikutambua kitu hiki, maana ningeweza kutenga muda wa kutafakari. Kusema kweli kutafakari kulinipatia nguvu na upeo mkubwa wa kutambua mambo mengi katika maisha mwanadamu...”

Mandela, anatoa mifano mingi juu ya mambo yaliyotokea gerezani na kumsaidia kutafakari kwa kina.

Mfano, anasema kuna mfungwa aliyepigwa vibaya sana na kuumizwa na Mandela hakuvumiliwa kitendo hicho. Aliamua kwenda kulalamika kwa Mkuu wa Gereza. Mfungwa huyo alipohongwa kwa kupatiwa chakula kingi zaidi ya kile alichokuwa akipata kila siku, alimgeuka Mandela na kusema Mandela alikuwa amesema uongo kwa mkuu wa Gereza. Maana yeye (mfungwa) hakupigwa wala kuumizwa.

Tukio hilo na mengine mengi ya namna hiyo, yalimuumiza sana Mandela na kumfanya kutafakari kwa undani juu ya mwanadamu, jinsi mtu anavyoweza kuhongwa ili akubali ukiukwaji wa haki zake.

Hivyo, pamoja na mambo mengine mengi tunayoweza kujifunza kwa Mandela, kama vile kuwasamehe adui zetu, tunaweza pia kujifunza hili la kutafakari.

Hatuna muda wa kutafakari juu ya maisha yetu, maana ya kuishi, kutafuta mali, kulijenga taifa bora na kulirithisha taifa kwa vizazi vijavyo.

Nina maana ya mtu kutenga muda wake mwenye na kufanya tafakuri juu yake mwenyewe, juu ya maisha kwa ujumla na juu ya mbingu na dunia, kugundua kwamba hapa duniani tunapita. Hata ukiishi miaka 95 kama ya Mandela, au zaidi, bado ni muda mfupi ukilinganisha na miaka ambayo dunia imekuwepo na itaendelea kuwepo.

Na ukigundua kwamba duniani tunapita haraka sana, ni lazima uishi kwa amani, kwa kusamehe, kwa kiasi bila kujilimbikizia vitu ambavyo havina umuhimu mkubwa katika maisha yako na kwa kushirikiana na wengine.

Tungekuwa tunatafakari, tusingeruhusu upuuzi wa kuichezea elimu ya watoto wetu, bila mfumo mzuri wa kutoa elimu na kuhakikisha wanajifunza badala ya kukariri kama kasuku. Tusingeruhusu ujangili wa kuingiza bidhaa bandia katika taifa letu.

Kwa vile hatuna muda wa kutafakari, tunafikia hatua ya kufanya kila kitu kuwa bidhaa na kukiweka sokoni. Elimu, ardhi, madini, samaki, mbuga za wanyama na hata utu tunaugeuza bidhaa na kuuweka sokoni bila kufikiri.

Madini wanachimba yanakwisha na kuacha mashimo, samaki wamevuliwa hadi wanaisha bila kuacha alama na gesi, itachimbwa na kuisha bila kuacha alama.

Hivyo,

Tusipoteze muda kuwalinganisha Mandela na Nyerere, bali tufakari juu ya maisha yao na kujifunza kutoka kwao.