Hoja za makundi, Ngorongoro zatawala uchaguzi wa CCM Arusha

Arusha. Wakati wajumbe wakijiandaa kumchagua Mwenyekiti wa CCM Mkoa Arusha, hoja za kumaliza makundi na sakata la Ngorongoro limeonekana kuteka mijadala ya wajumbe kabla ya kuanza rasmi kwa uchaguzi.
Arusha wanafanya uchaguzi huo kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mwenyekiti, Zelothe Stephen aliyefariki dunia Oktoba 26, mwaka huu.
Wajumbe wa mkutano Mkuu wa CCM Mkoa Arusha, tangu asubuhi ya leo, Desemba 4, 2023 wamejitokeza katika Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC), kushiriki uchaguzi huo.
Halimashauri Kuu ya CCM, ilipitisha majina manne, Dk Daniel Pallangyo, Thomas Ole Sabaya, Solomon Kivuyo na Edina Kivuyo lakini mchuano mkali unaonekana utakuwa kwa Dk Pallangyo ambaye aliwahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na Thomas Ole Sabaya ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Arumeru.
Sabaya ni baba mzazi wa aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.
Katibu mwenezi wa CCM Mkoa Arusha, Saipulani Ramsey amesema maandalizi yote ya uchaguzi huo yamekamilika.
"Kama ambavyo unaona wajumbe wanaendelea kuja kutoka wilaya zote za Mkoa Arusha na tunatarajia mkutano utakwenda vizuri,"amesema.
Hata hivyo, katika uchaguzi huo, ambao umetawaliwa na makundi miongoni mwa hoja ambazo zinazungumzwa ni jinsi ya kumaliza mgogoro wa Ngorongoro na kuondoa mpasuko ndani ya CCM.
Mjumbe wa mkutano huo, Jeremiah Mollel amesema miongoni mwa mambo ambayo yanatarajiwa kuwa mwiba kwa wagombea ni majibu ya kutafuta suluhu ya Ngorongoro.
"Uchaguzi huu una hoja mbili kubwa kwanza mambo ya Wilaya ya Ngorongoro pia kuvunja makundi ndani ya CCM ambayo yanatishia kuwagawa wanachama katika chaguzi zijazo,"amesema.
Mkutano huo haujafunguliwa rasmi na wajumbe wanaendelea na kampeni nje ya Ukumbi wa AICC.