INEC yaahirisha uchaguzi Fuoni, sababu yatajwa
Muktasari:
- Abbas Mwinyi ambaye ni kaka mkubwa wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, alifariki dunia jana Septemba 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Lumumba iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Dar es Salaam. Kufuatia kifo cha mgombea ubunge wa Fuoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abbas Mwinyi, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeahirisha uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo hadi pale itakapopanga tarehe nyingine ya uteuzi wa wagombea.
Abbas ambaye ni kaka mkubwa wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, alifariki dunia jana Septemba 25, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Lumumba iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Septemba 25, 2025 na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Fuoni, Miraji Mwadini Haji, amepokea barua kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar kuhusu taarifa ya kifo cha Abbas.
Amesema kutokana na kutokea kwa tukio hilo, uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Fuoni lililopo Wilaya ya Magharibi B- Zanzibar, umesitishwa kuanzia Septemba 25, 2025.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 71(2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani namba 1 ya mwaka 2024, Tume kwa notisi itakayochapishwa katika gazeti la Serikali itapanga tarehe nyingine ya uteuzi wa wagombea na taratibu za uchaguzi wa ubunge katika jimbo husika zitaanza upya.
“Hivyo, uteuzi kwa wagombea wengine ambao walioteuliwa kihalali utabaki kama ulivyokuwa awali, isipokuwa kama mgombea atajitoa na kwamba hakutakuwa na kampeni kwa wagombea ubunge katika Jimbo la Fuoni mpaka baada ya uteuzi wa mgombea mwingine,” inaeleza taarifa hiyo.
CCM yamlilia Mwinyi
Katika hatua nyingine, CCM Ofisi Kuu ya Zanzibar imeeleza kupokea kwa huzuni na masikitiko taarifa ya kifo cha Abbas kilichotokea Septemba 25, 2025 katika Hospitali ya Mkoa Lumumba, alipokuwa akipatiwa matibabu.
Chama hicho kimeeleza kwamba Abbas alikuwa ni rubani na mbunge wa Jimbo la Fuoni kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita 2020 hadi 2025 na hadi umauti unamfika alikuwa ni mgombea wa ubunge katika Jimbo la Fuoni kwa tiketi ya CCM.
“Chama cha Mapinduzi kinatoa mkono wa pole kwa familia ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, wananchi wa Jimbo la Fuoni na wafiwa wote kwa ujumla na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu wawe na moyo wa subra katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo,” inaeleza taarifa hiyo.
Abbas anatarajiwa kuzikwa leo katika makaburi ya familia huko Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini Unguja. Taarifa hiyo ya CCM inaeleza kwamba marehemu Abbas ameacha wake wawili na watoto tatu.