Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kamati Kuu NLD kujifungia siku mbili kujadili hali ya siasa

Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, akizungumza na waandishi wa habari. Picha na Mbonea Herman

Muktasari:

  • Chama cha National League for Democracy (NLD) kitaanza kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu jijini Dar es Salaam kesho kujadili hali ya siasa nchini na mikakati ya kujiimarisha.

Dar es Salaam. Chama cha National League for Democracy (NLD) kitaanza kikao cha siku mbili cha Kamati Kuu kesho Jumatano, Julai 1, 2026 jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kinajiri wakati hali ya kisiasa nchini ipo katika mjadala mpana wa zuio la mikutano ya hadhara lililotangazwa wiki iliyopita, hatua iliyotajwa na Serikali kuwa ni tahadhari ya kiusalama nchini.

Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano ya Umma wa chama hicho, Pogora Ibrahim leo Jumanne, Juni 30, 2026 amesema kikao hicho kitahusisha wajumbe wa kamati kuu pamoja na viongozi wengine wa chama.

Katika taarifa hiyo, Pogora amesema kikao hicho kitajadili tathmini ya hali ya chama baada ya uchaguzi, hali ya kisiasa nchini, ujenzi na uimarishaji wa chama pamoja na mafunzo kwa viongozi.

"Pamoja na kujadili hali ya chama baada ya uchaguzi, kikao kitatoa nafasi ya mafunzo kwa viongozi, wajumbe wa Kamati Kuu na watendaji wa ofisi kuu ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya chama," amesema Pogora katika taarifa hiyo.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu kikao hicho, Katibu Mkuu wa chama hicho na mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Doyo Hassan Doyo, amesema tathmini ya uchaguzi ni ajenda muhimu kwa sababu itawezesha chama kupima kwa kina utendaji wake, kubaini mafanikio na changamoto pamoja na kuweka mikakati mipya ya kujiimarisha kisiasa.

Amesema kikao hicho kinalenga kujenga msingi wa mageuzi ya ndani yatakayokifanya chama kiwe na uwezo mkubwa zaidi wa kuwafikia wananchi na kujiandaa kwa ushindani wa kisiasa wa siku zijazo.

"Tunataka kikao hiki kiwe mwanzo wa hatua mpya za kukiimarisha chama, kuongeza mshikamano wa viongozi na wanachama pamoja na kuweka mikakati itakayokifanya NLD kiwe chama imara na chenye ushawishi mkubwa zaidi katika siasa za Tanzania," amesema Doyo.

Kuhusu ajenda ya hali ya kisiasa nchini, Doyo amesema viongozi wa kamati kuu watajadili mazingira ya kisiasa yaliyopo, nafasi ya vyama vya siasa katika kuimarisha demokrasia na namna ya kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika mfumo wa kisiasa.