Katavi, Songwe wapata wenyekiti wapya CCM
Baadhi ya wajumbe wa CCM mkoa wa Katavi wakishangilia ushindi wa viongozi waliowachagua. Picha na Mary Clemence
Katavi/Songwe. Msimamizi wa uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Katavi, Wazizi Kidamba amemtangaza Idd Hassan Kimanta kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho mkoa wa Katavi.
Kimanta amepata kura 308 dhidi ya mpinzani wake, Juma Said Kaombwe aliyepata kura 44.
Kimanta anachukua nafasi inayoachwa na Beda Alfred Katani ambaye jina lake lilikatwa na halmashauri kuu ya Taifa.
Akitangaza matokeo hayo katika uchaguzi uliofanyika leo Jumatatu Novemba 21, 2022 katika ukumbi wa madini Manispaa ya Mpanda, Kidamba amesema idadi ya wajumbe ilikiwa 368 waliopiga kura ni 359 halali 352 zilizoharibika ni 7.
Nafasi ya Mjumbe wa halmashauri kuu CCM, NEC Gilbert Jordan Sampa ametetea kiti chake baada ya kupata kura 357 akimbwaga chini mgombea mwenza Buhura Chasama aliyepata kura 7 kati ya kura halali 364.
"Idadi ya wajumbe ilikiwa 368 zilizoharibika ni 2 hivyo Sampa ameshinda sawa naasilimia 97.01," amesema Kidamba.
Viongozi hao baada ya kutangazwa wamesisitiza kuimarisha umoja na mshikamamo katika chama wakidai hawatasita kuwachukulia hatua wanachama watakaoleta makundi yenye nia ovu.
Huko mkoani Songwe, msimamizi wa uchaguzi huo Jumaa Homera amemtangaza Radwell Mwampashe kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa baada ya kupata kura 415 na kuwashinda wapinzani wake Kissa Kibona aliyepata kura (104) na Isabela Mbaya aliyepata kura (27).
Mwampashe anachukua nafasi ya Ellynico Mkola ambaye alipojitosa kugombea nafasi hiyo jina lake naye lilikatwa.
Katika nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia mkoa Homera amemtangaza Aden Mwakyonde aliyepata kura 328 na kuwashinda wapinzani wake wawili Ombeni Nanyalo aliyepata kura (211) na Stansraus Nsojo.